Friday, 4 December 2015

Tagged Under:

Kituo cha Redio chachomwa Z’bar

By: Unknown On: 00:10
  • Share The Gag
  • Na Mwandishi Wetu, Zanzibar WATU wasiojulikana wakiwa na silaha wamevamia studio za kituo cha Radio Hits FM kilichopo eneo la Migombani mjini Unguja na kukichoma moto kwa kutumia mafuta yanayosadikiwa kuwa ni petroli.
    Akizungumza jana mjini Unguja, msemaji wa kituo hicho, Juma Ayoub Amohamed, alisema tukio hilo lilitokea saa 7:30 usiku wa kuamkia jana ambapo zaidi ya watu 15 walivamia studio hiyo na kufanikiwa kuchoma moto.
    Alisema hadi sasa bado hawajajua nini chanzo cha kufanyiwa hivyo, na kuongeza kuwa hakuna siku hata moja waliyopewa onyo na mtu, kundi au taasisi yoyote juu ya uendeshaji vipindi vyao.
    “Tunashangaa hili kundi lilitokea wapi na nini chanzo chake, ila kazi kubwa tumewaachia Jeshi la Polisi ambao wanaendelea na uchunguzi wao wa kisheria,” alisema Juma.
    Hata hivyo alisema tathmini ya awali ya hasara waliyopata baada ya kuchomwa kwa studio hiyo ya redio, ni zaidi ya Sh milioni 40, huku akieleza taarifa zaidi wataitoa baada ya kukamilisha kazi hiyo.
    Mmoja wa wafanyakazi wa redio hiyo, Ali Abdallah, ambaye alikuwa zamu kituoni hapo wakati wa tukio hilo, alisema alikuwa anaendelea na uendeshaji wa vipindi ghafla alisikia sauti za watu wakiwa ndani ya studio hiyo.
    Alisema watu hao ambao walikuwa zaidi ya 15 wakiwa wamejifunika uso, walimwamuru anyanyuke na kutoka nje ili wafanye wanachokitaka.
    Abdallah alisema kuwa mara baada ya taarifa yao hiyo alisita kidogo, na mmoja wao akamsogelea na kuanza kumpiga kwa mabapa ya panga na kumnyanyua na kumfunga kitambaa cha uso na kumtoa nje kijeshi.
    “Walinitaka kwa ukali nitoke nje, nilisita kidogo nao walinichukua wakiwa kundi na kunipiga mabapa ya mapanga mwilini huku wakiwa wamenifunga kitambaa usoni na wakisema kwa sauti kuwa tunataka kufanya jambo humu ndani,” alisema Abdallah.
    Alisema muda mfupi baada ya kutolewa nje, huku yeye na walinzi wa zamu wa studio wakiwa wamewekewa ulinzi na baadhi ya vijana wa kundi hilo, alishuhudia moshi mkubwa ukiteketeza vifaa vyao vya studio.
    Abdallah alisema wakati moto huo ukiteketeza vifaa hivyo, kundi hilo la watu lilitoka nje na kuondoka eneo hilo.
    “Walipoondoka tu mimi na askari wetu tulijitahidi sana kutafuta watu wa kutusaidia tulienda hadi katika nyumba ya Rais mstaafu Aboud Jumbe tukawaelezea wale askari waliokuwapo pale jinsi ya tukio letu, nao walipiga simu kituoni kwao, baada ya muda mfupi kikosi cha askari kikaja ila hawakufanikiwa kukuta hao wachomaji walikuwa wameshaondoka na gari lao,” alisema.
    Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Naibu Kamishna wa Polisi Zanzibar, Salum Msangi, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 7:40 usiku.
    Alisema kituo hicho kilivamiwa na watu wengi ambao idadi yao haijajulikana.
    “Baada ya kukivamia kituo hicho, walimfunga kamba mtangazaji wa zamu aliyejulikana kwa jina la Ally Abdallah na kumtoa nje kisha kukichoma moto kituo hicho. Na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwatia mbaroni waliohusika na tukio hili,” alisema Kamishna Msangi.
    Hili ni tukio la pili katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo miezi michache iliyopita watu kama hao waliokuwa na silaha walivamia kituo cha redio cha Coconut Fm na kuwatisha watangazaji.

    Created by Gazeti la Mtanzania

    0 comments:

    Post a Comment