*Gor Mahia wataja dau kubwa, Kerr asema hajaona alichofanya Chalenji
NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
MPANGO wa klabu ya Simba kumnasa Straika wa Gor Mahia, Michael
Olunga, umeingia mushkeli baada ya klabu yake kuitaka Simba ilipe dola
200,000 (zaidi ya Sh milioni 400 za Tanzania), kitu ambacho ni kigumu
kwa klabu ya Wekundu hao wa Msimbazi kulipa kwa sasa.
Simba ilianza kumfukuzia Olunga tangu kwenye michuano ya Kagame,
iliyofanyika hapa nchini kwa Azam kuwa mabingwa, lakini walishindwa
kuafikiana na timu hiyo.
Habari za ndani ilizozipata MTANZANIA, zimedai kuwa dau hilo la Gor
Mahia limeonekana kuwa ni kubwa sana kwa Simba, hivyo kuanza kupoteza
matumaini ya kufanikisha mpango wao huo.
“Hela hiyo ni nyingi sana na inaweza kutumika kusajili wachezaji
wengi zaidi, hivyo kwa sasa uhakika wa kumpata tena Olunga ni mdogo,
labda hadi atakapomaliza mkataba wake mwishoni mwa mwezi huu, ambapo
tunaweza kufanya naye mazungumzo kama mchezaji huru na kumsajili kwa
ajili ya kumtumia msimu ujao,” kilisema chanzo cha habari hizi.
Chanzo hicho ambacho hakikutaka kutajwa jina lake gazetini kilieleza
kwa upande wa mchezaji Paul Kiongera, yeye atajiunga na wenzake hivi
karibuni kama walivyokuwa wametangaza awali, kumalizia mkataba wake wa
miezi saba uliobaki na baadaye kuangalia kama wanaweza kufanya
mazungumzo naye kwa ajili ya kuongeza mkataba.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Dylan Kerr, amedai kuwa
hakuna alichokifanya Olunga kwenye michuano ya Chalenji akiwa na timu
yake ya Kenya, ambao wametolewa hatua ya robo fainali huku akidai
kutokumfahamu Kiongera.
“Sijui walichokifanya kwenye timu zao za huko Kenya, lakini Olunga sijaona alichokifanya kwenye michuano ya Cecafa Ethiopia.
“Hivi Ligi Kuu ya Kenya ni bora kuliko ya Tanzania? Wachezaji wake ni
wazuri kuliko wa huku? Kwanini wanawachukua?” alihoji Kocha huyo.
Awali Kerr kabla ya kuanza kwa usajili huu mdogo alipanga kuongeza
wachezaji, hasa wa ndani, ili kuweza kukipa nguvu kikosi chake huku
akiamini kuwa Tanzania ina wachezaji wengi wazuri.
Created by Gazeti la Mtanzania.
Friday, 4 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment