RAIS John Magufuli ameeleza muongozo wa Serikali ya Awamu ya Tano,
huku akisema amejipa kazi ya kutumbua jibu, ambalo anajua kuwa utumbuaji
huo unauma, lakini hana namna. Akielezea sababu ya kujipa jukumu hilo,
Dk Magufuli alianza kwa kuelezea mambo aliyolalamikiwa na wananchi
wakati alipokuwa akifanya kampeni, ambapo alitumia barabara kuzungukia
wananchi nchi nzima.
Alisema wakati wa kampeni, alilalamikiwa sana na masuala mbalimbali
hasa rushwa na ufisadi ambao wananchi walionesha hisia zao namna
wanavyochukia kwa kulalamikiwa maeneo yote yanayogusa wananchi.
Maeneo ya rushwa, kero Akianza kutaja sekta na ofisi
zilizolalamikiwa, Dk Magufuli alisema ni pamoja na Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambako alisema kumekuwa na malalamiko ya
ubadhirifu na uchelewaji katika utekelezaji wa miradi au miradi kuwa ya
viwango vya chini. Mbali na Tamisemi, alitaja pia sekta ya ardhi kuwa
imekuwa na migogoro baina ya wakulima na wafugaji na sehemu nyingine
kumeonekana udhaifu katika mipango miji, huku baadhi ya watu wakitumia
fedha kujenga katika maeneo ya wazi.
Dk Magufuli aliendelea kutaja maeneo hayo na baada ya ardhi akahamia
Bandari, ambako alisema imetajwa kuwa na vitendo vya rushwa na wizi na
kutaka watendaji wake wafanye kazi kwa pamoja ili kuondoa malalamiko
hayo. Kero nyingine aliyolalamikiwa, alisema ni pamoja na upatikanaji wa
maji safi na salama, kwamba vyanzo vyake vimekuwa mbali na makazi ya
wananchi na kuongeza kuwa kazi ya Serikali itakuwa kuwatua wanawake ndoo
kichwani.
Mbali na kukosekana kwa maji, Dk Magufuli alitaja Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) akasema imelalamikiwa na ukwepaji wa kodi kwa
wafanyabiashara wakubwa, urasimu na ubadhirifu. Ukiacha malalamiko hayo
ya TRA, Dk Magufuli alisema malalamiko mengine ya wananchi ni katika
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na yalihusu kero ya kukatika kwa
umeme pamoja na mgawo wa mara kwa mara.
Sekta nyingine iliyotajwa kuwa kero kwa mujibu wa Dk Magufuli, ni
maliasili na utalii na malalamiko yake yamejikita katika ujangili, suala
alilosema kuwa watendaji wa sekta hiyo wanahusika, kwani meno ya tembo,
hayawezi kushikiliwa katika nchi za Ulaya bila wahusika kufahamu pamoja
na upotevu wa mapato na migogoro ya mipaka. Rais alisema malalamiko
mengine ni huduma za afya kuwa mbali na wananchi, kutopatikana kwa dawa
na huduma za vipimo, vitendea kazi, rasilimali fedha na watu pamoja na
lugha mbaya kwa wafanyakazi wa sekta ya afya.
Pia wananchi wamemlalamikia kuhusu Idara ya Uhamiaji na utoaji uraia,
kwamba kumekuwa na utaoaji hati na vibali vya kufanya kazi kwa wageni
bila kufuata utaratibu na utoaji vibali vya ajira kwa wageni kwa kazi
zinazofanywa na Watanzania. Katika suala la elimu, alisema kumekuwa na
malalamiko ya michango mingi, maslahi madogo ya walimu, ukosefu wa
miundombinu na nyumba za walimu na masuala mengine ya utoaji elimu
kutopatikana.
Alisema pia Jeshi la Polisi limelalamikiwa kwa kubambikiza kesi
wananchi, kutoa upendeleo kwa walalamikaji, askari kutotimiziwa haki zao
na Jeshi la Zimamoto kuchelewa katika matukio na wakati mwingine kufika
bila maji ya kutosha.
Mizani pia imetajwa katika kero kwa wananchi, kwamba imekuwa
ikichelewesha magari yanayosafirisha bidhaa nje ya nchi, kwa lengo la
kupata rushwa, huku Idara ya Mahakama ikilalamikiwa kwa uchelewaji wa
kesi. Katika sekta ya madini, Dk Magufuli alisema wananchi walilalamika
kutofaidisha wenyeji, kukosekana kwa mikopo kwa wachimbaji wadogo,
ukwepaji kodi na kulipwa fidia kwa wananchi.
Kwa upande wa kilimo na ufugaji, Dk Magufuli alisema kilio kikubwa ni
malalamiko ya kukopwa mazao yao, kukosekana masoko na wataalamu,
kukosekana malambo na majosho, huku uvuvi wakilalamikia vifaa duni,
kukosekana masoko na viwanda huku nchi ikiwa na ukanda wa bahari wenye
urefu wa kilimeta 1,422.
Shirika la Reli nalo halikuachwa, ambapo Dk Magufuli alisema
limelalamikiwa kwa kuwa na miundombinu chakavu, huku Shirika la Ndege
Tanzania (ATC), likiwa na wafanyakazi wengi wanaohangaika na ndege moja
tu.
Kuhusu makundi maalumu, Dk Magufuli alisema kuna malalamiko ya haki
za wazee, walemavu, wanawake na watoto pamoja na kodi za wafanyakazi
kuwa kubwa ikiwemo ya Lipa Kadri Unavyopata (PAYE), hivyo ni lazima
Serikali ijipange kushughulikia na kutatua kero kwa kushirikiana na
Bunge.
Kazi iliyo mbele Baada ya kuorodhesha kero hizo, Dk Magufuli alisema
kazi atakazofanya na mambo atakayosimamia, ni pamoja na udhibiti wa
matumizi ya fedha serikalini kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Dk Magufuli amesema ataunda Serikali ndogo huku akionya watumishi
wazembe akisema wajiandae kwani wakati wa kuchezea na kuchakachua
Watanzania umekwisha na habari za michakato inayoendelea kwenye kazi
serikalini vitakoma kwani wapo wanaolipwa mishahara, lakini hawafanyi
kazi na kufanya serikalini kuwa eneo la kuchuma.
Katika kuongeza mapato na kupunguza matumizi ya Serikali, Dk Magufuli
alisema kwa miaka mitatu iliyopita, ukusanyaji mapato uumekuwa chini ya
makadirio kutokana na wakwepa kodi hivyo sasa atawachukulia hatua na
kuhakikisha kila anayenunua bidhaa anapewa risiti.
Dk Magufuli amesema ataziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali
kwa kuanza na kupunguza safari za watumishi zisizo na lazima nje ya nchi
na badala yake atatumia mabalozi na akilazimika, kiongozi hatakwenda na
misururu ya watu.
Gharama safari za nje Akitoa mfano namna safari hizo zilivyokuwa
zikila fedha, Dk Magufuli alisema zaidi ya Sh bilioni 356.3 zilitumika
kwa safari za nje, ambapo tiketi za ndege ilikuwa Sh bilioni 183.16,
mafunzo ya nje Sh bilioni 68.62 na posho za kujikimu Sh bilioni 104.552.
Alisema Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Fedha, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Wizara ya
Mambo ya Ndani, ndiyo zinaongoza kwa matumizi ya fedha nyingi za safari
za nje, wakati fedha hizo zingetumika kuboresha maisha ya Watanzania na
zingeweza kutengeneza barabara ya kilometa 400.
Aliwaomba wabunge kumsaidia katika kudhibiti matumizi, kwani suala
kama la mafunzo, badala ya kundi la watumishi kwenda nje ya nchi,
wangeweza kumleta mwalimu nchini na kupata mafunzo husika.
“Hatuwezi kutatua matatizo yaliyopo kwa kuendelea kuwa na matumizi ya
hovyo, kuna mtu kasafiri nje ya nchi kuliko alivyokwenda kumsalimia
mama yake,” alisema na kufanya wabunge kuangua kicheko.
Alisema pia katika kudhibiti matumizi, atadhibiti semina, warsha na
makondamano yasiyo na tija, kwani siku hizi wizarani lazima wakutane
hotelini hata kama kuna ukumbi wakati suala lenyewe, hata kwenye mti
wanaweza kukutana na kulijadili.
Akizungumzia Sheria ya Manunuzi, Dk Magufuli alisema ni mdudu
mwingine mbaya kwani nyumba inayojengwa kwa Sh milioni 30 kwa sheria
hiyo itajengwa kwa Sh milioni 200 au peni ya Sh 1,000, itanunuliwa kwa
Sh 10,000. Alisema sheria hiyo ni mbaya katika kudhibiti matumizi ya
Serikali na kuwataka wabunge kumuunga mkono wakati muswada wa
marekebisho ya sheria utakapopelekwa bungeni. Rushwa Dk Magufuli alisema
atapambana bila kigugumizi dhidi ya vitendo vya rushwa kwani dawa ya
jipu ni kutumbua na anajipa kazi hiyo ya kutumbua majipu ingawa anajua
kuna maumivu lakini hakuna dawa nyingine.
“Naomba mniombee wakati nikitumbua majipu, nawaomba na wabunge
mniunge mkono kwani najua changamoto na ugumu wa kutumbua majipu kwani
wanaojihusisha na vitendo hivi, ni wakubwa wenye dhamana ya utumishi
walioomba ridhaa kwa wananchi,” alisisitiza.
Alisema kutokana na dhamira yake hiyo, ameamua kuunda Mahakama ya ya
Rushwa na Ufisadi na kutaka vyombo vinavyohusika kumuunga mkono.
Dk Magufuli pia alitoa onyo kwa viongozi atakaowateua, kukumbuka
kwamba anayo mamlaka ya kuwawajibisha akibaini wanajihusisha na vitendo
vya rushwa na ufisadi, kwani atawatimua mara moja na baada ya hapo hatua
za kisheria zitafuata.
Alisema Watanzania wana maisha ya chini na wameshindwa kunufaika na
rasiliamli zao, wakati nchi yao ni tajiri hivyo Serikali itafuatilia
mienendo ya watendaji wake na wakibainika kuwa na vitendo hivyo,
watachukua hatua katika ngazi zote.
Katiba mpya, madini Kuhusu Katiba mpya, alisema Serikali ya Awamu ya
Tano imekuta kiporo cha katiba ambacho hakikukamilika kuandikwa,
kutokana na kuchelewa kwa suala la kuandikishwa wapigakura na kwa
kuthamini haki ya wananchi waliotoa maoni yao ya katiba mpya, Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na Bunge la Katiba, serikali yake itatekeleza
wajibu wake.
Rais Magufuli pia alizungumzia kuimarisha misingi imara ya kiuchumi
kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara za mikoa, wilaya na katika ameneo
muhimu. Alisema uboreshaji wa barabara, bandari utafanyika pamoja na
ujenzi wa reli mpya kwa kiwnago cha kimataifa kutoka Dar es Salaam-
Tabora-Kigoma hadi Mwanza na Uvinza –Burundi, Mtwara-Songea- Bambabay na
kwingineko.
Akizungumzia suala la madini, maliasili na gesi asilia, alisema
yatatumika kwa manufaa ya Taifa kwa kuzingatia sheria na taratibu huku
akipongeza Sheria Mpya ya Usimamizi wa Mapato ya Gesi iliyopitishwa na
Bunge la 10.
Created by Gazeti la bahariLeo
Saturday, 21 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment