Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema mikataba
yote ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni za kufua umeme
siyo mizuri na haina manufaa yoyote kwa Taifa.
Profesa Muhongo
alisema hayo juzi wakati akijibu hoja ya kuongezeka kwa deni la Tanesco
iliyotolewa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika wizara hiyo, John
Mnyika.
Kambi ya upinzani imekuwa ikisema mikataba ya Tanesco
haina tija kwa Taifa na imekuwa ikiliua shirika hilo. Katika hotuba
yake, Mnyika alisema Tanesco imekuwa ikiilipa IPTL Sh300 milioni kwa
siku kama gharama za uendeshaji.
Profesa Muhongo alikiri kwamba
ni kweli deni la Tanesco ni kubwa na limesababishwa na uongozi dhaifu,
rushwa, wizi na mikataba mibovu ambayo Tanesco imeingia.
Alisisitiza kwamba hakuna mkataba unaolinufaisha Taifa.
“Lazima
niseme ukweli, mikataba yote ya Tanesco siyo mizuri. Tumekuwa
tukiwalipa Songas gharama za uendeshaji Dola 4.6 milioni; IPTL
tunawalipa Dola 2.6 milioni; Agreco tunawalipa Dola 2.0 milioni. Hakuna
mkataba wenye manufaa kwa Taifa,” alisema Profesa Muhongo na kuahidi
kwamba wizara yake itachukua hatua ili kulinusuru shirika hilo na mzigo
huo wa madeni kila mwezi.
Alisema wizara yake imeanza utaratibu
wa kufanya tathmini ya utendaji wa wafanyakazi wa Tanesco ili
kuhakikisha wanatoa huduma bora.
Alisema tathmini hiyo inafanywa kwa
mameneja wa Tanesco kwa kuangalia wameingiza kiasi gani na wameunganisha
wateja wangapi.
“Kila baada ya miezi mitatu tunafanya tathmini
ya mameneja wetu na mwezi wa sita tutafanya tathmini ya pili. Wapo ambao
walishindwa kukidhi vigezo katika tathmini iliyopita, wameondolewa,”
alisema waziri huyo.
Kuhusu suala la umeme vijijini, Profesa
Muhongo alisema Hazina imetoa Sh70.2 bilioni kwa ajili ya kumalizia
utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa umeme vijijini, unaosimamiwa na
Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).
Jambo hili lililalamikiwa na
wabunge wengi wakisema wakala huyo anashindwa kutekeleza majukumu yake
kwa sababu fedha zake hazitolewi na Serikali.
Walishauri fedha za Rea
ziwekwe katika akaunti yake maalumu bila kupitia Hazina. Hata hivyo,
Profesa Muhongo alilihakikishia Bunge kwamba miradi yote iliyobaki
katika awamu ya pili ya Rea itakamilika kufikia mwisho wa mwezi ujao.
Alisema
miradi ya Rea haitatetereka kwa sababu ya Shirika la Changamoto za
Milenia la Marekani (MCC) kusitisha kutoa misaada kwa Tanzania akisema
Serikali imejipanga kusimamia miradi ya maendeleo bila kutegemea misaada
ya wahisani.
“Tumeanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta (Pura).
Wakala huyu atakuwa na jukumu la kusimamia mikataba yote ya mafuta na
atasimamia pia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),” alisema
Profesa Muhongo.
Kuhusu suala la migodi kutolipa kodi, waziri
huyo alisema ni kweli mingi hailipi na kusema ameanza kusimamia suala
hilo na kuwa wote lazima walipe kodi.
Alisema Serikali pia
itawalipa fidia wakazi wa Lindi katika eneo ambalo kitajengwa kiwanda
cha kupakia gesi (LNG). Alisema fedha zipo na vijana wakasome Veta ili
wapate ajira katika kiwanda hicho.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment