Meli ya mv Mapinduzi II ikiwa imetia nanga katika bandari ya Zanzibar ikitokea Korea Kusini. (Picha na Miza Othman-Maelezo Zanzibar). |
MELI mpya ya Mv Mapinduzi (II) imewasili katika Bandari ya Zanzibar jana kwa ajili ya kuanza safari zake baada ya kukamilika kwa ujenzi wake nchini Korea Kusini.
Hafla ya kushuhudia kuwasili kwa meli hiyo iliongozwa na Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Omar Yussuf Mzee ambapo alisema ujenzi wa meli hiyo ni agizo la Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Mzee alisema meli hiyo bado iko katika mikono ya wajenzi hadi sasa na inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Dk Shein. Alisema meli hiyo ina vifaa vya kutosha kama vile maboya ya kujiokolea pamoja na boti ndogo ili kuweka usalama kwa abiria watakaosafiri na meli hiyo.
Waziri wa Fedha alisema meli hiyo itasafiri Pemba pamoja na Dar es Salaam hivyo kuwataka wananchi kuitunza meli hiyo kwani ni matunda yao. Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Dk Juma Malik alisema lengo ni kulifanya Shirika la Meli lifanye kazi kibiashara ili kuongeza Pato la Taifa.
Aliwaomba wananchi kuitunza na kuitumia vizuri meli hiyo kwani wamefanya kazi kubwa na kutumia gharama hadi kufikia kukamilika kwa meli hiyo.
Created by Gazeti la HanbariLeo.
0 comments:
Post a Comment