Kwa mara nyingine jana wakazi wa Jiji la Tanga walikumbwa na taharuki
baada ya kijana mmoja kurusha bomu la mkono chini ya daraja wakati
wananchi walipokuwa wakimfukuza baada ya kukurupushwa na polisi.
Kamanda
wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paulo alisema kijana huyo alikurupushwa
na askari waliokuwa kwenye msako wa kuwatafuta majambazi waliofanya
mauaji Aprili 20, mwaka huu katika duka la Central Bakery.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi saa mbili usiku kwenye Mtaa wa Makora, Tarafa ya Ngamiani.
Awali,
Kamanda Paulo alisema kijana huyo anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya
25 na 30, alipokurupushwa alianza kutimua mbio.
“Alipoanza kukimbia
ndipo wananchi wakaingilia kati, walimfukuza na kumshambulia kwa mawe
huku wakimpiga na kitu chenye ncha kali kisogoni, ndipo wakati
akipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo akafariki dunia njiani,”
alisema Kamanda Paulo.
Mapema kabla hajafariki dunia, kamanda alisema kijana huyo alipokurupushwa alikimbia akiwa ameshikilia bomu mkononi.
Kamanda
aliwataka wakazi wa Tanga kuwa watulivu kwa sababu vyombo vya dola viko
katika operesheni maalumu ya kuwasaka walioshiriki mauaji ya hivi
karibuni katika hilo la mikate.
Walioshuhuda tukio hilo walisema
kijana huyo alishambuliwa na wananchi baada ya kukwapua simu ya
mwanamke mmoja katika Mtaa wa Makorora.
Walisema alianza
kukimbia na alipoona wananchi wanamfukuza aliwatahadharisha kuwa
wakimsogelea atarusha bomu alilokuwa amelishika mkononi.
Kufuatia
kutishiwa na bomu hilo, wananchi waliokuwa wakimkimbiza walipiga simu
Kituo Kikuu cha Polisi cha Chumbageni kwa ajili ya kupatiwa msaada.
“Kwa
hili tunawapongeza polisi. Walitumia dakika chache kufika eneo la tukio
lakini walipobaini kwamba ni bomu, wakaamua kuwasiliana na maofisa
wataalamu wa kutegua mabomu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) ambao
waliwasili eneo la tukio,” alisema Rajabu Hamis.
Wakizungumza
kuhusu tukio hilo, baadhi ya wakazi wa Tanga waliomba vyombo vya ulinzi
na usalama kuimarisha ulinzi kwa sababu wamejawa na hofu, kwa kuwa
matukio yanayohatarisha amani yanazidi kutokea.
“Hii ni
changamoto kwa vyombo vya ulinzi na usalama, matukio haya yanazidi
kuwapa hofu wananchi. Mwezi uliopita yalifanyika mauaji makubwa Central
Bakery, leo bomu tena,” alisema Kassim Mbughuni.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment