Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wanasiasa walioshindwa kwenye Uchaguzi
Mkuu hawaruhusiwi kuitisha mikutano ya hadhara kwa ajili ya kuwashukuru
wananchi kwa kuwa wanaweza kuvuruga shughuli za maendeleo.
Waziri
Mkuu alisema hayo wakati akilishukuru Jeshi la Polisi wilayani Ruangwa
kwa kufanya kazi ya kusimamia Uchaguzi Mkuu uliomalizika Oktoba 25 kwa
CCM kushinda kiti cha urais na kuzoa takriban viti 180 vya ubunge.
“Naendelea
kuwashukuru kwa mchango wenu mkubwa kiulinzi, lakini pia usimamizi wa
zoezi zima la uchaguzi na hatimaye hivi sasa watu wameshapatikana,” alisema Waziri Majaliwa nje ya ofisi za jeshi hilo.
“Na
tumesema, siasa tumeshazimaliza. Sasa tunataka tufanye kazi za
maendeleo. Hatuhitaji tena watu kuja kutuvuruga. Mikutano ya shukrani
itafanywa na wale tu walioshinda kwenye maeneo yao. Wengine watulie.
“Vyama
sasa viache wale tu waliochaguliwa kwenye maeneo yao washukuru, wengine
hawa watakuja kuleta maneno ambayo yatatuvuruga. Mimi naamini mko
imara.”
Wakati
Waziri Majaliwa akisema hayo, tayari Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea
urais wa Chadema na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), alishapanga kuanza ziara ya kuzunguka nchi nzima kwa lengo la
kuwashukuru wananchi waliompigia kura.
Hata
hivyo, ilipofika siku ya kuanza ziara hiyo, Chadema ilitangaza kuwa
imeahirisha hadi itakapotangazwa tena, ikiweka bayana kuwa uamuzi huo
hautokani na vitisho vya makamanda wa polisi wa mikoa.
Awali,
amri ya kuzuia mikutano ya kisiasa ilikuwa ikitolewa kwenye mikoa na
baadhi ya makamanda wa polisi, lakini tamko hilo la juzi la Waziri
Majaliwa linatia msumari marufuku hiyo ya kuendesha shughuli za kisiasa
kwa hoja ya kushukuru wananchi.
Lowassa,
ambaye alihamia Chadema siku chache baada ya kukatwa jina lake na CCM
mwezi Julai, aliweka rekodi ya kuwa mgombea wa upinzani aliyepata kura
nyingi baada ya kupigiwa kura na watu milioni 6.07 ikiwa ni asilimia
39.9, huku mshindi akipata kura milioni 8.88 sawa na asilimia 58.46.
Tamko
hilo la Waziri Majaliwa tayari limeanza kupingwa sehemu mbalimbali,
ikiwa ni pamoja na kwenye mitandao ya jamii na vyama vya siasa kutoa
matamko.
“Hii
ni kauli ya ajabu kutolewa na mtu anayesimamia utendaji wa shughuli za
kila siku za Serikali inayotaka kuwaaminisha (wananchi) kuwa itakuwa
tofauti na serikali nyingine zilizopita za CCM,” inasema Chadema katika tamko lake la jana jioni kujibu kauli ya Waziri Majaliwa.
“Kama
wao (CCM) ndiyo walioshinda kama ambavyo Waziri Mkuu Majaliwa amesema
na kwamba wanaendelea kutekeleza wajibu waliokabidhiwa na wananchi,
tunahoji hofu yao nini hasa wakiona au wakisikia Chadema wanapanga
kwenda kuongea na wananchi? Wanaogopa nini?”
Taarifa
hiyo iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano, Chadema imesema kuwa waziri
Majaliwa ametoa tamko hilo siku chache baada ya kufanya mkutano mjini
Lindi uliowabagua wananchi kwa itikadi zao kwa kutoa nafasi kwa chama
kimoja cha siasa ambacho ni CCM kuhutubia na kufanya siasa.
“Matukio
haya yanaanza kumdhihirisha Waziri Mkuu Majaliwa ni kiongozi mwenye
uelekeo wa namna gani hivyo kuanza kuifunua Serikali ya Rais John
Magufuli chini ya CCM kwa miaka mitano ijayo itawapeleka wapi
Watanzania,” inaeleza taarifa hiyo.
“Ni
dalili za wazi za watu waliolewa madaraka na kuchoka kuwa viongozi na
sasa wanataka kuwa watawala wenye kudhani kuwa fikra zao ndizo
zinazongoza nchi badala ya misingi ya inayokubalika miongoni mwa jamii
nzima kupitia Katiba, Sheria, Kanuni na taratibu mbalimbali.”
Naye
makamu mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema uamuzi
huo ni kinyume na Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa na kwamba Serikali
inazuia wapinzani kufanya mikutano ya kushukuru wananchi kwa kuwa
inajua watatoa ushahidi wa jinsi kura zilivyoibwa.
“Wanatuzuia kwa sababu wanajua tutakwenda kutoa ushahidi wa jinsi CCM ilivyoiba kura za urais na ubunge,” alisema Profesa Safari.
“Kiongozi
anaweza kuzuia mkusanyiko iwapo tu nchi itakuwa katika hali ya hatari.
Jambo hili hata Rais hawezi kulizua kienyejienyeji tu,” alisema Profesa Safari ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Alisema
Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 imeeleza wazi majukumu ya vyama
vya siasa, kuwa ni pamoja na kufanya mikutano na maandamano.
Pamoja
na tamko la Waziri Mkuu kumruhusu kufanya mikutano kutokana na ukweli
kuwa alishinda uchaguzi wa ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Kiongozi wa
ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alizungumzia marufuku hiyo kuwa ni kauli ya
kisiasa isiyo na mantiki.
“Mikutano
inaratibiwa na Sheria ya Vyama vya Siasa. Hii kauli ya Majaliwa naona
kama ilikuwa ya kisiasa zaidi. Jeshi la polisi ndilo lenye jukumu la
kuzuia mikutano na litafanya hivyo kama kutakuwa na hali ya hatari na si
vinginevyo,” alisema Zitto.
Mwanasheria
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia
alimtaka Waziri Mkuu kujikita katika uwajibikaji badala ya kuingilia
vyama vingine.
“Sheria hairuhusu mtu yeyote kuzuia mikutano ya kisiasa isipokuwa kama kuna tishio la vita,” alisema Sungusia.
“Kuruhusu baadhi ya watu kufanya mikutano na wengine kuwazuia ni kuwanyima haki watu.”
Credit; Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment