Raisi Magufuli akipokea zawadi ya Biblia kutoka kwa Paroko, Peter Pinto
aliposhiriki ibada ya Jumapili ya Kupaa kwa Bwana katika Kanisa Katoliki
Parokia ya Toleo la Bwana Jimbo Kuu la Arusha, jana.
RAIS John Magufuli amesema hatua anazochukua dhidi ya watumishi wa
umma waliofanya ubadhirifu serikalini na taasisi zake zinalenga
kuwarudisha kwenye maadili ya utumishi wa umma, kufuata misingi ya kazi
na sio vinginevyo.
Alisema hayo jana katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Burka mjini hapa
alikoshiriki ibada na waumini wa kanisa hilo. Rais Magufuli alisema
watumishi wa umma walijisahau, wakafanya ubadhirifu na kukiuka kwa
makusudi maadili ya kazi kwa hali ya juu na kufanya Watanzania wanyonge
kuendelea kuteseka wakati wao wakiendelea kuishi maisha ya peponi.
Alisema anapambana na watumishi hao kwa hali na mali na
atawasimamisha kazi na hata kuwafukuza kazi kwa kuwa aliahidi kutetea
wanyonge. Alisisitiza hilo kwake halitarudi nyuma. Rais alisema yeye sio
mkatili wala jeuri kama ambavyo baadhi ya watu wanafikiria.
Alisema kwa hali ilivyokuwa, ni lazima achukue hatua madhubuti kwa
watumishi wa umma walioifilisi nchi kwa manufaa yao, iweze kusonga
mbele. ‘’Mimi sio mkatili wala jeuri, lakini ni lazima uchukue hatua kwa
watumishi wa umma walioifikisha nchi hapa tulipo,’’ alisema.
Aliongeza kusema; “Nimejitoa kafara kwa ajili ya wanyonge kama
nilivyoahidi kipindi nilipokuwa naomba kura kutaka niwe Rais na hilo
litawaudhi baadhi ya watu wakubwa, lakini itabidi wanivumilie tu.
“Niko pamoja na ninyi ndugu zangu Watanzania na wana Arusha wote,
napenda kuwaahidi tena sitawaangusha, nitasimama mbele kuwatetea
masikini. Siku zote nitakuwa upande wenu, siku zote nitatembea na ninyi,
nasema kwa dhati kabisa na nataka muamini hilo kwamba sitawaangusha,”
alisema Magufuli huku akishangiliwa na waumini walioshiriki ibada hiyo.
Rais ambaye alisisitiza kukerwa na hali mbaya ya kimaisha ya
Watanzania wanyonge wakati baadhi ya watumishi wa umma wakiishi kama
wako peponi, alisema kasi yake ya kupambana na watumishi hao hataipungua
kamwe na ndiyo kwanza inaanza.
“Najua baadhi ya wakubwa watakerwa na hatua ninazochukua, kwa hiyo
nawaomba Watanzania mniombee kwa Mungu ili niweze kufanya kazi yangu kwa
amani kubwa, ‘’Watumishi wamejisahau na wamekuwa wakifanya kazi kinyume
na maadili ya utumishi wa umma na hatua ninazochukua msizitafsiri kuwa
ni ukatilii au udikteta hapana,’’ alisema.
Rais Magufuli alisema, ‘’Watumishi wa umma wamekuwa wakiwadhulumu
Watanzania kwa muda mrefu kwa kuwanyonya jasho lao; hivyo ni lazima
maamuzi ya kuwarudisha katika mstari yachukuliwe.”
Alisema ili nchi iweze kupiga hatua lazima kuwe na nidhamu ya kazi,
uadilifu na kuwajibishana linapokutwa kosa. Alisema bila ya hivyo, nchi
haiwezi kusonga mbele itakuwa ni kujidanganya. Rais aliongeza kuwa
Watanzania wanyonge ni lazima wapate haki yao pale wanapohitaji na
kutokuwa na matabaka ya walionacho na wasio nacho.
“Ninajua kuongoza ni kazi kubwa, ninajua kuongoza taifa lililo
masikini kama Tanzania inahitaji mkono wa Mungu, kwa hiyo niwaombe sana
ndugu zangu Wakristo na Watanzania kwa ujumla, muendelee kuliombea taifa
hili, kuniombea mimi, na pia kujiombea sisi wote ili amani tuliyonayo
katika nchi yetu iendelee kudumu katika maisha yote.
“Lakini siku zote katika matendo yetu kila tunapofanya tumtangulize
Mungu kwa sababu Mungu ndio kila kitu, lakini tutambue kwamba siku moja
tutakufa, kwa hiyo ni vyema katika matendo yetu tutakapokuwa hapa
duniani tujitahidi sana kufanya matendo mazuri kwa ajili ya watu na hasa
watu wanyonge, ambao kwa kweli Watanzania waliowanyonge wanapata shida
sana,” alisema.
Akihubiri kwenye ibada ya misa takatifu kanisani hapo, Padri Geramani
Longoi, aliwataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii na kuwa waadilifu
kazini. Katika misa hiyo ya Siku Kuu ya Kupaa Mbinguni kwa Yesu Kristo,
Longoi alisema hata Yesu Kristo alifanya kazi yake duniani na baada ya
kuwatumikia ipasavyo wanadamu, alipaa mbinguni.
Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Jonathan Mushi aliwataka Watanzania
kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi ngumu anayofanya. Mushi alisema
kila Mtanzania mwenye nia njema na nchi yake, hanabudi kumuunga mkono
Rais Magufuli kwa kuwa uamuzi anaouchukua ni mgumu. Alisema uamuzi wake
unataka kila mmoja kufuata maadili ya kazi na kuwa muadilifu.
Chanzo HabariLeo.
Sunday, 8 May 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment