Naibu Spika wa Bunge la 10 na mbunge wa Kongwa, Job Ndugai. |
WABUNGE jana walianza kujisajili kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 11 wiki ijayo, huku wengi wao wakitoa maoni ya sifa wanazozitaka kwa Spika mpya wa Bunge hilo, zikiwemo uzoefu, busara, kujua kanuni na mwenye utayari wa kuyakabili mabadiliko.
Pia wabunge hao wametoa maoni ya kuomba Mungu amuongoze Rais Dk John Magufuli ateue Waziri Mkuu ambaye atakuwa mfuatiliaji wa mambo na mwenye uwezo wa kufanya maamuzi makini. Mbunge wa Kavuu, Dk Pudenciana Kikwembe (CCM) akizungumza alisema ni muhimu kupata Spika mzoefu, mwenye busara na atakayeweza kutafsiri vyema kanuni.
“Hili Bunge litakuwa na changamoto nyingi sana, kuna haja ya kupata mtu atakayeweza kutumia vyema kanuni, lakini afahamu sheria na awe na uzoefu wa kutosha. “Kwa Waziri Mkuu, awe na uwezo wa kazi, mfuatiliaji na ambaye ataweza kukabiliana na changamoto mbalimbali,” alisema mbunge huyo, ambaye awali alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa.
Mbunge wa Mpwapwa, George Malima Lubeleje (CCM), ambaye alikuwa Mbunge wa jimbo hilo kuanzia mwaka 1990 hadi 2010, kabla ya kurejeshwa tena safari hii, alisema kwa uzoefu wake anaamini Bunge hilo linahitaji Spika mzoefu, anayejua kanuni na sheria na asiegemee upande wowote. Kuhusu Waziri Mkuu, alisema anahitajika msomi na anayeijua vizuri Tanzania, mtendaji na atakayeweza kuendana na kasi ya Rais Magufuli, huku akitaja sifa ya ziada kwamba ni kujulikana kimataifa.
Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk Hamis Kigwangwala alisema bunge hilo la 11 litakuwa la vuguvugu, hivyo anahitajika Spika mwenye hekima na anayeweza kukabili mabadiliko ya wakati. “Ni Bunge la siasa za kazi si siasa za siasa, Spika awe na busara za kutosha, uzoefu na hekima za kutosha. “Waziri Mkuu mzuri ni yule atakayeendana na kaulimbiu ya Hapa Kazi tu, ni vizuri akija mtu mpya maana Watanzania wanataka mabadiliko, hata baraza la mawaziri liwe na sura mpya si mambo ya sura zilezile zilizozoeleka.
“Huko mitaani watu wakisikia kuna mabadiliko ya aina fulani tu ya viongozi, kwao hilo ni furaha tosha, wanataka nao waone utendaji wao,” alisema Dk Kigwangwala ambaye hii ni awamu yake ya pili. Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema), alisema suala la uzoefu na kujua sheria ni mambo ya msingi kwa Spika mpya, lakini lazima awe na uwezo wa kuhimili changamoto za bunge hilo.
“Bunge hili litakuwa si mchezo, vijana wengi, wa umri wa kati na hata wazee, pia idadi ya wapinzani imeongezeka sana, kutakuwa na mambo mengi na hili Bunge litakuwa moto kuliko mabunge yote katika historia ya Tanzania. “Spika wa kuburuza Bunge hatufai, atakayesikiliza upande fulani tu hatufai, tukimpata Spika atakayeingia na itikadi za vyama hapatatosha hapa,” alisema Mbunge huyo ambaye hiyo ni mara ya kwanza kuingia bungeni.
“Kuhusu Waziri Mkuu, naomba sana Mungu amuongoze Rais apate mtu atakayemsaidia hasa, mchapakazi na si mlegevu. “Rais ana mambo mengi, sasa tunataka amsaidie, awe Waziri Mkuu makini, akienda Rais Muhimbili yeye ana uwezo wa kuchukua hatua za kiufuatiliaji mara moja,” alisema Bilago. Naye Mbunge wa Mikumi, ambaye pia ni mpya katika bunge hilo, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ alisema kuna changamoto nyingi na anaamini Bunge la 11 litakuwa la aina yake.
“Namna nilivyowasikia kaka zangu walionitangulia Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki) na Joseph Mbilinyi (Mbunge wa Mbeya Mjini), tunahitaji Spika mtenda haki, mzalendo na ambaye hatayumbishwa na upande wowote. “Kwa Waziri Mkuu tunahitaji mzalendo, ambaye atakuwa mshauri mzuri sana kwa Rais,” alisema Haule. Kwa upande wa Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM), alisema yeyote atakayepitishwa na CCM atakuwa Spika mzuri na ana imani chama hicho ni makini katika kufanya uamuzi.
Kwa upande wa Waziri Mkuu alisema watafurahi wakipata mtu ambaye anaweza kuchukua hatua na mwenye kufanya utafiti wa kutosha na kumtolea mfano Waziri Mkuu aliyepita, Mizengo Pinda kwamba alikuwa na busara na hakuwa akikurupuka. Naye Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alisema kwanza sifa kuu ya Spika ni lazima awe Mbunge kwani itakuwa si jambo jema kuwa na Spika asiyekuwa mbunge.
“Huwezi kuwa na Mkuu wa Majeshi ambaye si mwanajeshi, ama una mkuu wa Jeshi la Polisi halafu si askari, lazima Spika awe Mbunge, awe na uzoefu kama kushika nyadhifa mbalimbali mfano Naibu Spika, au Mwenyekiti wa Bunge. “Kwangu mimi bila kumung’unya maneno anayefaa kuwa Spika ni Job Ndugai (Mbunge wa Kongwa CCM) na Naibu Spika ni Mussa Azzan Zungu (Mbunge wa Ilala, CCM). “Ndugai alikuwa Naibu Spika Bunge la 10, Zungu Mwenyekiti wa Bunge, sifa zinatosha,” alisema mbunge huyo.
Naye Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM), alisema anahitajika Spika mchapakazi, ambaye hataangalia sura ya mtu bali kazi tu. Kwa upande wake Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), alisema ni vyema kupata Spika ambaye hatafungwa na itikadi za vyama, lakini pia awe na uwezo wa nafasi hiyo. Idadi kubwa ya wabunge ilijitokeza jana kujisajili ikiwa ni suku ya kwanza tu, ambapo shughuli ya usajili itaenda hadi kesho.
Waliojitokeza Katika hatua nyingine, leo ndio mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu kwa wanachama wa CCM wanaoomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Spika na Naibu Spika katika Bunge la 11, linalotarajiwa kuanza wiki ijayo, idadi imeongezeka kwa waombaji na kufikia 22. Akizungumzia uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM anayeshughulikia Oganaizesheni, Muhammed Seif Khatib, alisema jana wabunge wawili walijitokeza kuchukua fomu za nafasi ya Spika na Naibu Spika.
Waliojitokeza hiyo jana kuchukua fomu ya Spika ni mbunge mteule wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko na mbunge mteule wa Ilala, Mussa Azzan Zungu ambaye mpaka jana alikuwa mgombea pekee wa nafasi ya Naibu Spika na tayari amesharudisha fomu hiyo. Khatib alisema hadi kufikia hiyo jana idadi ya waliokwishachukua fomu kuwania kuteuliwa nafasi ya spika kwa CCM, ni wanachama 22.
Akifafanua shughuli hiyo ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo, Khatib alisema utaratibu uliowekwa na chama hicho, ulikuwa ni kwamba kwa wanachama ambao si wabunge wachukue kuanzia Novemba 11 na 12, mwaka huu ili kutoa nafasi fomu zao kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa ajili ya uhakiki wa sifa zao. Alisema kwa mantiki hiyo, upande wao uchukuaji fomu ulikamilika juzi na nafasi iliyopo sasa ambayo hata hivyo itakoma ifikapo saa kumi jioni leo, ni kwa wabunge wa CCM, wenye nia ya kuwania nafasi hizo.
“Tumeshafunga milango kwa wananchama wasio wabunge wanaowania nafasi hizo, na sasa milango iko wazi tangu jana kwa wabunge wanaotaka nafasi hiyo, ila ifikapo saa kumi jioni kesho (leo) tutafunga,” alisema Khatib. Alisema baada ya kufunga milango kwa wanaowania nafasi hizo, kazi iliyobaki ya kuteua wagombea wa nafasi hizo, itafanywa na Kamati Kuu ya chama hicho, ambayo hata hivyo hakusema itakaa lini kuamua.
Majina Waliokwishachukua fomu kuwania nafasi ya Spika ni pamoja na aliyekuwa Naibu Spika katika Bunge la 10 na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Tulia Arkson na aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi.
Wengine ni Spika mstaafu, Samuel Sitta, Mbunge mteule wa Chato, Dk Medard Kalemani, Diwani wa Goba - Dar es Salaam, Mwakalika Watson, Julius Pawatila, Agnes Makune na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah Ali Mwinyi, Mbunge wa zamani wa Afrika Mashariki, George Nangale, Simon Rubugu, Banda Sonoko na Leonce Mulenda. Pia yumo aliyewahi kuwa Naibu Waziri, Ritha Mlaki na mhitimu wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 28, Veraikunda Urio.
Kadhalika yupo aliyekuwa mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes na aliyekuwa mmoja wa wagombea 42, waliojitokeza kuwania nafasi ya urais ndani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Dk Kalokola Muzzamil.
Wengine ni aliyekuwa mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi, aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Philip Marmo na Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu. Imeandikwa na Amir Mhando, Dodoma na Ikunda Erick, Dar.
Created by Gazeti la habarileo.
0 comments:
Post a Comment