Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.
SPIKA wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anatarajiwa
kuchaguliwa mjini hapa Jumanne ijayo, ratiba ya Bunge hilo imeeleza.
Kutokana na ratiba hiyo, ni wazi Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitalazimika
kumtaja mgombea wake atakayekuwa na nafasi kubwa ya kuwa Spika kati ya
kesho na keshokutwa na kumaliza mvutano wa nani anafaa kuwa spika, baada
ya wanachama 22 kujitokeza mpaka jana kuwania nafasi hiyo.
“Kutokana na kuitishwa kwa Bunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dk John Pombe Joseph Magufuli... Ofisi ya Bunge
inapenda kuwatangazia wabunge wateule wote kuwa wanatakiwa kuwasili
mjini Dodoma Novemba 13, 2015 (jana) tayari kwa ajili ya usajili
utakalofanyika bungeni kuanzia siku hiyo hiyo,” imeeleza ratiba hiyo
iliyowekwa katika ukurasa wa Facebook wa Bunge.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kuanzia jana mpaka kesho, wabunge wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watapaswa kuwa wameshawasili mjini
Dodoma na kujisajili kwa watumishi wa Bunge ambao wameshaanza kazi hiyo.
Baada ya kazi hiyo, ratiba ya Bunge hilo imeonesha kuwa keshokutwa
siku ya Jumatatu, wabunge wote wanatarajiwa wawe wameshajisajili ili saa
nne asubuhi washiriki kikao cha maelekezo katika Ukumbi wa Bunge
kitakachohusisha kutembelea ukumbi huo.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa siku hiyo hiyo kuanzia saa 10 jioni,
wabunge hao watakuwa na mikutano ya vyama vyao, ambako inatarajiwa hoja
kubwa itakuwa jina la Spika na Naibu Spika.
Spika Siku ya Jumanne wiki ijayo, Watanzania wataelekeza macho yao na
masikio katika Kikao cha Kwanza cha Bunge la 11 mkoani hapa, ambacho
kitatanguliwa na kusomwa kwa tamko la Rais Magufuli la kuitisha Bunge.
Mara baada ya kusomwa kwa tamko hilo, kutafuatiwa na uchaguzi wa
Spika utakaofanyika kwa kura za siri na mshindi akishatangazwa, atakula
kiapo siku hiyo hiyo, kisha atapigiwa Wimbo wa Taifa na dua itasomwa.
Siku hiyo hiyo, Spika huyo anatarajiwa kuanza kuapisha wabunge na
kazi hiyo ataendelea nayo siku ya Jumatano na kumalizia siku ya Alhamisi
asubuhi kwa wabunge watakaokuwa hawajala kiapo cha uaminifu.
Waziri Mkuu, Naibu Spika Alhamisi ya Novemba 16, saa 10 jioni Rais
Magufuli anatarajiwa kupeleka kwa Spika jina la Waziri Mkuu ambalo
litasomwa mbele ya wabunge wote na kuthibitishwa na wabunge kwa kura.
Baada ya kuthibitishwa kwa Waziri Mkuu, siku hiyo hiyo Naibu Spika
atachaguliwa na kula kiapo cha uaminifu na baada ya hapo wabunge
watajiweka tayari kwa Hotuba ya Kwanza ya Rais Magufuli itakayotolewa
Ijumaa saa kumi jioni na kufuatiwa na kuahirishwa kwa Bunge.
Wabunge wawasili Jana gazeti hili lilishuhudia wabunge mbalimbali
wakiingia bungeni na kwenda kusajiliwa katika meza zilizokuwa na
watumishi wa bunge hilo. “Umerudi na wewe bungeni? Aaah umemwangusha
Waziri ndugu yangu, sikuwezi unatisha sana,” hizo zilikuwa baadhi ya
kauli zilizokuwa zikisikika kwa wabunge mbalimbali walipokuwa
wakisalimiana mjini hapa.
Kauli hizo zilikuwa zikitumika kwa wabunge wa zamani waliokuwa
wakisalimiana wakati wa shughuli ya kujisajili. Wabunge kadhaa walikuwa
wakitaniana, huku wakipigana vijembe mbalimbali na wengine
wakikumbatiana kwa furaha na kuonesha kushukuru Mungu kwa kuwarudisha
tena bungeni.
“Uchaguzi sio mchezo, huko majimboni kuna changamoto nyingi sana,
tumetukanwa, tumesemwa vibaya, lakini hatimaye tumeshinda,” alisema
Mbunge wa Kavuu, Dk Pudenciana Temba (CCM).
“Sikuwa na sababu ya kuhofia, niliwafanyia wananchi wangu mambo
makubwa, barabara sehemu kubwa zinapitika, ndiyo sababu wamenirudisha
tena,” alisema Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM), alipokuwa
akizungumza na baadhi ya wabunge wenzake.
Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM), aliwashukuru
wapiga kura wake na kusema kuwa kazi yake ndiyo iliyomrudisha tena
bungeni. Ngonyani alikuwa akiwapiga vijembe wenzake itabidi afanye
utafiti wamerudi namna gani bungeni, huku pia Shabiby akimtania kwamba
naye anajua namna alivyowadhibiti wapinzani wake.
Kwa ujumla wabunge wa vyama vyote waliojiandikisha jana walionekana
kuwa na furaha na kupongezana kwa namna mbalimbali wakitakiana kila la
heri. Kivutio kikubwa ilikuwa kwa wabunge wapya, ambapo watumishi wa
Bunge waliokuwa wakipokea wageni walipata wakati mgumu kwa wale ambao
hawawafahamu hivyo kulazimika kila wanayemuona kumuuliza kama ni
Mheshimiwa au la ili wapate kumuelekeza eneo la kupelekwa.
Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema), alisema anashukuru
kushinda kwani alipambana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
(Uwezeshaji na Uwekezaji), Christopher Chiza na kwamba ilikuwa uchaguzi
si wa kitoto.
Bunge la sasa linatarajiwa kuwa na wabunge 393, ambapo ni wabunge wa
majimbo 264, huku wa viti maalumu wakiwa 113 na wale wa kuteuliwa na
Rais wakiwa 10 wa kutoka Baraza la wawakilishi watano na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali mmoja.
Bunge la 10 lililomalizika Agosti 21 mwaka huu lilikuwa na wabunge
357, ambapo wa majimbo walikuwa 239, viti maalum 102, wateule wa Rais
kumi, Baraza la wawakilishi watano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Saturday, 14 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment