MKUU
wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amefichua kuwa amekuwa akipigiwa simu
na baadhi ya wafanyabiashara vigogo wenye nia ya kutaka kupunguza
makali ya operesheni inayofanywa na wilaya yake dhidi ya waficha sukari.
Kwamba
simu hizo amekuwa akipigiwa hadi usiku wa manane na huku wengine
wakimtumia ujumbe mfupi wa simu wa maandishi (SMS). Amekemea
wafanyabiashara hao na kutaka waache mara moja mchezo huo, kwani vyombo
vya dola vinaendelea kuwafuatilia.
Hapi
alisema hayo jana wakati akizungumzia suala la Uadilifu kwenye Mkutano
wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini na Wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wanaotokana na shirikisho hilo.
Hata
hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya alibainisha kwamba amekuwa hapokei simu hizo
na SMS hizo za wafanyabiashara wakubwa kutokana na sababu mbalimbali.
“Sababu
ya kwanza sina sababu ya kuzipokea, lakini pili nahofia nikizipokea
nitarekodiwa na wafanyabiashara hao na sauti yangu itasambazwa kwenye
mitandao, kuonesha nipo pamoja nao.
“Wakati
mwingine mpaka usiku wa manane wanapiga simu na kutuma meseji na
wengine wanajitambulisha. Lakini huwa namuonyesha mke wangu na kumwambia
sina sababu ya kuzipokea, kwani naweza nikapokea lakini katika
mazungumzo yetu nikasema neno ‘sawa’, kisha neno hilo linaweza
kusambazwa katika mitandao kuonyesha kwamba nia yetu ni moja ya kuficha
sukari”, alisema Hapi.
Alisema
hao wafanyabiashara wanaoficha sukari, wanaleta madhara makubwa kwa
jamii na uchumi wa nchi, kama vile kuua viwanda vya sukari nchini.
Alisema
wafanyabiashara hao wamekuwa wakiweka ‘oda’ katika viwanda vya sukari
kuchukua bidhaa hiyo, lakini hawaendi kuichukua kwa madai ya kwenda
kuichukua siku za baadaye, lengo likiwa kuificha.
Hapi aliwaomba wakazi wa wilaya ya Kinondoni, kuendelea kuisaidia serikali kufichua watu wote walioficha sukari.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment