Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema atafanya
kazi kwa kasi ya Rais Magufuli katika kukabiliana na changamoto zilizopo
katika wizara hiyo.
Amesema changamoto ziko nyingi kuanzia chini mpaka juu, katika
Mahakama, magereza na kwingineko, hivyo aliomba apewe muda kuangalia
hali ikoje ili abadilishe mifumo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Akizungumzia suala la Katiba Mpya, alisema Rais alieleza vizuri kuwa
litafanyiwa kazi, kwani halikuishia pabaya hivyo muda ukifika
litakamilika.
Alisema watafanya kazi kubwa ili mfumo wa sheria usiwe pingamizi,
bali uendeleze kasi aliyoanza nayo Rais Magufuli. Nape Waziri wa Habari,
Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye alisema atatengeneza
utaratibu katika wizara hiyo, ili kuondoa utamaduni wa mtu mmoja kufanya
mambo mengi peke yake na kuahidi kuwa msikivu na kutengeneza sheria,
ili kila mmoja atimize wajibu.
Akizungumzia changamoto katika michezo, Nape alisema tatizo katika
michezo ni usimamizi wa sheria na kutokuwa na nidhamu kwa kila mtu
kufanya anavyotaka. Alisema zamani wanamichezo walikuwa wakifanikiwa
kutokana na nidhamu, hivyo watasaidiana na wadau mbalimbali kurudisha
nidhamu.
Manyanya na elimu ya juu Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia
na Ufundi, Stella Manyanya, alisema kinachosubiriwa ni kasi ya kuleta
mabadiliko kwa muda muafaka na jambo la msingi ni kazi na kila mtu
ahakikishe anatimiza wajibu wake.
Alisema changomoto katika wizara hiyo ni nyingi, ikiwemo suala la
mikopo ya elimu ya juu na kusisitiza kwamba wanafunzi wote wenye sifa ya
kupata mikopo, wanapaswa kupewa kwa kuwa huo ni mkopo ambao
wataurudisha.
Manyanya alisema wizara hiyo haitamvumilia mwalimu yeyote mzembe,
atakayetumia muda wake vibaya kwa kutotimiza wajibu, kwa kuwa hatua
zitakazochukuliwa ni kumfukuza kazi na sio kuhamishwa kituo cha kazi.
Mhagama, Kairuki Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama,
alimshukuru Rais kutambua mchango wake katika Serikali iliyopita na
kilichobaki ni kutimiza wajibu wao katika wadhifa huo.
“Rais katambua mchango wangu, nashukuru na sasa ni kuhakikisha
nakwenda na kasi yake, ili tumsaidie kutimiza ndoto za wananchi na hasa
kuondokana na tatizo la ajira,” alisema Mhagama.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi), Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alisema
anawiwa deni kubwa kuhakikisha anakwenda na kasi ya utendaji kazi ya
Rais Magufuli.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Sunday, 13 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment