Tuesday, 17 May 2016

Tagged Under:

Mahakama Kuu yatupilia mbali kesi ya Kafulila

By: Unknown On: 22:35
  • Share The Gag

  • Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.

    MAHAKAMA Kuu , Kanda ya Tabora imetupa maombi ya aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR – Mageuzi, David Kafulila ya kutaka Mahakama itengue matokeo yaliyompa ushindi Hasna Mwillima badala yake imtangaze yeye kuwa mshindi.

    Katika kesi hiyo Namba mbili ya mwaka 2015, iliyokuwa ikisikilizwa mjini Kigoma, Jaji Ferdinand Wambari alisema baada ya kupitia vipengele vinne ambavyo ndiyo msingi wa kesi hiyo, ameridhika kwamba hakuna mahali popote ambapo ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, unaonesha kuwa taratibu za uchaguzi zilizomtangaza Mwillima kuwa mshindi zilikiukwa.

    Akisoma vipengele hivyo kimoja baada ya kingine, Jaji Wambari alisema kuwa katika kipengele cha kwanza ambacho Kafulila alilalamikia taratibu za kuhesabu kura, hakuna mahali ambapo ushahidi unaonesha kuwa zilifanywa kinyume na sheria na taratibu za uchaguzi.
    Alisema watu wote wakiwemo mashahidi wake ambao walikuwa mawakala, wanakiri kuwa taratibu hizo zilifuatwa. Aidha katika kipengele cha pili ambacho Kafulila alikuwa anamlalamikia Msimamizi wa Uchaguzi katika jimbo hilo, Reuben Mfune; aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza kuwa alishinikizwa kumtangaza Mwillima kuwa mshindi wakati msimamizi huyo akijua kwamba yeye Kafulila ndiye.
    Kafulila alimlalamikia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya, Mkuu wa Wilaya Uvinza, Mrisho Gambo na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Uvinza, James Manyama. Hata hivyo, Jaji Wambari katika uamuzi, alisema hakuna shahidi yeyote miongoni mwa mashahidi wa mlalamikaji aliyeeleza kuhusu hilo na kuthibitisha tuhuma hizo; jambo alilosema lalamiko hilo halina msingi.

    Jaji Wambari ametupilia mbali lalamiko la tatu la Kafulila aliyekuwa akidai kuwa, alipata kura nyingi zaidi ya kura alizopata Mwillima aliyetangazwa mshindi. Akitoa maelezo kuhusu hilo, Jaji Wambari alisema katika ushahidi ambao Kafulila aliwasilisha mahakamani, amewasilisha takwimu mbili tofauti ,moja ikionesha alishinda kwa kura 34,069 na nyingine akionesha kushinda kwa kura 34,212 matokeo ambayo alisema hayana uthibitisho.
    Kwenye lalamiko la nne, Kafulila aliitaka Mahakama itengue matokeo hayo ya ubunge na imtangaze mshindi wa ubunge wa jimbo hilo. Jaji Wambari alisema hakuna sheria ya uchaguzi ambayo inatengua na kumtangaza mshindi mahakamani badala ya uchaguzi kufanyika upya.

    Akitoa maelezo ya jumla ya kesi hiyo, Jaji Wambari alisema Kafulila alishindwa kusimamia msingi wa malalamiko yake kwa kuleta ushahidi usiotia shaka wa kusaidia malalamiko hayo. Alisema malalamiko yote manne yaliyowasilishwa mahakamani hapo hayana msingi.
    Alimthibitisha Mwillima kuwa mbunge halali wa jimbo la Uvinza na kutaka mbunge huyo kupewa hati rasmi ya kumtambua kama mbunge rasmi. Akizungumza baada ya hukumu, Kafulila alisema kuwa hakuridhishwa na hukumu hiyo akidai imeegemea upande mmoja na kwamba anakusudia kukata rufaa kuipinga.

    Kwa upande wake , Mwillima alisema amesikitika kupotezewa muda mrefu ambao angetumia kutumikia wananchi, akawa anautumia kuhudhuria mahakamani. Baada ya hukumu hiyo, Mahakama ililipuka kwa shangwe na furaha kutoka kwa wafuasi wa mbunge huyo.
    Walimbeba na kutoka naye nje kabla ya kuanza maandamano yasiyo rasmi barabarani. Katika kesi hiyo, Mwillima alisimamiwa na Wakili Kenedy Fungamtama. Msimamizi wa Uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na Mwanasheria wa Serikali ambaye anaiwakilisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), aliwakilishwa na wanasheria wawili wa serikali; Gabriel Pascal na Juma Masanja.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment