NA JANETH MUSHI, ARUSHA
JAJI Gadi Mjemas wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha,
amelazimika kutumia tochi ya simu kuandika taarifa za kesi ya
utakatishaji fedha inayomkabili Wakili Median Mwale na wenzake watatu
baada ya umeme kukatika mara mbili wakati kesi hiyo ikiendelea.
Hali hiyo ilitokea juzi wakati mawakili wa pande mbili wakibishana
kisheria ambapo ghafla umeme ulikatika na kulazimu kutumia tochi za simu
zao huku askari polisi akitumia simu yake kummulikia Jaji Mjemas aweze
kuandika taarifa hizo.
Kesi hiyo jana ilisikilizwa ambapo shahidi wa kwanza wa upande wa
Jamhuri, SP. Fadhili Mdemu (39) alidai mahakamani hapo kwamba
washitakiwa hao walifanya jaribio la kuchepusha kiasi cha dola za
Marekani milioni 17.2.
Kesi hiyo iliyochukua miaka minne ilianza kusikilizwa juzi kwa mara ya kwanza saa 7 mchana hadi saa 1:40 usiku.
Shahidi huyo ambaye ni Ofisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya
Jinai, Kitengo cha Uhalifu wa Fedha (FCU), alidai kuwa watuhumiwa hao
walitaka kuingiza fedha hizo kwenye akaunti ijulikanayo kama East Africa
Malaria and HIV Support Program iliyopo Benki ya CRDB, Tawi la Meru
jijini Arusha.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Oswald Tibabyakomya, shahidi huyo
alidai fedha hizo zilitolewa kama sehemu ya msaada na taasisi ya
kimataifa ya Global Fund kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa malaria na
Ukimwi.
Shahidi huyo alidai kuwa fedha hizo zilipaswa kupelekwa kwenye
akaunti ya Serikali (Tanzania) iliyopo City Bank nchini Marekani chini
ya usimamizi wa Wizara ya Fedha.
“Badala yake watuhumiwa walitaka kuzichepusha na kuwaelekeza
wafadhili kwamba fedha hizo zinatakiwa kutumwa kwenye akaunti ya mradi
ya CRDB,” alidai shahidi huyo na kuongeza:
“Watuhumiwa walighushi barua iliyoonyesha imetoka kwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha wakati huo, Ramadhan Khijjah, ikieleza kuwa safari hii
Serikali ya Tanzania imeamua fedha hizo za msaada ziende kwenye akaunti
ya mradi ya CRDB badala ya kutumwa kwenye akaunti ya Serikali.
Alidai kuwa wakati Global Fund ikiwa kwenye matayarisho ya mwisho ya
kutuma fedha hizo, Wizara ya Fedha ilitoa maelekezo kwao ikidai kama
kungekuwapo na mabadiliko ya akaunti ya kutuma fedha hizo wangejulishwa
utaratibu wa kufanya ikiwamo kujaza fomu maalumu.
“Nilifanikiwa kupata nyaraka husika, picha zao na anuani ya Posta
2122 Arusha ikionyesha wanapatikana eneo la Unga Ltd jijini Arusha.
Taarifa hizo hazikutosha kuwapata wenye akaunti hiyo waliojulikana kama
Michael Crispine Chacha na Joseph Anderson Marwa ambapo barua ya
kuwatambulisha ilitoka ofisi ya JJ Mwale na kusainiwa na Wakili Mwale,”
alidai shahidi huyo.
Baada ya ushahidi huo, Jaji Mjemas aliamuru upande wa utetezi unaoongozwa na Wakili Omary Omary na wenzake wapitie nyaraka hizo.
Hata hivyo, mawakili hao waliomba mahakama isipokee nyaraka hizo kama
kielelezo kwa madai kuwa nyaraka hiyo hazikuwa kwenye orodha ya
vielelezo vilivyotajwa na upande wa mashtaka.
Mawakili hao walidai kuwa shahidi si muhusika wa kutoa nyaraka na
hawana ushahidi wa kimaandishi kama nyaraka hizo zilipatikana kwa
kufuata sheria.
Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Tibabyakomya waliiomba mahakama
ipokee vielelezo hivyo kwani vimekidhi vigezo na matakwa ya kisheria.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Mjemas aliahirisha kesi hiyo hadi atakapotoa uamuzi wa pingamizi hizo.
Created by Gazeti la Mtanzania.
Wednesday, 2 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment