Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema wapambe na
vigogo waliompigia debe na kumnadi Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed
Shein kuwania urais mwaka 2010, hivi sasa wamemgeuka na hata baadhi
yao kumuona kikwazo.
Kwa mujibu wa Umoja huo, vigogo hao sasa wamemgeuka na baadhi yao
wanamuona kikwazo kwa msimamo wake wa mapinduzi na kuonekana mtu
asiyeyumbishwa kwa kukataa vitisho.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Unguja jana na Kaimu Katibu Mkuu wa
UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alipozungumza na makundi ya vijana wa CCM
kutoka majimboni ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya marudio ya uchaguzi
wa Zanzibar.
Alisema madalali hao wa siasa hawakujua kama Dk. Shein ni zao la
mapinduzi huku wazazi wake wakiwa ni waathirika wa Mapinduzi ya Zanzibar
ya Januari 12 mwaka 1964.
“Laiti kama Dk. Shein asingelelewa, kuandaliwa na kukuzwa kwa
misingi ya mapinduzi, mbayuwayu na mbweha wanaopania kuyatokomeza
mapinduzi yetu wangepata mwanya wa kuukwapua urithi huo.
“Waafrika wenyeji wangerudi katika kutumikishwa kazi za uyaya na
ukuli na kulipwa ujira mdogo tofauti na jasho wanalolitoa,” alisema
Shaka.
Aliwataka Wazanzibari kuendelea kumuunga mkono Dk. Shein wakiamini kiongozi huyo si wakala wala dalali.
“Naona fahari kukitumikia chama changu nikiwa bado kijana, nakomazwa,
kufunzwa na kuelimishwa kujua pumba na mchele. Wanaojifanya vinara wa
uongo nawasikitikia kwa sababu watamalizika kwa aibu katika siasa,”
alisema.
Created by Gazeti la Mtanzania.
Wednesday, 2 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment