Watu 15 akiwamo mke wa marehemu, Sajenti Ally Salum Kinyogoli
wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na tukio la kuuawa kwa askari huyo
wa kikosi cha usalama barabarani usiku wa kuamkia jana.
Kinyogoli
aliyezikwa jana saa 10 jioni kwenye Makaburi ya Mzambarauni, Kitunda,
Dar es Salaam alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na kutoa taarifa
kuhusu hali ya usalama barabarani katika vyombo vya habari.
Kinyogoli
aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake,
Chatembo Kata ya Mwandege, Mkuranga mkoani Pwani mbele ya mtoto wake,
mwenye umri wa miaka kumi na moja.
Akizungumzia kukamatwa kwa mjane huyo, Kamanda wa Kipolisi Temeke, Gilles Muloto alisema:
“Sidhani
kama mnaweza kuzungumza naye kwa sababu hao waliomshikilia ni polisi na
wanakwenda naye kituoni. Hata hivyo, mimi siyo msemaji wa hili
anayeweza kulizungumzia ni Kamanda wa Mkoa wa Pwani.”
Hata
hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi ambaye
hakuwapo msibani alipopigiwa simu ilipokewa na mpambe wake ambaye
alisema: “Mkuu leo amebanwa na vikao vingi kuna Mwenge mkoani kwake na
hili tukio la kusikitisha.”
Mgogoro wa kifamilia
Mama mlezi wa
marehemu, Coletha Ndima alisema mara ya mwisho kuonana na Kinyogoli ni
juzi wakati marehemu alipopeleka baadhi ya samani zake kwa kile
alichodai mke wake mkubwa alikuwa akiziuza.
“Hatujui kama kuna
mgogoro lakini Kinyogoli aliwahi kutuambia kuwa anataka kuoa mke wa
pili, sijui alishaoa, kwa sababu alisema atakuja kumtambulisha mchumba
lakini hakufanya hivyo,” alisema.
Ndima alisema marehemu aliwahi kumwambia kuwa ana mgogoro na mkewe mkubwa lakini hajui ni wa nini.
Mmoja
wa polisi ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema polisi
wanamshikilia mama huyo kwa kuwa yeye ndiye aliyemuita Kinyogoli aende
nyumbani kwake na mauti kumfika.
“Marehemu alitengana na mke
wake mkubwa, lakini siku moja kabla ya kifo, mama huyo alimuita
akimwambia watoto wamemkumbuka, usiku huohuo, ndipo walipomuua,”
alisema.
Mtoto asimulia mauaji yalivyotokea
Mtoto huyo ambaye ni
mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi Ebenezer iliyopo Mwandege
alieleza kuwa watu wawili walifika nyumbani hapo na kumtaka amuite baba
yake.
“Nilipoingia ndani kumuita baba, nilimkuta anatandika
kitanda, baba akaniambia waambie nakuja, wakati natoka, baba naye
alikuwa nyuma yangu, lakini niliwakuta wale watu safari hii wamevaa
ninja (mask) lakini kabla ya hapo walikuwa hawajavaa,” alisema.
Alisema
watu wale walianza kumkaripia baba yake wakimtaka awape funguo ya gari
lakini alikuwa akibishana nao na kisha kuanza kupambana nao lakini
walimpiga bastola ya kichwani na mbavuni.
“Wakati baba
anapambana nao alikuwa anawauliza nimefanya nini, lakini hawakumjibu,
alianza kupiga kelele, wanangu nakufa, wanangu nakufa,” alisimulia
kuongeza:
“Ujue baba alishawaweza wale, lakini walivyoona anawashinda nguvu waliamua kumpiga bastola.”
Baba wa marehemu, Salum Kinyogoli aliwataka polisi kufuatilia suala hilo ili wahalifu hao wapatikane.
Dada
wa marehemu, Zainab Kinyogoli aliyeonekana kuchanganyikiwa kutokana na
msiba huo alikuwa akilia mfululizo huku akisema: “Ally aje nimbebe,
nimemuachia ziwa, nimembeba.”
Maelezo ya polisi
Awali, Kamanda Mushongi
aliwaambia waandishi wa habari mjini Kibaha kwamba wauaji hao walifika
nyumbani kwa askari huyo wakitumia pikipiki aina ya Boxer na waliingia
ndani kwa kuruka uzio.
Hata hivyo, wauaji hao walipofika kwenye gari hilo hawakufanya lolote bali walitelekeza ufunguo huo na kutokomea.
“Naweza
kusema ni tukio la kushtukiza kwa kweli kwa sababu ilikua ni muda mfupi
tu toka askari aliporudi nyumbani kwake akitokea kazini na hawa wauaji
hawakuchukua kitu maana hata ufunguo wa gari waliouchukua pale nyumbani
walitoka nao nje na kuuacha,” alisema Mushongi.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment