Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majliwa akipokea taarifa ya makabidhiano ya Ofisi ya
Waziri Mkuu kutoka kwa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda kwenye ukumbi
wa ofisi hiyo Dar es Salaam jana.
WAZIRI Mkuu mstaafu Mizengo Pinda amekabidhi ofisi kwa Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa na kumtaka aimarishe ufuatiliaji wa maelekezo anayoyatoa
kwenda ngazi za chini.
Akizungumza wakati wa makabidhiano yaliyofanyika juzi kwenye Ukumbi
wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam,
Pinda alisema katika kipindi cha uongozi wake kulikuwa na ucheleweshaji
wa kupata majibu kutoka ngazi ya chini katika maelekezo aliyokuwa
akitoa.
“Ofisi ya Waziri Mkuu ni kubwa na ina mambo mengi ya kufuatilia. Kama
kuna changamoto nilikumbana nayo ni ucheleweshaji wa majibu kutokana na
maagizo niliyokuwa nikitoa. Itabidi uwe makini sana katika kufuatilia
hili,” alisema Waziri Mkuu mstaafu.
Alimtaka ahakikishe kila idara inakuwa na mpango kazi na kunakuwa na
ufuatiliaji wa kila kilichopangwa. “Pia ninashauri uandaliwe kikao na
watu wa Hazina ili wakueleze jinsi bajeti ya Serikali inavyoandaliwa ili
iwe rahisi kwako kufuatilia vipengele kadhaa vya bajeti ya Serikali
pindi maswali yanapoulizwa bungeni,” alisema Pinda.
Pia alimkabidhi taarifa yenye kurasa 104 inayoelezea majukumu
mbalimbali ya taasisi na idara zilizo chini ya Ofisi wa Waziri Mkuu.
Ofisi ya Waziri Mkuu ina taasisi nane, idara nane na vitengo saba.
Taasisi hizo ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Kudhibiti Dawa za
Kulevya, Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Tume ya
Uchaguzi (NEC), Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Baraza la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Baraza la Biashara la Taifa (TNBC)
na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Pinda alisema pia ameridhishwa na kasi ya utendaji kazi ambayo Rais
John Magufuli na Waziri Mkuu wameanza nayo na kwamba ana imani kwa
uchapakazi wao na uadilifu wao, anaamini wataweza kuivusha Tanzania na
kuifikisha kwenye uchumi wa kati ambako Serikali imejielekeza kufika.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Wednesday, 2 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment