Sunday, 27 December 2015

Tagged Under:

Magufuli, Shein wakutana Ikulu

By: Unknown On: 00:10
  • Share The Gag

  • Rais John Magufuli (kulia) akiwa katika mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein Ikulu jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Ikulu).

    RAIS John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein Ikulu jijini Dar es Salaam. Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya mazungumzo hayo jana, Rais Shein amesema lengo la mazungumzo hayo, ilikuwa kumpa taarifa Rais Magufuli, kuhusu hali ya mazungumzo ya kisiasa yanayoendelea huko Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu.
    Amesema mazungumzo ya hali ya Zanzibar yanaendelea chini ya Kamati Maalumu yenye viongozi wakuu wastaafu na viongozi wakuu wa sasa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo yeye ndiye Mwenyekiti. Wajumbe Mbali na Dk Shein ambaye ni Mwenyekiti, wajumbe wengine ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.
    Wengine ni Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungo wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete. Pia yupo Rais mstaafu wa Awamu ya Sita wa Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume na Rais mstaafu wa Awamu ya Tano wa Zanzibar Dk Salmin Amour.
    *Kazi yao
    Amesema tayari kamati hiyo imeanza mazungumzo tangu Novemba 9, mwaka huu na yamelenga kujadili hatma ya Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, uliofutwa. Rais Shein amebainisha kuwa mazungumzo hayo bado yanaendelea.
    “Kwa hiyo nimekuja kumpa taarifa Mheshimiwa Rais Magufuli kuhusu maendeleo ya mazungumzo yetu, ili ajue kinachoendelea akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo Zanzibar ni sehemu yake na sisi ni jukumu letu kumpa taarifa hiyo,” alisema Rais Shein.
    Kwa mujibu wa Rais Shein, mazungumzo hayo yatakapokamilika wananchi watajulishwa. Kamati Kuu Katika hatua nyingine, leo Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, inatarajia kukutana, chini ya Mwenyekiti wake, Rais Shein.
    Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu, amesema hayo katika taarifa aliyotuma jana kwa vyombo vya habari. Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Jabu, kikao hicho kitafanyika kuanzia saa 4:00 asubuhi katika Ofisi Kuu ya CCM, iliyopo Kisiwandui, Mjini Zanzibar.
    Taarifa hiyo imeeleza kuwa kikao hicho pamoja na mambo mengine, kitapokea na kujadili taarifa mbalimbali kutoka idara na vitengo vya CCM, kwa maendeleo ya chama na Taifa kwa ujumla.
    Kikao hicho kwa mujibu wa taarifa hiyo, kilitanguliwa na kikao cha Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar, iliyokutana Jumatano wiki iliyopita, chini ya Mwenyekiti wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai.
    Kikao hicho cha Jumatano, kimeelezwa kwamba ndicho kilichoandaa ajenda za kikao cha leo na mpaka jana maandalizi ya kikao hicho cha kawaida cha siku moja, yalikuwa yamekamilika. Magufuli na Seif Jumatatu wiki hii, Rais Magufuli alikutana na Maalim Seif Ikulu ya Dar es Salaam na kujadili hali ya kisiasa ya Zanzibar.
    Kwa mujibu wa Ikulu, wawili hao walikutana kutokana na maombi ya siku nyingi ya Maalim Seif, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF). Ikulu ilieleza kuwa mazungumzo ya viongozi hao, pia yalihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
    Taarifa hiyo ya Ikulu, ilieleza kuwa, viongozi hao watatu kwa pamoja walijadili hali ya kisiasa Zanzibar na kufurahishwa na hali ya usalama na utulivu inayoendelea. Mbali na kufurahishwa na hali ya utulivu, taarifa hiyo ya Ikulu ilieleza kuwa Rais Magufuli aliwapongeza Rais wa Zanzibar, Dk Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif na viongozi wote ambao wamekuwa wakishiriki mazungumzo ya kuleta hali ya uelewano Zanzibar.
    Rais Magufuli pia aliwapongeza na kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kudumisha amani na utulivu wakati wa mazungumzo baina ya viongozi wa CUF na CCM yakiendelea huko Zanzibar.
    Katika mazungumzo hayo, Maalim Seif alimueleza Dk Magufuli juu ya hali ya siasa Zanzibar kadri anavyoielewa yeye; na Rais Magufuli alimshukuru Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa taarifa yake nzuri, huku akimsihi waendelee na mazungumzo hadi muafaka upatikane.
    Ikulu pia ilisema majadiliano yanayoendelea, yanatoa fursa ya kudumishwa kwa utulivu na sifa njema ya nchi, hivyo viongozi hao kwa pamoja wamewaomba wananchi waendelee kuwa watulivu ili kutoa nafasi ya majadiliano yanayoendelea kufikia hatma njema.
    Rais Magufuli, alimhakikishia Maalim Seif kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, itahakikisha amani na utulivu inaendelea kudumishwa Zanzibar. Kufutwa Uchaguzi Z’bar Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, mwaka huu ulifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutokana na kasoro zilizobainika katika upigaji kura.
    Hali hiyo imesababisha sintofahamu kwa muda sasa, ambayo imelazimisha kuwepo na vikao vya kusaka mwafaka kuhusu sintofahamu hiyo, ambayo ilivigawa vyama vikuu viwili vya Zanzibar, CCM na CUF.
    CCM yenyewe iliafiki kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu na kupangwa kwa tarehe mpya ya kurudiwa kwa uchaguzi huo, lakini CUF ikikataa kufutwa kwa uchaguzi huo, huku Maalim Seif akijitangaza mshindi kinyume cha taratibu.Created by Gazeti la HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment