Spika Mstaafu wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano Tanzania, Anne Makinda akizungumza na wanahabari kwenye mkutano uliokuwa unapitia utekelezaji wa programu ya Ukanda wa
Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) katika kongani ya Ihemi
inayohusisha mikoa ya Iringa na Njombe kuhusu kuchaguliwa Dr. John Magufuli kuwa Rais wa awamu ya tano.
SPIKA mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania, Anne Makinda
amesema kuchaguliwa kwa Dk John Magufuli kuwa Rais wa Awamu ya Tano,
kumenusuru Watanzania na machafuko yaliyokuwa yakielekea kutokea.
Huku akipongeza mtindo wa Magufuli kuweka nchi sawa maarufu utumbuaji
majipu, ambao umekuwa ukikosolewa na viongozi wa Chadema, Makinda
amesema machafuko hayo, yalikuwa yasababishwe na tofauti kubwa ya vipato
vya wananchi baina ya masikini na matajiri.
Alisema hayo jana alipozungumza na wanahabari kwenye mkutano wa
kupitia utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania
(Sagcot), katika Kongani ya Ihemi inayohusisha mikoa ya Iringa na
Njombe.
“Tungeendelea tulivyokuwa tunaendelea, hakika tungekuja kuuana kwa
sababu wenye nacho waliendelea kupata zaidi na wasio nacho waliongezeka
kwa kuwa watumwa wa wenye nacho,” alisema Makinda.
Kauli hiyo ya Makinda, imekuja wakati viongozi wa Chadema wakionekana
waziwazi kutetea watuhumiwa wa matumizi mabaya ya madaraka na
ubadhirifu wa mali za umma ambao wamekuwa wakichukuliwa hatua na uongozi
wa Rais Magufuli.
Utetezi huo ulianza kutolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
mwanzoni mwa Februari mwaka huu, ambapo wakati huo alionya alichoita
fukuza fukuza ya watumishi wa umma bila utaratibu, huku akiomba viongozi
wa dini kumsaidia kukemea.
Baadaye alikuja kuungwa mkono na makada wa chama hicho, akiwemo
aliyekuwa mgombea wa Urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa na mwanasheria
wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye mbali na kuwatetea watuhumiwa hao,
alishauri watuhumiwa hao kwenda mahakamani akidai Rais Magufuli
anaongoza nchi kama mali yake binafsi.
Mamilionea bila kazi
Makinda katika mazungumzo yake ya jana, alisema bahati mbaya
iliyokuwa ikilikumba Taifa ambayo mwenye suluhisho lake ni Rais
Magufuli, ni baadhi ya matajiri kutoeleweka wanafanya kazi gani, lakini
wakifikia mafanikio waliyonayo kutokana na kunufaika kijanjajanja na
fedha za Serikali.
“Kuna watu walikuwa hawaeleweki wanafanya kazi gani, lakini ni
mamilionea, baadhi yao ndio wale walikuwa wananufaika na mamilioni ya
Serikali,” alisema.
Makinda alisema katika kuiweka nchi sawa katika nyanja mbalimbali,
kila Mtanzania ataonja machungu yatakayokuja kuliponyesha Taifa mbele ya
safari.
“Kutakuwa na magumu, wengi watasema aah huyo bwana mbona kabana hivi,
lakini ni muhimu Watanzania wajue hii ni oparesheni kubwa
itakayotuumiza wote, lakini mwisho wa yote Taifa na Watanzania
tutapona,” alisema.
Aliwataka Watanzania waendelee kumuombea kwa Mungu Dk Magufuli ili
aendelee kuwa na afya njema, busara na afanye kazi kwa kasi aliyoanza
nayo hadi atakapomaliza awamu yake.
Wanaompinga
Wakati Makinda akitoa kauli hiyo, Mwenyekiti wa Chadema Mbowe baada
ya kukosa kuungwa mkono na viongozi wa dini aliomba wamkemee Rais
Magufuli mwanzoni mwa Februari, alikuja kuungwa mkono na Lowassa.
Lowassa yeye alidai kuwa utumbuaji majipu umesababisha hali mbaya ya
maisha kwa wananchi, kwa kuwa watumishi hao wa umma wameachishwa kazi.
Mgombea huyo alienda mbali zaidi na kudai kuwa, anasononeshwa anapoona
watu wanaachishwa kazi katika mashirika ya umma.
Mbali na Lowassa, Lissu ambaye mbali na kuwa mwanasheria wa Chadema,
pia ni Waziri Kivuli wa Katiba, mwanzoni mwa mwezi huu, alidai bungeni
kuwa Rais Magufuli amesababisha hofu ya kutumbua majipu kutanda nchi
nzima, huku akimtuhumu kuwa ana viashiria vya udikteta.
Wanaomuombea
Wakati Makinda akiomba Watanzania wamuombee Rais Magufuli, huku
viongozi wa Chadema wakipambana na hatua anazochukua dhidi ya
wabadhirifu wa mali za umma, Askofu Mkuu wa Kanisa la Assemblies of God
(TAG), jimbo la Kilimanjaro, Glorious Shoo, amesema uongozi wa Rais
Magufuli, ni majibu ya maombi ya Kanisa na matarajio sahihi waliokuwa
nayo Watanzania wote.
Askofu Shoo aliyasema hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili
ofisini kwake, ambapo alisema kwa sasa heshima ya nchi imerudi baada ya
mataifa mengine ya nje kujionea uongozi wa Rais Magufuli unavyopiga vita
rushwa na dawa za kulevya.
Alisema kwa sasa Rais Magufuli, ameweza kurudisha ramani ya Tanzania
iliyowekwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na kueleza kasi ya
utumbuaji majipu inayoendelea ni jambo la kumshukuru Mungu, kwa kuipatia
nchi kiongozi anayethubutu kuchukua hatua, bila woga kwa ajili ya
kusaidia wanyonge.
Askofu Shoo alisema atashangazwa kuona kiongozi yeyote wa kisiasa
atakayepinga yanayofanywa na Rais, kutokana na uwajibikaji na nidhamu
mahala pa kazi kurudi.
Alipongeza hatua alizoita za kuponya fedha kwa kuwawajibisha watu
waliosababisha upotevu wa fedha na kufanya mabadiliko yaliyochangia
kuokolewa kwa fedha za umma, hali iliyosababisha heshima ya nchi kurudi
katika mataifa mengine.
“Utendaji kazi na aina ya uongozi wa Rais Magufuli ni majibu ya
maombi yetu sisi Kanisa na tunamuunga mkono kwa asilimia zote, kwani
yale masuala makubwa na ya msingi ameyafanyia kazi bila woga wowote,
ikiwepo vita dhidi ya rushwa, matumizi na biashara ya dawa za kulevya,
uwajibikaji na nidhamu mahala pakazi, ni moja ya baadhi ya maeneo
aliyoyagusa kwa muda mfupi na kuonesha matunda yake.
“Ukisafiri sasa sehemu mbalimbali za dunia, wanakueleza wanafahamu
habari za Tanzania kama moja ya nchi inayopambana na rushwa kwa kasi
kubwa pamoja na biashara ya dawa za kulevya, ambapo hapo awali Tanzania
ilitajwa zaidi kwenye masuala ya kupitisha dawa za kulevya, lakini kwa
kipindi hiki cha uongozi wa Awamu ya Tano hali imekuwa nzuri,” alisema
Askofu Shoo.
Upinzani usipuuzwe
Alishauri viongozi wa upinzani wasipuuzwe licha ya baadhi yao kuwa na
tabia ya kupinga vitu vinavyofanywa na Serikali, ambapo aliitaka
Serikali kuchuja masuala ya msingi yanayosemwa na viongozi hao, ili
yanayoweza kufanyiwa kazi kwa manufaa ya Watanzania wote katika kuiponya
nchi, yafanyiwe kazi.
Alisema sasa ni muda wa kuweka siasa pembeni kwa vyama vyote, ili
vishirikiane na Serikali iliyopo madarakani, ili mambo ya kweli
yanayopigiwa kelele na upinzani kama yana ukweli yafanyiwe kazi na
wananchi waridhike kweli yamefanyiwa kazi.
“Siasa ikae pembeni tuiponye nchi yetu wapinzani na Serikali kwa
kumuunga mkono Rais Magufuli ...lakini tutaogopa kama kila jambo
linalotoka kwa wapinzani litatupwa, tunatarajia baadhi yatafanyiwa kazi,
pia wapinzani nao tutawashangaa sana wakipinga kila kinachofanyika na
Serikali ya Awamu ya Tano,” alisema Askofu Shoo.
Alisema kwa sasa ni vyema Rais Magufuli aweke mfumo sahihi
utakaokwenda na kasi yake, ili viongozi wengine watakaokuwa kwenye
nafasi mbalimbali, wasitoke nje ya mfumo huo, ambao utazuia matatizo
yasitokee.
Imeandikwa na Frank Leonard, Njombe na Arnold Swai,Hai.
Chanzo HabariLeo.
Saturday, 21 May 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment