Wananchi wakiwa katika pilika pilika za usafiri Ubungo.
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imeanza
kutoa leseni za muda mfupi kwa kuongeza idadi ya mabasi katika njia ya
Dar es Salaam hadi Arusha.
Hatua hiyo ya Sumatra imekuja ili kukabiliana na ongezeko kubwa la
mahitaji ya huduma za usafiri kwenda maeneo mbalimbali nchini, ambapo
watu wengi wanataraji kufanya safari kwenda makwao kwa ajili ya sikukuu
za mwisho wa mwaka.
Akizungumza jana kuhusu hatua hiyo, Meneja Mawasiliano wa Sumatra,
David Mziray, alisema Sumatra imetoa leseni kwa mabasi matano ambayo
yalianza kutoa huduma za usafiri kuanzia Desemba moja na leseni hizo
zitakoma Januari 30, mwakani.
Mziray aliyataja mabasi ambayo hadi sasa yameshapewa leseni za muda
kwa ajili ya kupunguza kero hiyo ya usafiri kwa njia ya Dar es
Salaam-Arusha na ambayo tayari yameshaanza kutoa huduma hiyo ni yenye
namba za usajili T431BYX, T473CCC, T694 ALX, T924DFR na T922 DFR.
Aidha, alisema mabasi mengine 10 yanataraji kuanza kutoa huduma
kuanzia Desemba 7, mwaka huu katika njia tofauti za Dar-Mbeya, Dar
–Songea, Dar- Mwanza na Dar -Mtwara, huku bado wakikaribisha
wasafirishaji wengine kujitokeza kuomba njia wanazodhani zina uhitaji wa
nyongeza ya usafiri.
“Mamlaka inawakumbusha wamiliki wa mabasi wanaotaka kubadili njia
kuomba leseni za muda mfupi kwa lengo la kutoa huduma ya usafiri kwa
mikoa yenye upungufu wa huduma ya usafiri katika kipindi hiki cha
kuelekea mwisho wa mwaka,” alisema Mziray.
Pia aliwakumbusha abiria kupanga safari zao mapema na walipe viwango
vya nauli vilivyoidhinishwa na mamlaka hiyo, huku akitoa tahadhari pia
kwa wamiliki wa mabasi kutovunja sheria kwa kuingiza mabasi yao katika
njia mpya bila leseni hizo kwani kufanya hivyo ni uvunjaji wa sheria.
“Wapo wamiliki wanaovunja sheria kwa kuingiza mabasi yao katika njia
ambazo hawana leseni na bila ukaguzi wa mabasi yao… Kabla ya kupatiwa
leseni kuna ukaguzi hufanyika na hiyo ni faida kwa mmiliki wa gari,”
alisema Mziray.
created by Gazeti la HabariLeo.
Thursday, 3 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment