WAKATI abiria wa mabasi yaendayo haraka wanaanza kulipa nauli leo na
kuingia katika vyombo vya usafiri kwa foleni, imebainika kuwa mfumo wa
uchanjaji kadi haujakamilika, hali itakayowalazimu abiria kutumia tiketi
za kawaida.
Mfumo wa kuchanja kadi unamwezesha mtumiaji kuweka tiketi au kadi
katika eneo maalumu la mashine ya utambuzi, ambapo inatambuliwa na
kumwezesha abiria kuingia katika kituo cha daladala kusubiri usafiri ama
kutoka.
Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo ameziagiza mamlaka zote zinazohusika
na mfumo huo wa kuchanja kadi kukamilisha haraka ili zianze kutumika.
Mamlaka zinazohusika na mfumo wa kuchanja kadi ni Wakala wa Mabasi
yaendayo Haraka (DART), Kitengo cha Serikali Mtandao, Benki Kuu (BoT) na
Wakala wa huduma za mtandao (MaxMalipo).
Akitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam, Jaffo alisema ni vema
mamlaka hizo zikahakikisha zinakamilisha mfumo huo haraka kuondoa ujanja
wa watu kusafiri bila kulipa nauli.
“ Nawataka wakamilishe mfumo huu mara moja, kwanza itaondoa matumizi
ya karatasi ambazo zinachafua mazingira, lakini pia utafanya baadhi ya
watu kusafiri bila kukata tiketi alisema,” alisema Jaffo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya UDA-RT, David Mgwasa alisema kwa
sasa abiria watalazimika kukata tiketi zenye alama maalumu
zitakazotumika mpaka hapo mfumo wa kuchanja tiketi utakapokamilika,
ambayo ni zaidi ya siku tano zijazo.
“ Kadi tunazo, lakini hatuwezi kuanza kuuza kwa sasa mpaka hapo mfumo
wa kuchanja kadi utakapokamilika,” alisema. UDA-RT imeanza kutoa huduma
ya mabasi ya haraka siku saba zilizopita na kwa siku sita mfululizo
ilitoa huduma hiyo bure kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu
matumizi ya huduma hiyo.
Aidha, Jaffo alitaka vyombo vya usalama kutofumbia macho wananchi
wanaotumia miundombinu ya mabasi yaendayo haraka kufanya uhalifu na
kutaka kuudhibiti katika vituo vya mabasi hayo.
Onyo hilo limetokana na ombi la Joseph Kinyamagoha, mkazi wa Kimara
aliyetaka kuwepo ulinzi kutokana na watu wengi kuibiwa wakati wa
majaribio ya utoaji wa huduma hiyo.
“ Yeyote atakayekutwa anafanya
uhalifu katika vituo hatafumbiwa macho, tutawakamata na tusije
kulaumiana, onyo hili pia linakwenda kwa wananchi wenye vyombo vya moto
ambao wanatumia miundombinu hii, hatutawafumbia macho,” alisema Jaffo.
Aliwataka UDA-RT kuhakikisha wanaweka mfumo utakaohakikisha wananchi
wanapanga foleni wakati wa kuingia kwenye mabasi, jambo ambalo pia
litapunguza tabia ya udokozi kwenye mabasi hayo.
Pia, aliitaka DART kutumia changamoto zilizojitokeza katika awamu ya
kwanza ya mradi huo kama somo pindi wanapotekeleza awamu ya pili ambayo
ujenzi wake unatarajia kuanza muda wowote mwaka huu na pamoja na awamu
ya tatu.
Katika hatua nyingine, Mgwasa alisema leo huduma hiyo itaanza saa
11:00 alfajiri hadi saa sita usiku na mabasi 105 yatatatoa huduma katika
njia kuu nne.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Peter Sima alisema jeshi limejipanga kuimarisha ulinzi katika
miundombinu ya mabasi yaendayo haraka huku akiwataka wananchi kutumia
maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuvuka.
“ Watembea kwa miguu wanatakiwa kutumia alama zilizowekwa kwa ajili
ya kuvuka. Ni marufuku pikipiki kutumia maeneo hayo na hata mwenye
baiskeli anatakiwa kushuka anapovuka, ukikamatwa unavunja sheria za
barabarani hutafumbiwa macho,” alisema Sima.
Mabasi hayo yamegawanyika katika aina mbili; ya haraka (express)
yatakayosimama katika vituo takribani sita na ya kawaida yatakayosimama
kwenye kila kituo.
Mabasi hayo yatafanya safari kati ya Kivukoni na Ubungo, Kivukoni na
Kimara Mwisho, Kivukoni na Morocco, pia yapo yatakayofanya safari kati
ya Kariakoo na Ubungo, Kariakoo na Kimara Mwisho; kati ya Kariakoo na
Morocco, Morocco na Kimara Mwisho na kati ya Mbezi Mwisho na Kimara
Mwisho.
Nauli kwa huduma hiyo ni Sh 400 kwa njia ya pembezoni (Mbezi- Kimara
Mwisho), Sh 650 kwa safari za njia kuu huku wale wa njia kuu na
pembezoni (Mbezi-Kivukoni au Kariakoo) ikiwa Sh 800.
Chanzo HabariLeo.
Sunday, 15 May 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment