VIONGOZI mbalimbali wa dini nchini, wamempongeza Rais John Magufuli
na kuwaomba Watanzania kuendelea kumsaidia na kumuombea ili atekeleze
majukumu yake kikamilifu katika kuboresha uchumi wa taifa.
Aidha, takribani wachungaji 10, wamejikusanya kwa pamoja na kumfanyia
maombi kiongozi huyo ili aendelee na moyo wake wa ujasiri katika
kuwatumikia wananchi na kupambana na baadhi ya watumishi wasio
waadilifu, wakiwemo wafanyabiashara wasio waaminifu. Viongozi hao
walitoa rai hiyo kwa nyakati tofauti, ambapo walionesha kuguswa na kasi
ya utendaji wa Dk Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika
kushughulikia kero za wananchi ikiwemo tuhuma za ufisadi.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk
Jacob Chimeledya aliwaomba Watanzania wakiwemo wabunge, viongozi wa
Serikali wa ngazi zote, viongozi wa vyama vya siasa na madhehebu ya dini
kumsaidia kiongozi huyo katika kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Askofu huyo alisema hayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya Jubilee
ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Dayosisi ya Kanisa la Anglikana mkoani
Morogoro juzi, zilizofanyika makao makuu ya kanisa hilo.
Alimpongeza Dk Magufuli na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan kwa
kuchaguliwa kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano na kubainisha kuwa
viongozi hao, wameanza kazi vizuri na kuonesha matumaini mema kwa
Watanzania.
Pia alimpongeza Rais mstaafu, Benjamin Mkapa aliyekuwa mgeni, kwa
uongozi wake uliokuwa umejengwa na uwajibikaji na uwazi uliowezesha
kukuza uchumi na kupunguza mfumuko wa bei na uchumi kuwa imara.
Kwa upande wake, Mkapa alilipongeza Kanisa na kubainisha kuwa licha
ya kutoa huduma za kiroho, pia limekuwa mstari wa mbele kushirikiana na
Serikali katika kutoa huduma za kijamii zikiwemo za afya na elimu.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya
Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Emmanuel Makala, alisema wataendelea
kumuombea Rais Magufuli kutokana na kuendelea kupambana na mafisadi
ikiwemo wanaojihusisha na dawa za kulevya.
Alisema hayo juzi wakati wa ibada ya kuingizwa kazini Mchungaji wa
Jimbo la Bariadi mkoani Simiyu, Aron Mkaro katika kanisa la KKKT
Usharika wa Tumaini mjini humo. Makala alisema kuwa ni wajibu wa
viongozi wa dini, kumwombea Rais na wasaidizi wake kuhakikisha
wanabadilisha maisha ya Watanzania.
Alisema watamuombea Rais Magufuli na viongozi wengine wakuu ili
kuhakikisha nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma inarejea, ikiwa pamoja
na kupamba na mfumo mbovu wa utoaji huduma kwa jamii.
Mkoani Mara, wachungaji zaidi ya 10 kutoka makanisa mbalimbali
wilayani Tarime, wamefanya kikao cha kumuombea Rais Magufuli ili
aendeleze juhudi zake za kuwakomboa wananchi, wakiwemo wa kipato cha
chini kwa kuwabana na kuwachukulia hatua watumishi wa Serikali wasio
waadilifu.
Wachungaji walioshiriki katika dua hiyo, wakiongozwa na Makamu Askofu
wa Kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT) John Mwita,
kumuombea Dk Magufuli ili Mwenyezi Mungu amwongoze na kumlinda dhidi ya
maadui wa Taifa wenye nia mbaya kwa taifa. Habari hii imeandikwa na John
Nditi, Morogoro, Samson Chacha, Tarime na Kareny Masasy, Bariadi.
Tuesday, 1 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment