*Mama Maria Nyerere atangulia Uganda
NA MWANDISHI WETU
ZIARA ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis nchini
Uganda imetajwa kuwa itafufua mchakato wa kumtangaza Hayati Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa mtakatifu.
Kwa mujibu wa mtandao wa ETN wa nchini Uganda, ziara hiyo ya kitume
ya Papa Francis itamfikisha katika eneo la Namugongo ambalo mashahidi wa
imani ya dini ya Kikristu walichomwa moto.
Ni katika eneo hilo la Namugongo ambako Hayati Nyerere alitangazwa
kuwa Mwenyeheri huku mchakato wa kumtangaza mtakatifu ukiwa ulianza
miaka tisa iliyopita.
Namugongo ndiko ambako pia waumini wa dini ya Kikristu wa Afrika Mashariki na sehemu nyingine duniani hufika kuhiji.
Taarifa ya ETN imeeleza kuwa ziara ya Papa Francis Namugongo
itasaidia kufufua mchakato uliodumu kwa miaka tisa sasa wa kumtangaza
Hayati Baba wa Taifa kuwa mtakatifu.
Tayari mjane wa Hayati Mwalimu Nyerere, Mama Maria Nyerere yuko
nchini Uganda ambako amekwenda kujumuika na waumini wengine wa dini ya
Kikristu kumpokea na kushiriki ibada itakayoongozwa na Papa Francis.
ETN imemkariri Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, akisema kuwa mchakato
wa kumtangaza Hayati Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu umetokana na
mchango wake wa kuhimiza heshima na usawa kwa binadamu ambao aliutoa
wakati akiwa kiongozi.
Kwa mujibu wa ETN, Rais Museveni amesifu mchango wa Hayati Mwalimu
Nyerere ambao haukuwa tu wa kuunganisha Watanzania bali alifanya kazi
kwa kujali utu wa Waafrika.
“Hayati Julius Nyerere alikuwa mwanaharakati wa Afrika ambaye
alimpenda Mungu na alijali utu, aliwaunganisha Watanzania wa dini zote
na alisaidia ukombozi wa mataifa mengine ya Afrika kama vile Zimbabwe,
Namibia, Angola, Afrika Kusini na Uganda,” alisema Museveni.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kupitia simu yake ya kiganjani
kuhusu hilo, Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini,
alisema mchakato wa kumtangaza Hayati Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu
unaendelea vizuri.
Alisema suala la kuendesha mchakato huo ni jukumu la Tanzania na si
Uganda hivyo jina la Hayati Mwalimu Nyerere linaweza kuibuka katika
ziara ya Papa nchini Uganda kwa kutajwa tu, kwa sababu Rais wa nchi
hiyo, Yoweri Museveni, amekuwa na mazingira ya karibu na familia ya
Hayati Mwalimu Nyerere.
“Jukumu la kuendesha mchakato wa kumtangaza Hayati Baba wa Taifa kuwa
Mtakatifu ni letu na linaendelea vizuri. Kuna mambo mengi ya
kuchunguzwa mpaka mtu kutangazwa kuwa mtakatifu, inawezekana Papa
akamzungumzia Mwalimu kwa sababu ya Rais Museveni mara kwa mara
ameonyesha kuguswa na mwenendo wa mchakato huo,” alisema Askofu Kilaini.
Papa Francis aliwasili nchini Uganda jana jioni saa 4:50 na kulakiwa
na Rais Museveni na viongozi wa Kanisa Katoliki nchini humo.
Kwa mujibu wa ziara yake nchini humo iliyotolewa na Kanisa Katoliki
la Uganda leo anatarajiwa kufanya ziara ya kitume katika miji ya
Munyonyo, Nikiyanja, Nalukolongo, Namugongo, Kalolo na Rubaga na kesho
atamaliza ziara yake nchini humo na kusafiri kwenda nchini Afrika ya
Kati (CAR).
Taarifa kutoka nchini Uganda zinaeleza kuwa ulinzi umeimarishwa na
Serikali imeandaa wahudumu wa afya 400 na magari 38 ya kubebea wagonjwa
ambayo yamepelekwa maeneo yote ambayo Papa atayatembelea.
Papa Francis atakuwa Papa wa tatu kutembelea taifa hilo ambapo mwaka
1969, Papa Paul VI alitembelea nchi hiyo akifuatiwa na Papa Paul II
mwaka 1993.
Kampeni za urais zasimama
Katika hatua nyingine wagombea urais wa vyama vyote wamelazimika
kuahirisha mikutano yao ya kampeni kwa ajili ya kupisha ziara ya Papa
Francis nchini humo.
Rais Museveni ambaye anawania urais kwa muhula mwingine, aliwaambia
wafuasi wa chama chake kuwa atamuomba Papa asaidie kutangaza utalii wa
taifa hilo.
Akemea ukabila na rushwa nchini Kenya
Awali kabla hajaondoka nchini Kenya, Papa Francis alihutubia maelfu
ya vijana katika Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi ambapo aliwahimiza
vijana wa taifa hilo wasijihusishe na ukabila.
Alisema vijana wanaweza kuchangia katika kukabiliana na changamoto za
ukabila ambazo zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya mataifa ya Afrika.
Aliwashauri viongozi wa Serikali kuhakikisha vijana wanapata elimu na
ajira kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuwazuia kujiingiza katika
makundi yenye itikadi kali za kigaidi.
Kabla ya kuhutubia vijana katika Uwanja wa Kasarani, Papa Francis,
alitembelea Mtaa wa Kangemi ambako wanaishi watu masikini na kukemea
dhuluma ya huduma bora ambazo wanatakiwa wapatiwe masikini.
“Ninafahamu kuhusu tatizo kubwa linalosababishwa na wawekezaji wasio
na sura ambao hujitwalia ardhi na hata kujaribu kunyakua viwanja vya
kuchezea watoto wenu shuleni. Hili ndilo hufanyika tunaposahau kwamba
Mungu aliwapa watu wote ardhi waitumie kwa maisha yao bila kutenga au
kupendelea yeyote,” alisema Papa Francis.
Created by Gazeti la Mtanzania.
Saturday, 28 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment