Mbunge
wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola jana alichangia Bajeti ya Wizara ya
Kilimo kwa hisia kali huku akimpongeza Rais John Magufuli kwa kumtumbua
Katibu Mkuu Kiongozi.
Ingawa hakumtaja kwa jina, Balozi Ombeni Sefue ndiye Katibu Mkuu Kiongozi aliyeondolewa na Rais Magufuli Machi mwaka huu bila kubainisha sababu ikielezwa kwamba angepangiwa kazi nyingine.
Lugola
alisema Rais Magufuli ameonyesha kwa vitendo kuwa anamuenzi Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kauli yake kuwa Ikulu ni mahali
patakatifu.
Mbunge
huyo alitoa kauli hiyo Bungeni mjini Dodoma wakati akichangia hotuba ya
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba.
Lugola
alisema kwa kuwa alikuwa akichangia kwa mara ya kwanza bajeti ya
Serikali ya Awamu ya Tano, ni vyema akampongeza Rais kwa namna
anavyotumbua majipu kwa ujasiri na bila kupepesa macho.
Lugola
akirejea kauli inayosema “kama unataka mali utaipata shambani”,
alimtaka Waziri Nchemba kutumbua majipu katika wizara yake.
“Hatuwezi
kupata mali shambani kama hutatumbua majipu kwenye wizara yako ambayo
yameota sehemu nyeti .. Rais ametumbua jipu la watumishi hewa. Wizara ya
Kilimo ina wakulima hewa na ni jipu ambalo unatakiwa ulitumbue nchi
nzima.”
Huku
akiungwa mkono na baadhi ya wabunge alisema vocha za pembejeo kwa
wakulima ni jipu akisema baadhi ya watumishi wanasajili wakulima hewa na
wengine wakiwa ni marehemu na Serikali inaendelea kuwalipa.
Huku
akiwataja baadhi yao kwa majina, Lugola alitoa mfano wa kata moja
jimboni kwake ambako wakulima hewa wamelipwa vocha zenye thamani ya
Sh46.3.
Alisema
jipu jingine ni mbegu za pamba aina ya Quton ambazo hazioti akisema
zimelalamikiwa na wabunge lakini mwekezaji anakumbatiwa. “Hili ni jipu
ikiwezekana ukitoka hapa ukatumbue jipu hili."
Mbunge ahoji kilimo cha mirungi
Mbunge
wa Same Mashariki (Chadema), Naghenjwa Kaboyoka aliitaka Serikali
kuzungumza na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ili kujua ni kwa nini
wamehalalisha kilimo cha mirungi.
Alisema
Rais huyo ametoa Dola za Marekani milioni mbili, sawa na Sh4 bilioni za
Tanzania ili kusaidia ustawi wa kilimo hicho, ambacho kwa Tanzania ni
kosa la jinai kulima na kusafirisha.
“Rais
Kenyatta ameruhusu kilimo hiki tukizingatia kwamba tuko Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Tutahakikishaje kwamba hii mirungi haitaingia kwetu?”
alihoji.
Alimtaka
Waziri wa Kilimo awasiliane na Kenya ili kujua sababu za kuruhusu
kilimo hicho na namna ambavyo wataweza kudhibiti kisilete madhara
Tanzania.
Ataka marufuku ya nyavu
Mbunge
wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba aliitaka Serikali kupiga
marufuku uzalishaji wa nyavu za kuvulia samaki ambazo haziruhusiwi
badala ya kuwakamata wavuvi. “Kwa nini nguvu kubwa isielekezwe katika
kudhibiti uzalishaji wa hizi nyavu. Mpige marufuku uzalishaji wake
badala ya kwenda kuzikamata kwa wakulima na kuzichoma,” alisema
Serukamba.
Wizara ihame Dar
Mbunge
wa Nchemba (CCM), Juma Nkamia alitaka makao makuu ya Wizara ya Kilimo
yahame kutoka jijini Dar es Salaam na kwenda katika mikoa yenye mifugo
mingi.
Pia
aliishauri Serikali kujenga mazingira yatakayovutia kujengwa kwa
viwanda vya nyama kwenye mikoa yenye mifugo mingi badala ya kusafirisha
mifugo hai umbali mrefu.
Msimamo wa kambi ya upinzani
Akiwasilisha
hotuba ya msemaji mkuu wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni, waziri
kivuli wa wizara hiyo, Magdalena Sakaya (CUF), alisema itaendelea
kulaani ubakaji wa demokrasia Zanzibar.
“Tutaendelea
kulaani kubakwa kwa demokrasia kulikotokea huko Zanzibar katika
Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana,” alisema.
Akizungumzia
wizara hiyo, Sakaya alisema taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha asilimia 75 ya machinjio nchini
hayana huduma na vifaa vinavyozingatia usafi na ubora wa nyama.
“Hali
hii si nzuri hata kidogo kwa kuwa magonjwa ya kuambukiza nchini
hayataisha kutokana na uchafu uliopo katika machinjio ambayo yanalisha
maelfu ya walaji wa nyama,” alisema.
Pia
kambi hiyo imeitaka Serikali kupitia upya mikataba yote iliyoingiwa na
wawekezaji katika mashamba makubwa kuona kama ina masilahi kwa nchi.
Kambi
hiyo ilisema kati ya Sh60.3 bilioni ambazo ziliidhinishwa na Bunge
katika mwaka fedha 2015/2016, Sh19.3 zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo
hazikupokewa.
Alisema
taarifa ya wizara inaonyesha kuwa hadi Machi 31,2016, wizara hiyo
ilikuwa haijapokea hata shilingi moja, hivyo akasema hata mipango
inayotaka kutekelezwa sasa itakuwa ni ngonjera.
“Hii
mipango ambayo ipo kwenye taarifa ya wizara na ile iliyotolewa katika
hotuba ya Waziri Mkuu ni ngonjera tu za kuwafariji wadau lakini ukweli
sekta ya mifugo na uvuvi iko mahututi.
"Kambi
rasmi ya upinzani inaona kwamba kukua kwa sekta hizi itakuwa ni ndoto
kwani hali halisi ni kwamba hakuna fedha za kuendeleza malengo
yaliyowekwa katika awamu ya kwanza,” alisema.
Aliikumbusha
Serikali kuwa inatakiwa kulipa Sh2 bilioni zilizotokana na amri ya
Mahakama kutokana na kesi ya kukamatwa kwa meli ya uvuvi maarufu “samaki
wa Magufuli.”
Alisema Serikali inawajibika kulipa fedha hizo kutokana na kufanyika kwa uamuzi ambao haukuzingatia sheria.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment