RAIS John Magufuli, juzi aliendelea kudhihirisha kuwa serikali yake
haitakuwa na simile kwa watendaji wazembe baada ya kuivunja Bodi ya
Wakurugenzi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) pamoja na kumuondoa
madarakani Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Hussein Kidanto.
Kaimu mkurugenzi huyo amerudishwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine na sasa Profesa Lawrence Mseru wa
Taasisi ya Mifupa (MOI) atakaimu nafasi hiyo.
Dk Magufuli alichukua hatua hiyo kutokana na kusikitishwa na taarifa
ya kutofanya kazi kwa mashine za CT- Scan na MRI kwa takribani miezi
miwili huku mashine kama hizo zikifanya kazi katika hospitali za watu
binafsi.
Rais pia alisikitishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa, hususan
wanaolala chini. Kinachojitokeza ni kwamba rais hakupata maelezo ya
kuridhisha ni kwa nini mashine hizo muhimu zimeshindwa kutengenezeka kwa
muda mrefu kiasi hicho.
Ingawa sababu ya kutotengenezwa kwa mashine hizo kwa wakati inaweza
kuwa uzembe, lakini inaweza pia kuwa kile kinachodaiwa mitaani kwamba
zimekuwa zikiharibiwa kwa makusudi ili watendaji wake wafaidike kwa
mlango wa nyuma na zile zilizo katika hospitali binafsi.
Mtu anaweza kuelewa kwamba wagonjwa wanaofika kwenye hospitali hiyo
ya Taifa (MNH) ni wengi kuliko idadi ya vitanda vilivyopo na ndio maana
wanalazimika wengine kulala chini. Lakini inakuwa vigumu kuelewa pale
mashine muhimu zinapoharibika mara kwa mara kwenye hospitali hiyo kubwa
ya umma pekee, huku kwenye hospitali binafsi hali ikiwa kinyume chake.
Ikumbukwe kwamba mashine hizo zinapoharibika (kama kweli
zinaharibika), zinachangia pia ongezeko la mrundikano wa wagonjwa
wanaolazimika kusubiri huduma inayopatikana kwenye mashine hizo, hasa
wanapokuwa hawana uwezo wa kwenda kwenye hospitali binafsi ambako
gharama za vipimo ni ghali.
Sakata la Muhimbili linatufundisha mengi; moja ni umuhimu wa
kuboresha zaidi hospitali za mikoa na wilaya ili kupunguza mrundikano
kwenye hospitali za rufaa. Lakini kubwa ni kwamba yapo mambo ndani ya
uwezo wa watendaji katika taasisi za umma, lakini hayatekelezwi kutokana
na uzembe au ubinafsi tu.
Tunaamini kwamba, mbali na kuachana na utendaji kazi wa mazoea,
hospitali zote kubwa zitaanza kutenga sehemu ya mapato yake kwa ajili ya
kuhudumia mashine zake kwa matengenezo ya kawaida ya mara kwa mara kama
serikali ilivyoagiza.
Lakini, kubwa ni watumishi wa umma kila mahali nchini kubadilika kwa
kufanya kazi kwa bidii na maarifa wakihakikisha wanatekeleza majukumu
yao kwa asilimia 100. Hii itaongeza tija na kunyanyua uchumi na hivyo
hakuna mashaka kwamba hata kipato chao kitaongezeka muda si mrefu.
Kila mtumishi wa umma akitimiza wajibu wake, kwa maana ya kutoa
huduma nzuri na kuwaheshimu wananchi ambao ndio walipaji wa mishahara
kupitia kodi zao, hakutakuwa na hofu ya kutenda kazi kwa mashaka kwamba
ni lini itakuwa zamu yao ya kutembelewa bila taarifa na Rais Magufuli
kwani atakutaka kila kitu kiko sawa.
Creadit by Gazeti la HabariLeo
Saturday, 14 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment