WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imewataka wazazi na walezi wenye wanafunzi wanaotegemea kuanza masomo au kuendelea na masomo katika shule binafsi mapema Januari mwezi ujao, kuvuta subira hadi Desemba 15, mwaka huu serikali itakapotoa maelekezo mbalimbali ikiwemo suala la ada elekezi.
Akizungumzia
hatua zinazofanywa hivi sasa na serikali kuhusu ada elekezi kwa shule
binafsi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome, alisema timu
mbili hivi sasa zinafanya kazi ya uchambuzi wa michanganuo ya ada
kwenye shule hizo, na baada ya muda mfupi uamuzi utatolewa.
“Hili
sasa tumeliundia timu mbili za kufanya uchambuzi wa masuala ya ada
katika shule za msingi na sekondari binafsi, ili kuwa na ada ekelezi
kwenye utozaji wa ada kuanzia Januari mwakani,” alisema Profesa Mchome.
Aidha,
alisisitiza kuwa katika mchakato huo, na kwa muda uliopo hivi sasa hadi
Januari ni kipindi kifupi, hivyo inawezekana ada elekezi zikaanza
kutumika kwa baadhi ya shule za msingi binafsi, kama eneo la majaribio.
Aliongeza
kuwa Tanzania ina shule za msingi 17,000, zikiwamo za binafsi karibu
1,000 na zile za serikali 16,000 na kwamba iwapo wataanza na ada elekezi
kwa shule hizo binafsi, wanaweza kuona utekelezaji wake.
Kwa
upande wa shule za sekondari, Profesa Mchome alisema ziko zaidi ya
shule 4,700 na kati ya hizo shule binafsi ni karibu 1,400 huku za
serikali zikiwa 3,300 na kwamba mchakato wa ada elekezi kwa shule hizo
binafsi unaendelea pia.
“Timu
yetu inaendelea kufanya kazi kwenye mchakato katika shule za sekondari
binafsi, zina wadau wengi kwa vile ni nyingi pia, hivyo hatuwezi kutoa
maekelezo ya harakaharaka bila kuangalia utekelezaji wake kwa kina,” alifafanua Katibu Mkuu.
Alisisitiza
kuwa kwa kuanzia, serikali ilifuta michango yote kwa shule zote nchini
na kwamba hatua hiyo inazihusu pia shule binafsi na kuzitaka kutotumia
ujanja wa kuingiza michango hiyo kwenye ada kwa madai ya kupandisha ada
kwa mwaka ujao wa masomo.
Credit; Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment