BAJETI ya Wizara ya Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi, juzi ilipitishwa kwa namna ya kipekee tofauti na ilivyozoeleka.
Hali hiyo inatokana na wabunge wa vyama vyote, kuungana na kumtetea
Waziri wake, Profesa Joyce Ndalichako, wakitaka apewe muda aboreshe
elimu.
Wabunge wamepitisha bajeti ya Sh trilioni 1.3 huku wakisisitiza
serikali iboreshe elimu nchini, ikiwa ni pamoja na kuondoa changamoto
mbalimbali.
Wakati Bunge likiwa limekaa kama kamati, ambako wabunge hushika
mshahara wa waziri hadi wapate majibu ya kuridhisha, kwa upande wa
wizara hii, waziri husika alitetewa na baadhi ya wabunge wakiwemo wa
upinzani.
Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi ) alilalamikia tatizo la
vitabu shuleni, ikiwemo kukosewa kwa mitaala, jambo alilotaka waziri
kuzungumzia.
Akijibu suala hilo, Ndalichako alisema nyaraka alizonazo mbunge yeye
hana, hivyo aliomba kupatiwa afanyie kazi, lakini Mbatia alikataa na
kusema nyaraka hizo si za siri, kwani zipo kwenye mitandao ya elimu huku
kukiwa na vitabu vinavyotumika shuleni.
Baada ya mjadala wa muda mrefu, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe
(ACT-Maendeleo) aliingilia suala hilo na kusema matatizo ya mitaala ni
mapana.
Alishauri suala hilo lirudishwe kwenye Kamati ya Bunge
inayoshughulikia suala hilo kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Mbatia
alikubaliana na ushauri wa Zitto na kurejesha shilingi, kisha kuendelea
na mjadala mwingine.
Awali, alipoanza kujibu hoja mbalimbali za wabunge, Profesa
Ndalichako aliwashukuru wabunge wote bila kujali tofauti za kisiasa, kwa
ushauri mbalimbali waliotoa na kusema atahakikisha anafanyia kazi.
Waziri huyo aliyeteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge na kisha
kupewa uwaziri, ikiwa ni mara yake ya kwanza kusoma hotuba ya wizara
hiyo, alikuwa akishangiliwa mara kwa mara na wabunge wa chama tawala na
upinzani.
Ilipofika wakati wa kuwahoji wabunge, Mwenyekiti wa Bunge, Musa Zungu
alipohoji wanaoafiki waseme ‘Ndiyo’, Bunge lote liliitikia. Hakuna
aliyesema ‘Hapana’.
Aidha Bunge lilizizima kwa makofi kutoka kwa wabunge wote kwa dakika
kadhaa, kabla ya kuahirishwa huku kwa umoja wao wakielekea katika kiti
alichokaa Waziri Ndalichako kumpongeza. Pia kwenye majadiliano, yapo
baadhi ya maeneo ambayo wabunge kwa pamoja, walikubaliana kumpa muda
waziri kufanyia kazi.
Akizungumzia mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala na mifumo mingine
ya elimu, Ndalichako alisema katika kuboresha elimu, lazima kuwe na
mabadiliko. Alisema katika utawala wake, watafanya mabadiliko kwa
kushirikisha wadau wa elimu.
Aliomba jamii kumuunga mkono, pale wanapofanya mabadiliko. “Wabunge
wengi mmechangia kwa uchungu kuhusu ubovu wa elimu nchini, hivyo
tumeanza kufanyia marekebisho ili kuboresha elimu; hivyo ni vema
kutuunga mkono,” alisema.
Chanzo HabariLeo.
Sunday, 29 May 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment