Friday, 25 December 2015

Tagged Under:

Serikali Yatangaza ‘Kuminya’ AJIRA za Wageni......Wanaoishi Nchini Bila Kibali Kukiona cha Moto

By: Unknown On: 00:29
  • Share The Gag

  • Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga ameagiza waajiri kote nchini kutowapa ajira wageni kwa kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.

    Pia, ameagiza maofisa wa Idara ya Uhamiaji kufanya operesheni maalumu kuwatimua raia wote wasio na vibali vya kuishi nchini ifikapo Januari 31, 2016.

    Kitwanga ambaye alitembelea idara hiyo jana, alisema wizara yake kwa kushirikiana na Uhamiaji imeanzisha operesheni ya kuwakamata raia wote wa kigeni wanaoishi nchini kinyume cha sheria na kuwachukulia hatua stahiki.

    Waziri huyo alisema kutokana na watu wengi kuishi nchini bila vibali, amewapa mwezi mmoja Idara ya Uhamiaji kufanya uchunguzi katika maeneo yote ya kazi na makazi, ili kuwaondoa walioingia nchini kinyemela.

    “Katika operesheni hii, tutahakikisha tunawakamata wote na nimetoa maelekezo kwamba nitakuwa nikipewa ripoti kila Ijumaa kuanzia wiki ijayo, mpaka ifikapo Januari 31 tuwe tumesafisha nchi kabisa,” alisema Kitwanga.

    Alisema kutokana na mpaka wa nchi kuwa mkubwa, Uhamiaji watawezeshwa ili kukabiliana na tatizo la upitishwaji wa wahamiaji haramu kutoka nchi mbalimbali, kama ilivyoripotiwa hivi karibuni.

    Pia, alitoa agizo kwa wananchi wa kawaida kuhakikisha wanatoa taarifa kuhusu wahamiaji haramu walioweka makazi katika maghala, kampuni na viwanda bubu ili kumaliza tatizo la wahamiaji haramu nchini.

    Wafanyakazi wageni
    Mbali na maagizo hayo, Kitwanga pia aliagiza wamiliki wa kampuni mbalimbali kuhakikisha hawatoi ajira kwa raia wa nje kwa kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.

    “…Lakini kazi zote ambazo Watanzania wana utalaamu wa kuzifanya zitafanywa na wazawa na si wageni na zile ambazo inaonyesha wazi kwamba Watanzania hawana ujuzi huo, basi zifanywe na wageni,” alisema Kitwanga.

    Kuhusu vibali, Waziri Kitwanga alisema hakuna raia yeyote wa kigeni atakayepata kibali cha kuishi nchini kama hajapata kibali cha kufanya kazi kama amekuja kwa ajili ya kazi. Lakini utaratibu mwingine kama mtu amekuja likizo utaendelea kama kawaida.

    Kitwanga alisema kuanzia Jumatatu ijayo, viongozi wa wizara husika na uhamiaji, wakae wapange utaratibu mzuri utakaoonyesha kwamba hakuna usumbufu kwa raia wa kigeni ambaye anakuja kufanya kazi nchini kwa kuzingatia vigezo.

    Pasi za kusafiria
    Aidha, Waziri Kitwanga alisema mfumo wa uombaji wa pasi za kusafiria na vibali vya ukazi, hivi sasa utakamilishwa kwa njia ya Tehama.

    Alisema mwombaji atatakiwa kufanyiwa mahojiano ya ana kwa ana pindi atakapokamilisha utaratibu wa kujaza na kuzilipia fomu hizo benki, na atapatiwa pasi ya kusafiria baada ya siku tatu huku kibali cha ukazi akikipata baada ya siku tano ili kupunguza urasimu.

    “Tumeafikiana uboreshaji wa namna ya kufanya kazi na kwa mtazamo wa mbali,” alisema.
     Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kulia) akimsalimia Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile wakati alipowasili Makao Makuu ya Uhamiaji, Kurasini jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya ziara ya kikazi. Wapili kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil, na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, John Mngodo.
    Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (aliyevaa tai) akiwasalimia wananchi  wanaosubiri kupata huduma ya Hati za Kusafiria katika Ofisi za Makao Makuu ya Uhamiaji, Kurasini, jijini Dar es Salaam.
    Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile (kushoto) akiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, wakati Waziri huyo alipokuwa anafanya ziara ya kikazi Makao Makuu ya Uhamiaji, Kurasini, jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na Uhamiaji. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
    Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (katikati) akiwaeleza jambo Watendaji Wakuu wa Idara ya Uhamiaji wakati alipofanya ziara ya kikazi Makao Makuu ya idara hiyo, Kurasini, jijini Dar es Salaam jana. Wapili kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani
    Credit;Mpekuzi blog

    0 comments:

    Post a Comment