Mkazi wa Kijiji cha Chala B, Tarafa ya Chala wilayani Nkasi, Mkoa wa
Rukwa, Moses Nambasita (48) ameuawa kwa kuchomwa visu kutokana na
kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Akisimulia
mkasa huo
mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Vincent
Mwanambuu alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 10 jioni baada ya
kuvamiwa na kijana mmoja alipokuwa akitoka nyumbani kwake kwenda nyumba
jirani, alishambuliwa kwa kuchomwa visu.
Mwanambuu alisema
baada ya kupata taarifa hizo alitoa taarifa Kituo kidogo cha Polisi
Chala, askari walifika na kuchukua mwili kwa ajili ya uchunguzi na
kuanza msako dhidi ya mtuhumiwa.
Akielezea chanzo cha mauaji
hayo, Mwanambuu alisema mtuhumiwa alipata taarifa kuwa Nambasita ana
uhusiano na mtalaka wake, ambaye walikuwa wameachana kipindi kirefu.
Alidai kuwa kutokana na taarifa hizo, mtuhumiwa alipeleka shauri la ugoni katika Mahakama ya Mwanzo Chala.
“Lakini
kabla hata shauri hilo halijamalizika, tunashangaa kuona mtuhumiwa
ameamua kujichukulia sheria mikononi, baada ya kutekeleza unyama huo
alikimbia na kutokomea kusikojulikana,” alisema.
Mtendaji wa
Kijiji cha Chala, Godfrey Mwanakatwe alisema kutokana na mazingira hayo
polisi wanawashikilia watu wanne kwa kosa la kushiriki mauaji hayo.
Hatua
hiyo inatokana na baada ya wao kutoa taarifa kwa muuaji kuwa Nambasita
ana uhusiano wa kimapenzi na mtalaka wake, ambaye mpaka sasa haijulikani
alipo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba, baada ya uchunguzi wa
polisi ndugu wa marehemu waliruhusiwa kuuzika mwili huo.
Mwaruanda
alisema chanzo cha kifo hicho ni wivu wa mapenzi na kuongeza kuwa
mtuhumiwa alianza vizuri kwa kufuata sheria, lakini haijulikani
kilichosababisha kuchukua uamuzi huo wa kinyama.
Alisema
wanawashikilia watu watatu wakituhumiwa kushiriki mauaji hayo, kwa kutoa
taarifa kwa mtuhumiwa kwamba Nambasita alikuwa na uhusiano na mtalaka
wake.
Kamanda Mwaruanda aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi, hivyo wafuate taratibu kupata haki zao.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment