Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.
SUKARI iliyoagizwa na serikali kutoka nje kwa ajili ya kujazia uhaba
wa sukari kwa mfumo rasmi, imewasili nchini na tani takribani 12,000
zitaanza kusambazwa leo katika maeneo mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na waandishi wa habari
nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana, alisema kuna upungufu wa
sukari kwa mfumo rasmi, lakini serikali ilichukua hatua ya kuhakikisha
inapatikana sukari kufidia uhaba huo na kuwa suala la sukari lisionekane
kuwa tatizo kubwa.
“Sukari ipo lakini sio kwa kiwango halisi kinachopaswa kuwepo, lakini
kama wafanyabiashara wangefanya biashara ya kuuza sukari kwa utaratibu
mzuri uliowekwa wangekwenda sambamba na mfumo rasmi wa kuagiza sukari
kujazia uhaba uliopo,” alisema Majaliwa.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, kiuhalisia zinahitajika tani 420,000
lakini uwezo wa viwanda vya ndani kuzalisha ni tani 320,000 kwa hiyo
kuna upungufu wa tani 100000 na ndio maana serikali imelazimika kuagiza
nje kufidia upungufu huo.
Alisema mkakati wa serikali ni kuimarisha viwanda vyake vya kuzalisha
sukari, sambamba na kudhibiti sukari ya nje kuvifanya viwanda vya ndani
vinakuwa na uwezo wa kuzalisha sukari ya kutosha pamoja na kuhamasisha
wananchi kuwa na utamaduni wa kutumia bidhaa yao ya ndani.
Tani 11,957 zatua “Lakini tumechukua hatua kwa sasa kuagiza sukari
nje tani 70,000 kujazia upungufu huo kwa sababu kwa sasa hivi viwanda
vyetu havina uwezo wa kuzalisha sukari ya kutosha, vipo vingine
vinahitaji kuboreshwa ama kukarabatiwa kabla havijaanza kazi,” alieleza
Waziri Mkuu.
Alisema katika kujazia upungufu huo, tayari serikali imeingiza tani
11,957 ambazo zimeshawasili na zitaanza kusambazwa leo kikanda pamoja na
kiwango cha tani kwenye mabano mikoa ya Kaskazini (tani 2,000), Kanda
ya Ziwa (tani 3,000), Kusini (2,000), Nyanda za Juu Kusini (2,000) na
Kanda ya Kati (2,000).
Alisema tani nyingine 24,000 za sukari, zinatarajiwa kuwasili Ijumaa
hii na kwamba hadi kukamilisha taratibu na kutoka bandarini itakuwa kama
Jumapili, hivyo zinaweza kusambazwa kuanzia Jumatatu ijayo.
Waziri Mkuu alisema pia tani nyingine 20,000 zitawasili baadaye
mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwezi ujao na kwamba serikali inaamini
upungufu uliokuwepo, utakuwa umejaziliziwa vizuri wakati ikitarajia
ifikapo mwezi Julai viwanda vya ndani vitakuwa katika hali nzuri ya
kuanza uzalishaji.
“Watanzania wasiwe na wasiwasi kuhusu uhaba wa sukari uliojitokeza
hivi karibuni kwani umesababishwa na watu wachache. Rais amekuwa makini
kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na uhaba huo ikiwa ni pamoja na
kuagiza waliohodhi bidhaa hii wakamatwe na sukari isambazwe,” alisema.
Awabana wafanyabiashara Waziri Mkuu aliwataka wafanyabiashara na
wasambazaji wa sukari, watoe sukari na kuuzia wafanyabishara wadogo ili
wao wauze kwa wananchi kwa bei elekezi ya Sh 1,800, sambamba na kuwataka
wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, kuhakikisha wanaendelea kusaka na
kufichua watu walioficha sukari kwenye maghala yao.
Alisema serikali imeanza mkakati wa kuhakikisha uzalishaji wa sukari
nchini unaongezeka kwa kuweka utaratibu mzuri wa namna wazalishaji wa
ndani wanaweza kuzalisha katika viwanda vyao ili ifikapo mwaka 2019
tatizo la uhaba wa sukari liwe limemalizika.
Waziri Mkuu alisema mkakati mwingine wa serikali, kuboresha viwanda
vya ndani na wamiliki wa viwanda pamoja na kualika wawekezaji kutoka nje
ili waje kuwekeza hapa nchini kwenye viwanda vya sukari.
“Serikali ina maeneo matatu makubwa yako Bagamoyo, Ngerengere
(Morogoro) na Kigoma, huku serikali ina mashamba makubwa ambapo
mwekezaji atakayevutiwa anaweza kuja kupitia Kituo chetu cha Uwekezaji
na kuona namna wanavyoweza kuwekeza katika sekta hii,” alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa aliongeza kuwa kazi ya kufichua wafanyabiashara,
wanaohodhi sukari nchini kwa nia ya kujinufaisha na kutaabisha
Watanzania ni endelevu, lakini pia viwanda vya ndani vitakapoanza
kuzalisha, serikali itaendelea kuhakikisha inadhibiti uingizaji wa
sukari kutoke nje.
Dar yanasa tani nyingine
Mkoani Dar es Salaam, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa
ikishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, jana ilikamata sukari
iliyokuwa imefichwa katika ghorofa moja lililopo wilaya ya Kinondoni
eneo la Hananasif.
Sukari hiyo ambayo ni mifuko 160 yenye ujazo wa kilo 25, ilikamatwa
baada ya kufanyika kwa msako katika nyumba hiyo inayomilikiwa na Bashiru
Ismail baada ya kamati hiyo kupata taarifa kuhusu uwepo wa sukari hapo.
Mbali na kukamatwa kwa sukari hiyo katika Manispaa ya Kinondoni, pia
kumebainika kuwepo sukari tani 52,000 zilizofichwa na mfanyabiashara
ambaye anahangaika kuzificha. Akizungumza baada ya kufanya ziara ya
kushtukiza, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa, Paul
Makonda alisema kukamatwa kwa sukari hiyo ni jitihada za kufuata agizo
la Rais la kuwataka kuwafuatilia wafanyabiashara wanaoficha sukari na
kusababisha wananchi wa hali ya chini kukosa bidhaa hiyo.
“Ni kosa kuhodhi bidhaa hii watu wasichukulie upungufu uliopo na
kufanya wanayoyafanya wafanyabiashara wanatumia nguvu ili tuonekane
hatuna uwezo wa kusambaza sukari,” alisema Makonda na kutoa mwito kwa
wananchi kuwa sehemu ya kuwafichua wafanyabiashara wanaoficha sukari na
kutoa taarifa kwa Dola.
Kwa upande wake, mmiliki wa jengo hilo, alisema sukari hiyo siyo ya
biashara bali ni kwa ajili msaada ambao amekuwa akigawa kwa vituo vya
watoto yatima waliopo katika vituo mbalimbali na watu wasiojiweza.
Alisema ina miezi sita hapo na kwamba yupo tayari kuchunguzwa kama
anauza.
Mbunge, Zakaria matatani tena
Nayo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa
ushirikiano na Jeshi la Polisi, wametoa saa 36 kwa Kampuni ya Al Naeem
yenye sukari tani 1,840 zilizo bandarini, ziwe zimeingia sokoni na
kuuzwa kwa bei elekezi.
Agizo hilo lilitolewa jana Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa
Takukuru, Leonard Mtalay wakati taasisi hiyo na Jeshi la Polisi
walipofanya ziara ya ghafla katika bandari ya Dar es Salaam ili kubaini
ukweli wa taarifa za uwepo wa sukari iliyokaa muda mrefu bila kuingizwa
sokoni.
“Tulipata taarifa kutoka kwa msiri wetu kuwa kuna sukari iko
bandarini imehodhiwa na mfanyabiashara Turky (Salim Hassan- Mbunge wa
Mpendae), ambaye hataki kuingiza sokoni na sisi kwa ushirikiano na
Polisi tulifanya uchunguzi wetu na tulibaini ni kweli sukari hiyo ipo
kontena 70,” alisema Mtalay.
Alisema katika uchunguzi wao, walimuuliza mfanyabiashara Turky kuhusu
sukari hiyo na alikiri ni yake na katika uchunguzi wao walibaini pia
kuwa sukari hiyo ilikuwa na mchakato mrefu wa kulipiwa kodi na kupata
vibali.
“Tumebaini mengi, kuagiza sukari kunahitaji vibali na tumejiridhisha
kuwa sukari hii imeshalipiwa kodi hivyo inatakiwa kuondolewa hapa na
tumewapa Kampuni ya Al Naeem ambao ndio wanaonekana kuwa wamiliki wa
sukari hii saa 36, kuanzia sasa, wawe wamefikisha sukari sokoni na kwa
bei elekezi,” alisisitiza Mtalay.
Utata wa muda Hata hivyo, katika hali ya kushangaza Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Kampuni ya Al Naeem pamoja na Kitengo cha Huduma ya
Makontena Bandarini (TICTS), kila mmoja alitoa taarifa inayokinzana na
mwenzake kuhusu ukweli wa muda ambao sukari hiyo imefika bandarini hapo.
Kwa upande wa TRA, Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
Jockton Kyamuhanga alisema sukari hiyo ina zaidi ya mwezi mmoja iko
bandarini huku wamiliki wake wakifanya taratibu za kuitoa.
“Kampuni ya Al Naeem na patna wake Turky wanahusika na mzigo huo na
taratibu za kutoa sukari hii zimechukua muda wa kama mwezi, vibali vyote
vilikamilika tangu Ijumaa wiki iliyopita, sasa wanamalizia hatua za
mwisho za kuiondoa bandarini,” alisema Kyamuhanga.
Alisema sukari hiyo haikuagizwa kutumika nchini, bali ilikuwa
ipelekwe Bujumbura, Burundi na kwamba wahusika waliona hali ya siasa sio
nzuri nchini humo na hivyo wakaiuza hapa nchini.
“Ni kweli sukari hii ilikuwa inapelekwa Burundi, ila mwenye mzigo
alisema hali ya usalama na siasa nchini humo sio nzuri hivyo aliamua
kuiuza kwa Al Naeem na huyo patna wake,” alisema Kyamuhanga.
Turky anena
Akizungumza na vyombo vya habari kwenye ukaguzi huo bandarini hapo,
Turky alikana kuhusika na sukari hiyo na kusema yeye ni patna na mmiliki
wa Kampuni ya Al Naeem, Haruni Zakaria.
“Mimi sihusiki na sukari hii, ila niko hapa kwa sababu mmiliki wa
Kampuni ya Al Naeem ni patna wangu katika biashara, na nimekuja
kumsaidia baada ya kusikia kuna vikwazo vya kutoa sukari, ila utaratibu
umekamilika na sukari itatolewa na itakuwa sokoni,” alisema mbunge huyo
wa CCM.
Aliongeza kuwa sukari hiyo ilikuwa inakwenda Burundi, lakini hali
mbaya ya siasa nchini humo, imefanya sukari hiyo ibaki nchini na
kutafutiwa vibali ili itolewe na kuuzwa hapa hapa nchini. “Ni miezi
mitatu sasa sukari hii imefika hapa bandarini, ilikuwa sio ya hapa
ilikuwa inaenda Burundi ila hali ya siasa sio nzuri na ndio tumeitafutia
vibali ibaki nchini,” alidai Turky.
Meneja ya Al Naeem anena
Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya Al Naeem, Naeem Zakaria
aliyekuwepo eneo la ukaguzi alisema wao walinunua sukari hiyo Februari
mwaka huu na Machi mwaka huu, walilipia ushuru.
Aidha, kibali cha kuingiza sukari walikipata Mei 5, mwaka huu na
vibali vingine vya ukaguzi wa ubora wa bidhaa hiyo kikiwemo kibali cha
Shirika la Viwango Tanzania (TBS), walikipata Mei, 9 mwaka huu; hali
inayozua maswali mengi kwa nini kama bidhaa hiyo haikupata vibali muda
wote huo.
“Hizo zote hapa nilizo nazo ni vielelezo vya sukari hii, kampuni
ilinunua sukari kutoka kwa kampuni ya India iliyokuwa ikipeleka sukari
hii Burundi, sisi tumeinunua Februari mwaka huu, na Machi ndio tumelipia
ushuru na Mei tukapata vibali, na jana Jumatatu (juzi) ndio tumepata
kibali cha TBS,” alisema Zakaria.
Alisema kampuni hiyo ya India waliwafuata wenyewe ili wawauzie sukari
hiyo kwa madai kuwa Burundi kuna machafuko hivyo hawawezi kuipeleka na
kwamba baada ya kuinunua wamelipa kodi na tozo zote na sasa wanasubiri
kuitoa sukari hiyo.
TICTS wanasemaje?
Kwa upande wao, TICTS walizungumzia muda sukari hiyo ilipoingia na
kueleza kuwa ina miezi mitano tangu imeingia nchini na kwamba katika
nakala za sukari hiyo zilionesha inakwenda Burundi.
Mkurugenzi wa Biashara na Maendeleo wa TICTS, Donald Talawa alisema
wao walipokea sukari hiyo miezi mitano iliyopita na kwamba nakala za
sukari hiyo iliyozalishwa Brazil, zinaonesha kwamba ilikuwa inakwenda
Burundi.
“Sisi tulitoa kontena 70, ambazo 30 ziko hapa na nyingine 40 ziko
bandari kavu yetu ya Ubungo, mara baada ya kuzipokea siku 21 zilipita
bila mwenye mzigo kuutoa na sisi kama sheria inavyoelekeza tulikabidhi
kontena hizo TRA,” alisema Talawa na kusisitiza kuwa kontena hizo
zimekaa bandarini hapo bila kutolewa zaidi ya miezi mitano na sio mwezi
mmoja na kwamba wao walishazikabidhi kwenye mamlaka husika kwa hatua
zaidi.
Agizo la Takukuru Akitoa agizo la sukari hiyo kuwa sokoni kuanzia
leo, Mtakay alisema ni vyema wafanyabiashara wakatii maagizo ya serikali
na kuacha tabia ya kuficha sukari, bali waitoe na kuuza kwa bei elekezi
ya Sh 1,800, vinginevyo wakibainika bidhaa hiyo itataifishwa na
kugawiwa kwa wananchi.
Habari hii imeandikwa na Angela Semaya, Sophia Mwambe na Ikunda Erick.
Chanzo Habarileo.
Tuesday, 10 May 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment