Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameagiza kuchunguzwa kwa
sukari kontena 115 ambayo ni zaidi ya tani 3,000 iliyokutwa katika
bandari kavu ya PMM iliyopo eneo la Vingunguti.
Makonda alitoa agizo hilo jana wakati alipofanya ziara ya kushtukiza
katika bandari hiyo na kubaini uwepo wa sukari hiyo ambayo ni mali ya
Mohamed Enterprises, ambayo kwa taarifa zake aliambiwa zilikuwa kontena
165.
Alisema anazitaka mamlaka zinazohusika kama Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), pamoja
na Shirika la Viwango (TBS) kuichunguza sukari hiyo kutokana na sababu
mbalimbali zilizojitokeza katika uwepo wa sukari hiyo kama sukari
kuagizwa kutoka Dubai lakini imetoka Brazil na imepakiwa Dubai, na
upangwaji wa kontena hizo katika bandari hiyo.
“Nashindwa kuelewa kwa nini sukari iagizwe kutoka Dubai lakini itoke
Brazil na kufungashwa Dubai inaonesha inaweza kuwa imeshawahi kuisha
muda wake hivyo nataka ichunguzwe na tunataka tujue kama Mohamed
Enterprises anaficha sukari ili ipelekwe kwa wananchi kwa matumizi,”
alisema Makonda.
Mbali na kutoa maagizo hayo, Makonda pia amezuia kutumika kwa sukari
mifuko 22,000 iliyokutwa katika ghala la Mohamed Enterprises Tanzania
Limited (MeTL) lililopo Barabara ya Nyerere na kutaka wapeleke vielelezo
kuhusu sukari hiyo kwa mamlaka zinazohusika kama ya matumizi yoyote.
Alisema sukari hiyo inayodaiwa kuwa ni ya viwandani ni lazima
iangaliwe kama kweli ipo kwa ajili ya mahitaji ya viwandani au ilikuwa
itumike tofauti na ilivyokusudiwa. Kwa upande wake, Meneja Operesheni wa
bandari kutoka MeTL, Firoz Ebrahim alisema sukari hiyo imefuata
taratibu zote na imefika katika bandari hiyo wiki moja iliyopita.
Katika hatua nyingine, Kampuni ya Al Naeem iliyopewa agizo la saa 36
kuanzia juzi iwe imeshaanza kusambaza sukari kwa bei elekezi iliyokuwa
katika bandari ya Dar es Salaam, imeanza kutekeleza agizo hilo jana
jioni.
Akizungumza na gazeti hili jana Dar es Salaam, Meneja wa kampuni
hiyo, Haruni Zakaria alisema juzi wakati Takukuru na Polisi walipofanya
ukaguzi wa sukari hiyo, walishindwa kufanikisha utaratibu wa uondoaji wa
mizigo bandarini na hivyo ikawalazimu kumalizia taratibu hizo jana na
jioni wakaanza kutoa sukari. Imeandikwa na Sophia Mwambe na Ikunda
Erick.
Chanzo HabariLeo.
Wednesday, 11 May 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment