Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipotembelea bandarini na kugundua uozo mkubwa bandarini hapo.
HATUA anazozichukua Rais John Magufuli, katika kukabiliana na ufisadi
ndani ya taasisi na idara za Serikali, zimeanza kuzaa matunda. Hatua
hizo ambazo zinafahamika kama ‘kutumbua majipu’, pia zimeonesha kuungwa
mkono na wasomi, wananchi, washirika wa maendeleo na mataifa mbalimbali
ya nje.
Mathalani, kutokana na juhudi hizo za Rais, makusanyo ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka kutoka Sh bilioni 900 hadi Sh
trilioni 1.3 kwa mwezi. Pia, Serikali imeboresha ukusanyaji wa mapato
katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kuhimiza matumizi ya mfumo
wa kielektroniki.
Kwa upande wa reli, Serikali imetangaza kuwa itaanza kujenga reli ya
kisasa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Bara hivi
karibuni, ili kuboresha usafiri kwa wananchi na kuongeza mizigo
inayosafirishwa.
Hata hivyo, wizara iliyoathirika zaidi na hatua hizo za Rais ni
Uchukuzi, ambayo katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na
Rais Magufuli hivi karibuni, Wizara ya Uchukuzi imeunganishwa na Wizara
za Ujenzi na ile ya Mawasiliano; na sasa kutambulika kama Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Wizara hiyo ya Uchukuzi ilikuwa na taasisi zipatazo 13 zilizo chini
yake. Hadi sasa Rais Magufuli ameshashusha rungu kwa taasisi tatu za
juu, huku ikitarajiwa rungu hilo kuendelea kuzitafuna idara nyingine.
Taasisi ambazo zilikuwa chini ya Wizara ya zamani ya Uchukuzi ni
Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Shirika la Huduma za Meli
(MSCL), Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA)
na TPA.
Nyingine ni Shirika la Ndege (ATCL), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri
wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA),
Kampuni ya Reli (TRL), Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara),
Chuo cha Bahari (DMI), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege (TAA) . Taasisi ambazo zimekamuliwa majipu yake hadi
sasa ni TPA, RAHCO na TRL.
Tayari watendaji wakuu wa TPA na RAHCO, wamesimamishwa kazi na
kuvunjwa bodi za wakurugenzi wa taasisi hizo; pamoja na bodi ya TRL na
baadhi ya maofisa wake wa juu, wakiamuriwa kuchunguzwa na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Rais alitengua utezi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaban
Mwinjaka kutokana na kushindwa kwake kusimamia vyema taasisi hizo zilizo
chini yake na pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadhi
Massawe.
Bodi ya TPA ambayo ilianza kazi Juni 2, mwaka huu ikiongozwa na
Mwenyekiti wake, Profesa Joseph Msambichaka na wajumbe wake walikuwa
Naibu Spika wa Bunge wa sasa, Dk Tulia Akson, Musa Ally Nyamsingwa,
Donata Mugassa, Haruna Masebu, Gema Modu, Dk Francis Michael,
Crescentius Magori, Flavian Kinunda nayo ilivunjwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa naye aliwashushia rungu watendaji wengine
wa TPA kwa kuwasimamisha kazi, ambao ni viongozi watano wa sekta
zilizotoa ruhusa makontena kutoka ndani ya bandari bila kulipa kodi
pamoja na watumishi wanane wa bandari kavu, ambao walihusika na ukwepaji
kwa makontena 2,387.
Wiki hii Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni
Miliki ya Rasimali za Reli (RAHCO), Benhadard Tito na kuivunja Bodi ya
Wakurugenzi iliyokuwa ikiongozwa na Profesa Mwanuzi Fredrick.
Mkurugenzi wa Rahco, Benhadard Tito mbali na kusimamishwa kazi,
lakini Rais Magufuli ameagiza kuchunguzwa kwa kina na Takukuru kufuatia
ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi, uliobainika katika mchakato wa
utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.
Majipu yaliyokamuliwa katika taasisi hizo tatu ,yamesababisha hadi
taasisi zilizo chini ya wizara nyingine kama TRA iliyo chini ya Wizara
ya Fedha na Mipango na Takukuru iliyo chini ya Ofisi ya Rais,Tamisemi,
Utumishi na Utawala Bora, nazo watendaji wake kuathirika kutokana na
makosa yaliyofanywa na taasisi zilizokuwa Wizara ya Uchukuzi.
Rais Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Rished Bade kutokana na ubadhirifu wa mapato katika
Bandari ya Dar es Salaam na pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa
Takukuru, Dk Edward Hoseah.
Created by Gazeti la HAbariLeo.
Saturday, 26 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment