Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wananchi wa jimbo lake.
MAWAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na wa Maliasili na Utalii,
wameonya askari wa Wanyamapori wanaojihusisha na utesaji, unyanyasaji na
kujipatia fedha haramu kwa kukamata mifugo au wakulima, waache mara
moja badala yake, wazingatie maadili ya kazi yao.
Aidha, Serikali imetangaza kusitishwa kwa operesheni za kuwaondoa
wafugaji kwenye maeneo wanayochungia mifugo ikiwemo mapori tengefu,
wakati ukifanyika utaratibu wa kuwawezesha kuendesha shughuli zao.
Matamko hayo yalitolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo
Makani, kupitia mkutano uliofanyika kati ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi, Mwigulu Nchemba na wafugaji, wakulima wa Kanda ya Ziwa.
Tamko la mawaziri hao ambalo ni sehemu ya mikakati yao ya kukomesha
kero kwa wakulima na wafugaji, limekuja huku Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akiwaagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa
Halmashauri zote nchini, kuhakikisha wanaongeza udhibiti na usimamizi wa
migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao husika.
Katika mkutano uliofanyika juzi katika uwanja wa Mnadani (Benaco)
Ngara, mkoani Kagera, Mwigulu aliongozana na Makani ikiwa ni sehemu ya
kusikiliza kero na kutafuta utatuzi wa kudumu wa tatizo la malisho
linalowakabili wafugaji.
Wafugaji kupitia Chama cha Wafugaji wa Kanda ya Ziwa (Chawakazi)
walilalamikia uonevu kutoka kwa baadhi ya askari wa Wanyamapori na
wakaomba serikali iachane na operesheni ya kuwaondoa wafugaji kutoka
kwenye maeneo yanayotumika kuchunga ng’ombe katika pori la Burigi.
Baada ya kusikiliza malalamiko ya makundi hayo, pia Mwigulu alimuomba
Naibu Waziri Maliasili kupitia ofisi yake, kuangalia uwezekano wa
kupitia upya mapori tengevu ili baadhi wapewe wafugaji na wakulima kwa
shughuli zao.
Akitangaza kusitishwa kwa operesheni za kuwaondoa wafugaji kwenye
mapori, Makani aliahidi ofisi yake itafanya haraka iwezekanavyo
utaratibu unaoendelea wa kupitia mapori 17 ukamilike ili kutoa maeneo
kwa watu wafanye shughuli zao za kilimo na ufugaji.
Akisisitiza askari Wanyamapori kuzingatia maadili ya kazi yao, Makani
alisisitiza kwamba Serikali itachukua hatua kuhakikisha askari wote
wanafanya kazi kwa kuheshimu sheria za nchi.
Akizungumza na viongozi wa mkoa wa Lindi hivi karibuni, Waziri Mkuu,
Kassim, aliagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa
Halmashauri zote nchini, kudhibiti migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao.
Waziri Mkuu alisema, “Ardhi ni mali ya Serikali lakini maeneo
yanayotwaliwa kwa sababu mbalimbali za maendeleo yasiwe chanzo cha
migogoro na wananchi tunaowaongoza.” Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema
anatambua kuna mgogoro wa eneo la mgodi katika wilaya ya Ruangwa baina
ya wananchi na wawekezaji wa kampuni ya Uranex.
Na hii ni kwa sababu wao ndiyo waliamua kufanya tathmini ya eneo
hilo. “Yale ni makosa kwa sababu aliyepaswa kufanya tathmini ni
Halmashauri na siyo mwekezaji,” alisema.
Created by Gazeti La HabriLeo.
Saturday, 26 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment