Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja na
baadhi ya washiriki wa Baraza la Maulid baada ya kuhutubia baraza hilo
kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuungana kwa pamoja
na kushiriki katika vita ya dawa za kulevya, kwani ushiriki wao utaweza
kumaliza vita hiyo, ambayo ni ngumu na inaliangamiza Taifa. Amesema
uwezekano wa kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya nchini upo, iwapo
viongozi wa dini watakuwa mstari wa mbele kuhubiri madhara ya dawa hizo,
ambazo zinaangamiza nguvu kazi kubwa ya taifa.
Majaliwa aliyasema hayo jana katika sherehe za Kuzaliwa kwa Mtume
Muhammad, zilizoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata),
zilizofanyika katika viwanja vya Kariamjee jijini Dar es Salaam, ambapo
pia viongozi mbalimbali walishiriki.
Alisema, wazazi na viongozi wa dini, wanapaswa kukemea na kuhubiri
juu ya madhara ya dawa za kulevya mara kwa mara ili kuweza kuchangia
katika kumaliza vita hiyo ambayo imekuwa ni tatizo linalowamaliza vijana
wengi.
Aidha, Waziri Mkuu alizitaka taasisi za kidini, kuendelea kutoa
huduma kwa jamii nzima bila ubaguzi ili kuweza kufikia malengo ya
maendeleo yaliyopangwa, huku wakiifundisha jamii kuwa wachamungu ili
kupunguza maovu.
“Kama kila mmoja atajua umuhimu wa kuwa Mcha Mungu, basi Tanzania
itaendelea kuwa kisiwa cha amani. Mcha Mungu ni mtu ambaye anazingatia
maadili na kufuata mafundisho yote ya Mwenyezi Mungu.
Hatutarajii kuona mcha Mungu anakuwa mstari wa mbele katika kutenda
maovu na mambo yasiyompendeza Mungu, tutakapokuwa na wachaMungu wengi,
maana yake hata maovu yatapungua,”alisema Majaliwa.
Alisema, kwa pamoja Tanzania inatakiwa kutokukubali kuwa na jamii
isiyokuwa ya wacha Mungu, ambapo aliwataka viongozi wa dini kuhakikisha
wanaiongoza jamii ili iweze kuishi katika uhuru, umoja na mshikamano.
“Tuna jukumu kubwa la kuhakikisha watu wetu wanaishi kwa uhuru, umoja
na mshikamano, kwani hakuna taifa lililoweza kupiga hatua bila
kushikamana, kama wanavyosema umoja ni nguvu... tushikamane ili tuweze
kufikia malengo ya kuwa na maendeleo,” alisema.
Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Abubakari Zubeir alisema Bakwata na
waislamu wote nchini, wanaunga mkono juhudi na hatua zinazochukuliwa na
Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli katika
kupiga vita ufisadi.
Alisema ufisadi ni jambo ambalo halikubaliki, kwani hata Kitabu
Kitakatifu cha Quran, kimeeleza jinsi gani Mwenyezi Mungu anavyochukizwa
na watu wanaofanya uharibifu. “Katika Quran....Mwenyezi Mungu kaeleza
wazi jinsi anavyochukizwa na uharibifu, na ufisadi ni uharibifu kwa
maana hiyo wanaofanya ufisadi wanaenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi
Mungu,” alisema Sheikh Zubeir.
Aliwataka waislamu kukumbuka na kuyafuata mafundisho ya Mtume
Muhammad, kwani miongoni mwa mafundisho hayo ni tabia njema, maadili na
kutenda wema, pia Waislamu kuwa chanzo cha amani na salama mahali
popote.
Alisema Waislamu hawana budi kuendelea kuishi kwa amani na utulivu,
kwani vitendo vya chuki si mafunzo ya Kiislamu na yanamchukiza Mwenyezi
Mungu. Hata hivyo, aliomba Serikali kutambua mchango wa viongozi na
taasisi za dini katika kuchangia, amani, utulivu na maendeleo katika
Taifa.
Pia kutambua dhamana yao katika jamii na kuwashirikisha katika mambo mbalimbali ili kuepusha migongano katika jamii.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Friday, 25 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment