Siku chache baada ya watu saba wa familia moja kuuawa kwa mapanga
wilayani Sengerema mkoani Mwanza, polisi wamefanikiwa kuwatia mbaroni
watu 12 kwa tuhuma za mauaji hayo huku mmojawapo akikamatwa kwa mganga
wa kienyeji alikokuwa akijitibu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Ahmed Msangi alisema hadi jana upelelezi wa tukio hilo lililozua
hofu kwa wakazi wa Kijiji cha Sima unaendelea na tayari watuhumiwa 12
wamekamatwa.
“Hakuna jiwe litakalobaki bila kugeuzwa katika
upelelezi wa jambo hili, tutawasaka na kuwakamata wote waliohusika kwa
njia moja au nyingine na mauaji haya ya kinyama,” alisema Msangi.
Habari
zilizopatikana kutoka kwa mtu wa karibu na familia ya marehemu Zakaria
Mbata iliyopoteza mama na watoto watatu katika tukio hilo, zinaeleza
kuwa wauaji walilenga kupora fedha zilizohifadhiwa kwenye mtandao wa
simu.
Pia, chanzo kimoja cha habari kilisema kuwa
polisi walimkamata mmoja wa watuhumiwa hao akiwa kwa mganga wa kienyeji
alikokuwa akijitibu jeraha alilopata siku ya tukio.
“Katika
purukushani za mauaji hayo, huyo mhalifu alijeruhiwa usoni, inaonekana
alipigwa na kitu kizito, akakutwa kwa mganga wa kienyeji na amekamatwa
kwa mahojiano,” kilisema chanzo hicho
Tukio Lenyewe
Usiku wa
kuamkia Mei 11, watu wasiojulikana walivamia familia ya Zakaria Mbata na
kuua watu saba kwa kuwakata mapanga sehemu mbalimbali za mwili.
Waliouawa
katika tukio hilo ni mama wa familia hiyo, Augenia Philipo (62), mdogo
wake Maria Philipo (56) na watoto wake; Yohana Mabula (20), Regina
Aloyce (12) na Mkiwa Philipo (13).
Wageni wawili wa familia hiyo, waliojulikana kwa jina mojamoja ya Donald na Samson nao pia waliuawa katika tukio hilo.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment