Wakati
Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli akionekana kuteka
hisia za Watanzania wengi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kimesema hakishtushwi kwani amekuwa akitumia hoja, mikakati
na Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.
Kaimu
Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, amesema kuwa wakati wa kampeni
Chadema ilieleza jinsi ya kupambana na ufisadi, kuwa na utaratibu bora
wa utendaji kazi, uadilifu na uzembe wa watumishi wa umma, mambo ambayo
sasa yanafanywa na Dk Magufuli.
Hata
hivyo, alisema kwa kuwa anachofanya hakikuwamo katika mipango ya Chama
cha Mapinduzi (CCM), anaamini atakumbana na changamoto siku zijazo.
“Akiomba
ushauri tutatoa kwa maana namna gani atekeleze, lakini ni mapema mno
kusema kama ana dhamira ya kuyafanya. Pengine anayafanya kwa ajili ya
kujitafutia umaarufu wa harakaharaka,” alisema Mwalimu.
Mikakati ya Dk Magufuli
Tangu
Novemba 5 mpaka sasa, Dk Magufuli ametangaza mikakati kadhaa ya kubana
matumizi ya Serikali, ili kuimarisha huduma za jamii, sambamba na
kufichua na kuminya mianya ya rushwa na ufisadi.
Miongoni
mwa mambo aliyoyafanya ni kusitisha safari za nje, kupiga marufuku
michango ya aina yoyote kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi kidato
cha nne, kufuta sherehe za Uhuru zilizotajwa kufanyika Desemba 9 na
kuagiza fedha za sherehe hizo zitumike kujenga barabara pamoja na kuibua
madudu ya ukwepaji wa kodi la rushwa katika Mamlaka ya Bandari (TPA) na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mwalimu
alisema mambo hayo ni kati ya mengi yaliyokuwa yakipigiwa kelele na
Chadema pamoja na vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kabla na wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25.
“Mambo
haya (yanayotekelezwa na Dk Magufuli) tulikuwa tumeyapeleka mbele ya
Watanzania ili watuamini na tuwafanyie. Wananchi wanajua nini
kilichotokea na si ajabu kuona wao (Serikali iliyopo madarakani)
wanachukua ya kwetu na kuyafanyia kazi, maana Watanzania ndiyo
walioyachagua na ndiyo waliyokuwa wakiyataka,” alisema.
Huku
akitolea mfano hoja za Chadema za ujenzi wa Chuo Kikuu Dodoma (Udom) na
kuandikwa kwa Katiba Mpya zilivyotekelezwa na Rais mstaafu Jakaya
Kikwete, Mwalimu alisema: “Uungwana ni vitendo (Dk Magufuli)
atakapokuwa anayafanya si vibaya akasema jamani haya yalikuwa si ya
kwangu bali nimeyakopa kutoka kwa wenzangu.”
Alisema
si vibaya kwa kiongozi au chama kuiga mambo mazuri ya chama kingine na
kusisitiza kuwa lengo la upinzani ni kuona mambo ya msingi yanafanyika
ili nchi iwe na maendeleo.
“Suala
atafanikiwa kwa kiwango gani hilo ni suala jingine, kama anayafanya
kwa utashi au kwa kuwahadaa Watanzania hilo ni suala jingine.
Mwishowe kama si lako linakuwa na changamoto katika kulitekeleza,” alieleza.
Alisema wapinzani hawawezi kuishiwa hoja za kuikosoa Serikali ambazo nyingi zinalalamikiwa na wananchi, “Mambo
yetu mengi wameyachukua ila swali linakuja je, wanaweza kuyatekeleza?
Chadema ni chama chenye ubunifu wa hali ya juu katika kutafuta suluhu ya
kero za wananchi.”
Alisema
chama hicho sambamba na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
wataendelea kuumiza vichwa ili kutafuta jinsi ya kuzitatua kero
zinazowakabili wananchi.
“Tunachokitaka
kukiona ni Watanzania wakipata haki zao na maendeleo, waishi katika
nchi yenye demokrasia, utawala bora na misingi mizuri ya sheria,” alisema Mwalimu.
Credit; Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment