Jeshi
la Polisi Zanzibar litamhoji Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif
Hamad Ijumaa ya wiki hii kuhusu masuala mbalimbali ambayo hata hivyo,
hayakuwekwa wazi.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Makame alisema jana: “Natambua kuwa wasaidizi wangu watazungumza naye Ijumaa. Wao ndiyo wanajua watamhoji nini.”
Alipoulizwa
kuhusu mahojiano hayo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
Zanzibar, Salum Msangi naye hakuweka wazi badala yake alisema kuna
masuala mengi ambayo ofisi yake inahitaji kuyafahamu kutoka kwa Maalim
Seif.
Hii
ni mara ya kwanza kwa Maalim Seif kuhojiwa na polisi tangu kumalizika
kwa Uchaguzi Mkuu ambao kwa Zanzibar ulirejewa Machi 20, baada ya ule wa
Oktoba 25 mwaka jana kufutwa.
Maalim
Seif ambaye kabla ya uchaguzi huo alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar, alipinga kurudiwa kwa uchaguzi huo msimamo ambao pia
ulichukuliwa na chama chake.
Kiongozi huyo amekuwa akitoa matamko kadhaa ya kuwashawishi wananchi kupinga utawala wa Serikali iliyopo madarakani.
Akiwahutubia
wafuasi wake huko Pemba hivi karibuni, Maalim Seif alisema Serikali ya
CCM imeanza kutikisika kutokana na vikwazo vinavyoendelea kuwekwa na
wahisani pamoja na hatua ya chama chake CUF kutowatambua viongozi wake
pamoja na Serikali.
“CCM
wajue wamekalia kuti kavu, siku yoyote wataanguka... tufanye kazi mpaka
haki yetu tuhakikishe imerudi na wenzetu hawana safari ya kudumu,” alisema.
Aliwataka
wanachama wake kuonyesha kwa vitendo kutoitambua Serikali ikiwamo
kukataa kulipishwa kodi za ovyovyo pamoja na kujitenga na viongozi wa
Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Mfano
tunaweza kuamua siku fulani kuanzia saa sita, tunasimamisha vyombo
vyote vya usafiri na siku nyingine tunaamua kupiga honi Zanzibar nzima
kuonyesha hatuitaki Serikali ya CCM,” alisema huku akishangiliwa na umati uliofurika katika ofisi za chama hicho.
Mapema
jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema kuwa
amesikia juu ya wito huo lakini hakuwa amepata taarifa rasmi kutoka kwa
mkuu wake.
“Nimesikia kama mlivyosikia ninyi,” alisema na kuongeza: “Nimeelezwa pia hata leo Kamishna wa Polisi Zanzibar alikuwa na mahojiano naye.”
Kuhusu hilo Kamishna Makame alisema: “Sijaonana wala kuzungumza naye leo. Hiyo si kweli.”
Juzi,
wakati akizindua ripoti ya Uvunjifu wa Haki za Binadamu uliofanyika
visiwani humo kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Naibu Katibu Mkuu
wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema wanazo taarifa za Serikali
kutaka kuwakamata viongozi waandamizi wa chama hicho na kuwashikilia.
Alisema wamebaini mpango wa kukamatwa kwao na kuwekwa kwenye Mahakama za bara ili kuwanyamazisha Wazanzibari.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment