Saturday, 21 May 2016

Tagged Under:

Ukomo wa miliki ya ardhi kutumika kumaliza migogoro

By: Unknown On: 22:03
  • Share The Gag

  • Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi

    SERIKALI imetangaza kuandaa programu ya kumaliza migogoro yote ya ardhi nchini, itakayohusisha ukomo wa miliki ya ardhi kwa kila anayeomba na kuanzishwa kwa Bodi ya Mfuko wa Fidia.
    Mbali ya hilo, miliki ya viwanja 248 katika halmashauri imebatilishwa kwa kukiuka masharti na mashamba 271 yamebainika kutelekezwa.

    Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema hayo jana bungeni wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/17.
    Lukuvi akizungumzia migogoro ya ardhi, wizara yake itashirikiana na Ofisi ya Rais – Tamisemi, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Maliasili na Utalii katika kutatua migogoro ya ardhi nchini.
    “Programu itaandaliwa ili katika miaka mitano ijayo migogoro yote iwe imetatuliwa,” alisema Lukuvi na kuongeza kuwa katika mwaka 2015/16 migogoro 1,130 imepokewa na kati ya hiyo, 734 imetatuliwa.

    Aliitaja migogoro iliyopo ni kati ya wakulima na wafugaji; migogoro ya uvamizi wa mashamba na viwanja; migogoro kati ya hifadhi na wananchi, na migogoro ya fidia kati ya mamlaka mbalimbali na wananchi.
    Alisema chanzo kikubwa cha migogoro ya matumizi ya ardhi nchini ni kasi kubwa ya ongezeko la watu na shughuli zao za kiuchumi ikilinganishwa na ardhi iliyopo ambayo haiongezeki.
    Aliwataka wabunge na wadau wengine wanaohusika na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi kutoa ushirikiano wa karibu katika kutatua migogoro hiyo.
    Kuhusu miliki ya ardhi, alisema wizara imeanza kukusanya maoni kutoka kwenye halmashauri mbalimbali yatakayotumika kuandaa mwongozo wa ukomo wa kumiliki ardhi nchini. Alisema hatua hiyo inachukuliwa ili kulinda makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wakulima na wafugaji kumiliki ardhi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii.
    “Katika mwaka wa fedha 2016/17, wizara inakusudia kuweka ukomo wa kumiliki ardhi kwa kila anayeomba kumiliki ardhi nchini kwa kuzingatia mapendekezo yatakayowasilishwa na halmashauri mbalimbali,” alisema Lukuvi.
    Alisema changamoto iliyopo ni kuhakikisha ardhi yote inapangwa, kupimwa na kumilikishwa kisheria, huku akibainisha kuwa hadi sasa, takriban asilimia 15 tu ya ardhi yote ya Tanzania imepangwa na kupimwa.

    Kuhusu uhakiki wa mashamba ya uwekezaji, alisema miliki za viwanja 248 katika halmashauri mbalimbali zimebatilishwa kwa kukiuka masharti na taratibu za umilikishwaji upya zinafanywa.
    “Mashamba yaliyofutiwa miliki yagawiwe kwa uwazi na kwa watu wenye uhitaji mkubwa wa ardhi hususan vijana. Mpango wa kugawa mashamba hayo uwasilishwe wizarani kabla ya ugawaji kufanyika,” alisema Lukuvi.
    Alisisitiza kwamba mashamba na viwanja ambavyo havijaendelezwa, vitapokonywa bila kujali vinamilikiwa na nani kwani Serikali haitaki tena kuona mapori makubwa yamekaa bila kuendelezwa. Aidha, alisema wizara itatoza asilimia moja ya thamani ya ardhi kwa wamiliki watakaoshindwa kuendeleza miliki kwa mujibu wa sheria.

    Kuhusu Bodi ya Mfuko wa Fidia, alisema bodi hiyo itasimamia shughuli zote za ulipaji wa fidia nchini kwa niaba ya serikali ili kuondoa kero kwa wananchi ikiwamo kuchelewa kulipwa fidia, kupunjwa au kunyimwa fidia kabisa. Katika mwaka 2016/17 imetengewa Sh bilioni tano kwa ajili ya kuanzisha Mfuko wa Fidia na kugharamia shughuli za Bodi.
    Mbali na hilo, alisema kutokana na maboresho ya sekta ya ardhi yanayofanyika hivi sasa, muda wa kutayarisha hati umepungua kutoka miezi mitatu hadi mwezi mmoja baada ya rasimu ya hati kupokewa kutoka halmashauri.

    Kuhusu upimaji wa viwanja na mashamba, alisema hadi Aprili,2016, ramani zenye viwanja 111,837 na mashamba 577 yameidhinishwa katika mikoa. Alisema katika mwaka 2016/17, wizara itaidhinisha ramani za upimaji zenye viwanja 200,000 na mashamba 400.
    Alisema wizara inaendelea na maandalizi ya rasimu ya mapendekezo ya Sheria ya Usimamizi na Uendelezaji Miliki ambayo ikiridhiwa na kuwa sheria itasimamia haki za wapangaji, kuongeza mapato ya serikali, kudhibiti majengo na huduma zake.

    Akizungumzia mapato na bajeti hiyo, Lukuvi alisema wizara inatarajia kukusanya Sh bilioni 111.77 kutokana na shughuli za sekta ya ardhi. Wakati akitarajia kukusanya Sh bilioni 111.77, Lukuvi ameliomba Bunge liidhinishe Sh 61,873,949,000 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka 2016/17.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment