Daraja la Nyerere. |
SERIKALI inatarajia kufanya mapitio ya viwango vya tozo, zinazotumika kwa vyombo vya usafiri vinavyopita kwenye daraja la Nyerere lililoko Kigamboni jijini Dar es Salaam. Hatua hiyo imekuja kutokana na maoni na malalamiko kutoka kwa watumiaji wa daraja hilo juu ya ukubwa wa viwango hivyo, vilivyoanza kutumika Aprili 16 mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (anayeshughulikia Ujenzi), Joseph Nyamhanga, alisema tangu waanze makusanyo, wamepokea ushauri na maoni na kisha watafanya mapitio ya viwango.
“Kwa sasa bado ni mapema sana, hatuna hata mwezi mmoja toka tuanze kupokea tozo, tunaendelea kupokea ushauri na baada ya mwezi mmoja tutakaa na kufanya mapitio tena kuangalia viwango hivyo,” alisema Nyamhanga.
Nyamhanga alisema Serikali itafanya tathmini kuona kama kweli viwango vinavyotumika sasa ni mzigo kwa watumiaji wa daraja na ikionekana malalamiko ni mengi na inahitajika kupunguza, itafanya hivyo.
“Ushauri wangu kwa wananchi wanaotumia daraja hilo ni kwamba wavute subira wakati tunaangalia hali ikoje, lakini waelewe duniani kote barabara za kulipia na hata madaraja yapo, hii ni mfumo ambao upo duniani kote,” alisema Nyamhanga.
Aidha alisema Wizara pia itaangalia namna ya kuweka mfumo ambao utawanufaisha zaidi watumiaji wa daraja hilo wa mara kwa mara kuwezesha kuwapo utaratibu wa kulipia tiketi za msimu zitakazotoa nafuu.
Awali, wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya watumiaji wa daraja, hususani madereva wa daladala, walilalamikia utaratibu uliopo wa kulipia kila wanapopita katika daraja na kusema inawagharimu zaidi kuliko mapato yao kwenye biashara hiyo.
“Kwa siku moja tunajikuta tunaingia gharama kubwa mno kwa sababu sisi tunapita hapa darajani mpaka mara 14 kwa siku na kila tukipita tunatakiwa kulipa Sh 7,000, hii siyo biashara kabisa,” alisema Maro Lyoki ambaye ni kondakta wa daladala.
Dereva wa daladala, Jacob Michael alisema fedha ambayo inapatikana kwa siku katika biashara hiyo haitoshi kulipia kuvuka katika daraja hilo na fedha ya kumpa mwenye gari. Aliomba serikali kusikiliza kilio chao cha kupunguza viwango hivyo linufaishe watu wengi.
Kwa upande wa waendesha pikipiki za biashara maarufu kama bodaboda, baadhi ya waliozungumza na gazeti hili, walisema wamelazimika kuongeza nauli kutoka Sh 2,000 hadi Sh 3,000 kutoka darajani hadi Kituo cha Uhasibu kwa ajili ya kufidia gharama za daraja.
Viwango vya sasa Katika daraja hilo, watembea kwa miguu wanapita bure, wenye baiskeli wanalipa Sh 300, pikipiki Sh 600, mikoteteni, guta, bajaj na magari madogo yanatozwa Sh 1,500, magari aina ya ‘pick up’ Station Wagon na yanayozidi tani mbili ni Sh 2,000.
Mabasi yanayobeba abiria wasiozidi 15 (mini bus) yanatozwa Sh 3,000, mabasi yanayobeba abiria kuanzia 15 hadi 29 Sh 5,000 huku mabasi yanayobeba abiria zaidi ya 29 yanatozwa Sh 7,000.
Ttrekta na magari yenye tani mbili hadi saba, yanalipa Sh 7,000, yenye tani saba hadi 15 wanalipa Sh 10,000, tani 15 mpaka 20 wanalipa Sh 15,000 na yenye tani 20 mpaka 30 yatalipia Sh 20,000.
Matrekta yenye matrela, magari makubwa yenye uzito wa tani saba hadi 15 yanatozwa Sh 10,000 wakati magari yenye uzito wa tani 15 hadi 20 yanatozwa Sh 15,000. Magari yote ya serikali na taasisi za umma yanatakiwa kulipa tozo kama ilivyobainishwa isipokuwa yale yenye namba za jeshi (Magereza - MT, Polisi - PT, JWTZ, Zimamoto) na magari ya wagonjwa.
Hivi karibuni, baadhi ya wabunge wakati wakichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, walishauri viwango hivyo vya tozo, viangaliwe upya hususani kwa daladala zinazopita.
Pia walishauri serikali itumie mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji mapato kwa watu wanaopita darajani hapo. Miongoni mwa waliotaka kuangalia upya viwango ni Mbunge wa Mvomero, Suleiman Sadick Murrad (CCM) aliyesema Sh 7,000 zinazotozwa kwa daladala zinawaumiza.
Alitaka mapato ya watumiaji hao, yazingatiwe badala ya kuwakatisha tamaa kutumia daraja hilo. Pia Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Mageleri alisema viwango hivyo ni vikubwa. Alisema daraja lilipozinduliwa, wananchi waliona ni mkombozi wao, wataondokana na adha ya vivuko iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu. “Baada ya kutangazwa viwango hivyo imekuwa adha kubwa,” alisema.
Chanzo HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment