RAIS John Magufuli ameamuru fedha zilizopaswa kutumika kugharimia
shamrashamra za Sikukuu ya Uhuru Desemba 9, mwaka huu, kutumika kupanua
barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam, yenye urefu wa
kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson
Msigwa kwa vyombo vya habari jana, ilisema tayari fedha hizo, kiasi cha
Sh bilioni nne, zimepelekwa kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa ajili
ya utekelezaji wa agizo hilo, linalopaswa kuanza mara moja.
Akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale, Ikulu, Dar
es Salaam jana, Rais Magufuli alitaka ujenzi wa barabara hiyo uanze
haraka ili kukabiliana na adha ya msongamano wa magari katika barabara
hiyo.
Kujengwa kwa njia hizo, kutaifanya barabara ya Morocco hadi Mwenge
kuwa na njia tano. Rais Magufuli hivi karibuni alitangaza kufuta
maadhimisho ya Sikukuu ya Uhuru, ambayo huadhimishwa kwa kufanyika kwa
gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama kwenye Uwanja wa Uhuru.
Badala yake, mwaka huu maadhimisho hayo yafanyike kwa watu kufanya
kazi za usafi katika maeneo yao ya kazi na majumbani. Akiwa katika
kampeni za uchaguzi mkuu, Rais Magufuli aliahidi kumaliza tatizo la
foleni za barabarani akichaguliwa kuwa Rais, akisema utatuzi wa tatizo
hilo ulibidi usubiri kukamilika kwa mpango kabambe wa kuunganisha mikoa
yote kwa barabara za lami ili kufungua njia kuu za nchi.
Alisema mpango uliopo ni kuanza kujengwa kwa barabara za juu (fly
over) kwa kasi kwa kuanzia eneo la Tazara, ambapo mkataba umeshasainiwa
ili kuanza ujenzi.
“Suala la foleni za Dar es Salaam wala si tatizo kubwa. Tusingeanza
kujenga barabara za juu tukaacha mikoani hakuna barabara za uhakika za
lami, tungeshangaza ulimwengu. Sasa tunaanza ujenzi wa fly over kwa kasi
kubwa.
“Kuanzia Januari mwakani (2016) tutaanza ujenzi wa barabara ya lami
ya njia sita kutoka Dar es Salaam - Mlandizi hadi Morogoro kwa gharama
ya shilingi trilioni 2.3, ambayo pia itasaidia kupunguza foleni Dar kwa
vile magari yataweza kuingia na kutoka kwa urahisi kuliko sasa,”
aliahidi Rais Magufuli alipoomba kura kwa wakazi wa mkoa wa Dar es
Salaam.
Aidha, chini ya mkakati huo, Rais Magufuli alisema hatua zimeanza
kuchukuliwa ili barabara inayopita baharini katika eneo la Daraja la
Selander, yenye urefu wa kilometa 7.4, ianze kujengwa haraka
iwezekanavyo kutokana na kukamilika kwa hatua za mkataba wa ujenzi.
Kuanza kutekelezwa kwa ahadi hiyo ya kushughulikia kero za foleni
katika Jiji la Dar es Salaam, kunadhihirisha azma ya dhati ya Rais
Magufuli kutekeleza masuala mbalimbali aliyoahidi wakati wa kampeni kwa
kasi kubwa, ambayo haikutarajiwa.
Tayari Rais ameanza kushughulikia upunguzaji wa matumizi serikalini
kwa kupiga marufuku safari za nje zisizo za lazima kwa watendaji wa
serikali, kusimamia makusanyo ya kodi za serikali, kuboresha huduma za
afya na kusimamia utoaji wa elimu bure kuanzia Januari mwakani.
Juzi Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilitoa
Waraka wa Serikali Namba 5, wa mwaka 2015, kuwakumbusha watendaji wa
sekta ya elimu kuhakikisha kuwa wanasimamia utekelezaji wa utoaji wa
elimu bure kwa shule zote za umma na kufutwa kwa michango yote kuanzia
Januari, mwakani.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli jana alikutana na kufanya
mazungumzo na Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa
Ibrahim Lipumba, Ikulu, Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Profesa Lipumba alimpongeza Dk Magufuli kwa
kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na pia kwa kutoa hotuba nzuri ya uzinduzi wa Bunge la 11 la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyokonga nyoyo za Watanzania. Kwa
upande wake, Rais Magufuli alimpongeza Profesa Lipumba kwa msimamo wake
thabiti wa kupinga ufisadi na amemtakia heri katika shughuli zake.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 1 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment