Wakati uchunguzi wa kampuni ya Lugumi inayodaiwa kushindwa kutekeleza
mradi wa utambuzi wa vidole kwenye vituo vya polisi ukiendelea, Baraza
la Vijana la Chadema (Bavicha) limemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya
nchi, Charles Kitwanga kujiuzulu wadhifa wake kupisha uchunguzi huo.
Limesema
haiwezekani waziri anayetajwa kuhusika katika sakata hilo kuendelea na
kazi huku Jeshi la Polisi linalodaiwa kutapeliwa na kampuni hiyo likiwa
chini ya wizara yake.
Hata hivyo, waziri huyo amewajibu vijana
hao wa upinzani kwa kusema hawezi kubishana na watoto na hayo
waliyoyatoa ni mawazo yao binafsi wana haki ya kuyasema.
“Nimeshasema mara nyingi, siwezi kuzungumza tena kuhusu haya mambo. Wao kama wamesema waache waseme,” alisema.
Baraza
hilo lililoibuka na hoja tatu jana, limesema kama waziri huyo atagoma
kujiuzulu kupisha uchunguzi unaofanywa na kamati ndogo ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC), Rais John Magufuli anapaswa kumwajibisha
ingawa suala hilo ni gumu kutokana na uswahiba uliopo kati ya kiongozi
huyo mkuu wa nchi na Kitwanga.
Kampuni ya Lugumi ilibainika
kutotimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga mashine 14 tu kati
ya 108 zilizotakiwa kufungwa, licha ya kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya
fedha kwa mujibu wa mkataba ambazo ni Sh37 bilioni.
Ripoti ya
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14
ndiyo iliyofichua udhaifu huo na baadaye Bunge kuanza uchunguzi baada ya
kutoridhishwa na maelezo ya Wizara ya Mambo ya Ndani na polisi kuhusu
mkataba huo.
Kitwanga anahusishwa na Lugumi kupitia kampuni ya
Infosys anayodaiwa kuwa ni mmoja wa wanahisa. Infosys ambayo imekanusha
kuhusika katika sakata hilo, imedaiwa kuwa iliisaidia kampuni ya Lugumi
kupata vifaa kutoka kampuni ya Dell ya Marekani ili viweze kufungwa
kwenye vituo vya polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari,
Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita alisema: “Hotuba ya upinzani
inaeleza kuwa Lugumi inamilikiwa na Kitwanga na ana ubia hilo siyo siri.
Kilichoelezwa kama kingesomwa bungeni kingemfanya apoteze uhalali wa
kuwa waziri na tunajua Magufuli hawezi kumfanya chochote maana ni
maswahiba.
“Hotuba ile pia ilimtaja Rais ila cha ajabu upinzani
wakaambiwa wafute maneno ‘rais’. Rais Magufuli ameshindwa kuitumbua
Lugumi na kwa kilichotokea bungeni suala hilo haliguswi.”
Alisema
Rais anapaswa kujibu hoja zilizotolewa na wapinzani kuhusu Lugumi na
kubainisha kuwa kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza kampuni hiyo haiwezi
kutenda haki wakati Kitwanga akiendelea kuwa waziri.
Katibu
mwenezi wa baraza hilo, Edward Sembeye alisema: “Katika ripoti ya CAG
ameeleza juu ya ununuzi wa ile feri kuwa ni mbovu na haifanyi kazi hivi
hili siyo jipu?
Kuhusu suala la Jaji Mkuu, Mwita alisema kitendo
cha kuisifia Sheria ya Mtandao alipokuwa London, Uingereza hivi
karibuni si kizuri kwa maelezo kuwa kazi ya majaji ni kutafsiri misingi
ya kikatiba: “Tunamtaka afute kauli hii na aseme sheria hiyo imetungwa
itumike lakini uzuri na ubaya wake hapaswi kuusema maana ni kama anatoa
hukumu kabla watuhumiwa hawajafikishwa mahakamani.”
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment