KAMPUNI ya Said Salim Bakhresa (SSB) inachunguzwa na vyombo vya dola
kwa tuhuma za kushiriki kukwepa kodi na hivyo kuikosesha serikali
mabilioni ya fedha kutokana na makontena yaliyohifadhiwa kwenye bandari
yake ya nchi kavu (ICD) ‘kupotea’ bila kulipiwa kodi. Tayari Mamlaka ya
Mapato (TRA) imepiga marufuku SSB kuingiza makontena katika bandari hiyo
kavu ambako ndiko kunadaiwa kufanyika kwa vitendo hivyo vya ukwepaji wa
kodi kutokana na baadhi ya makontena kupotea katika mazingira ya
kutatanisha.
Katika barua iliyoandikwa kwenda kwa Meneja Mkuu wa SSB iliyosainiwa
na Wolfgang Salia kwa niaba ya Kamishna wa Ushuru na Forodha wa TRA,
inaeleza kuwa usitishwaji huo unatokana na kampuni hiyo ya Bakhresa
kuchunguzwa kwa tuhuma za kuwepo madai ya kujihusisha na ukwepaji wa
kodi kwa baadhi ya kontena zilizoingia na kutoka kwenye ICD yake.
Kwa mujibu wa barua hiyo, vitendo hivyo vya ukwepaji wa kodi
vimefanywa kinyume cha Sheria ya Ushuru wa Pamoja wa Nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki ya Mwaka 2004 na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
“Kwa hali hiyo, imeamriwa kusitishwa kuingizwa kwa makontena katika
ICD yako, uamuzi huo unaanza mara moja tangu kuandikwa kwa barua hii.
Pande zote zinashirikishwa katika kushughulikia suala hili,” ilisema
sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa Novemba 17, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Richard Kayombo alipoulizwa juu ya suala hilo jana,
alikiri kampuni hiyo kuchunguzwa, lakini akagoma kuzungumzia kwa undani
kwa kuwa suala hilo liko kwenye uchunguzi.
“Mimi siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu liko kwenye
uchunguzi na wanaofanya uchunguzi huo ni state organ (vyombo vya dola).
Katika hatua hiyo, mimi siruhusiwi kusema lolote,” alisema Kayombo.
Meneja wa Kundi la Makampuni ya Said Salim Bakhresa, Said Mohamed
alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema yeye hahusiki na masuala ya
ICD badala yake mambo hayo aulizwe Meneja wa ICD aliyemtaja kwa jina
moja la Khan. “Mimi niulizie unga umekosekana... Sihusiki kabisa na
mambo hayo,” alisema Mohamed.
Hata hiyo, Mohamed aligoma kutoa mawasiliano ya Khan, akisema: “Hiyo
namba mimi hapa sina, wewe mtafute tu huko ICD atakupa maelekezo zaidi.”
Habari zilizopatikana jana pia zilieleza kuwa mmoja wa wafanyakazi wa
SSB anayeishi maeneo ya Kinyerezi (jina tunalihifadhi), alivamiwa na
kundi la maofisa wa Serikali kuanzia asubuhi hadi jioni na kufanya
upekuzi kwake.
“Tangu asubuhi hawa jamaa wamekuja hapa wakamchukua mjumbe wa eneo
hili na kwenda naye kufanya upekuzi, hadi sasa hivi wanaendelea kufanya
kazi hiyo,” alisema Tito Bagule, mkazi wa eneo hilo.
Tayari Rais John Magufuli ameshamsimamisha Kamishna Mkuu wa TRA,
Rished Bade kutokana na tuhuma za uzembe na rushwa na kusababisha
upotevu wa makontena zaidi ya 349 yenye thamani ya Sh bilioni 80.
Upotevu huo umegundulika baada ya makontena hayo kuonekana kwenye mifumo
ya Mamlaka ya Bandari, lakini haimo kwenye mifumo ya TRA.
Kabla ya kusimamishwa kazi, Bade alikiri kupotea kwa makontena hayo,
wizi ambao alisema unafanywa kati ya bandari kuu na bandari kavu (ICD)
ya Ubungo.
Alisema kutokana na upotevu wa kontena hizo mmiliki wa bandari hiyo
ameamriwa kulipa faini ya Sh bilioni 12.6 na hadi sasa alishalipa Sh
bilioni 2.4. Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai (DCI), Diwani Athuman, amesema tayari jeshi hilo limeanza
upelelezi kuhusu kashfa ya upotevu wa makontena iliyobainishwa hivi
karibuni na kusababisha baadhi ya vigogo wa TRA kusimamishwa kazi.
Pamoja na upelelezi huo, alisema wameanza uchunguzi wa mali za
wafanyakazi wote waliohusishwa na kashfa mbalimbali TRA kama
ilivyoagizwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili kubaini kama zinaendana
na kipato chao halisi. Akizungumza na gazeti hili jana, Diwani alikiri
kuwa jeshi hilo linawashikilia watumishi wanne kati ya watano wa TRA
ambao jeshi hilo liliagizwa liwakamate na kuwahoji kuhusu sakata la
upotevu wa kontena 349.
“Tuliagizwa tuwakamate watumishi watano, mpaka sasa tumewakamata
wanne, mmoja ndio tupo kwenye utaratibu wa kumkamata, lakini kikubwa ni
kwamba tumeanza upelelezi, kama tulivyoagizwa,” alisisitiza DCI Diwani.
Kuhusu suala la mali za watumishi hao, alisema ni jambo ambalo bado
lipo kwenye upelelezi na linahusisha taratibu nyingi za kisheria, hivyo
asingependa kulizungumzia kutokana na sababu za kipelelezi.
Kutokana na ziara ya ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam, Waziri
Mkuu Majaliwa alibainisha kupitishwa kwa makontena zaidi ya 300
bandarini bila kulipiwa kodi na kuisababishia hasara Serikali ya zaidi
ya Sh bilioni 80. Kutokana na kashfa hiyo, Rais Magufuli alimsimamisha
kazi Bade na kumteua Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Philip
Mpango kukaimu nafasi hiyo mpaka hapo uchunguzi utakapokamilika.
Maofisa wengine waliosimamishwa ni Kamishna wa Forodha, Tiagi
Masamaki, Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya, Mkuu wa
Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande,
Hamisi Ali Omari na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu, Eliachi Mrema.
Wengine ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 1 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment