Mgombea Usipika kwa Chama Cha Mapinduzi, Job Ndugai akiongea na waandishi wa habari
baada ya kuchaguliwa kugombea nafasi hiyo kwenye kikao maalumu cha
kamati ya wabunge wote wa chama hicho mji.
UCHAGUZI wa Spika wa Bunge la Tanzania unatarajiwa kufanyika leo
ambapo wagombea wanane kutoka vyama tofauti wamejitosa kuwania nafasi
hiyo katika Bunge la 11 linalotarajiwa kuanza leo mjini hapa.
Akizungumza mjini hapa jana, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah
alisema mwisho wa vyama vya siasa kuwasilisha majina kwenye ofisi yake
ilikuwa jana saa 10 alasiri. Aliwataja watakaopigiwa kura leo na vyama
vyao katika mabano ni Peter Leonard Sarungi (AFP), Hassan Kisabya Almas
(NRA), Dk Godfrey Rafael Malisa (CCK), Job Yustino Ndugai (CCM), Godluck
Joseph ole Medeye (Chadema), Richard Shedrack Lyimo (TLP), Hashim
Spunda Rungwe (Chaumma) na Robert Alexander Kasinini (DP).
Kati ya wagombea hao, ni Ndugai peke yake ambaye ni Mbunge katika
Bunge la 11 ambaye katika Bunge la 10 lililomalizika Agosti mwaka huu,
alikuwa Naibu Spika. Ndugai ni Mbunge wa Kongwa tangu mwaka 2000. Kwa
upande wa Ole Medeye amepata kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne na hadi Agosti
alikuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi kupitia CCM.
Alikihama chama hicho tawala Agosti mwaka huu, na alikuwa mshirika
mkubwa wa mgombea urais kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
huu, Waziri Mkuu aliyejiuzulu mwaka 2008, Edward Lowassa. Kwa upande
wake, Rungwe ambaye kitaaluma ni mwanasheria, aligombea urais katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kupitia Chaumma na mwaka 2010 aligombea
kupitia chama cha NCCR-Mageuzi.
Dk Kashililah alisema hadi kufikia mchana jana, wabunge 348 walikuwa
wameshajisajili kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha Kwanza cha
Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 11. Mapema jana, Ndugai aliibuka kidedea
kuwania nafasi hiyo kwa CCM baada ya wagombea wengine wawili kujitoa.
Juzi Kamati Kuu ya CCM iliteua majina matatu na kuyawasilisha kwenye
Kamati ya Wabunge wa CCM ili yapigiwe kura kupata jina moja
litakalopelekwa bungeni kupigiwa kura na wabunge wote kwa nafasi ya
Spika leo.
Pamoja na Ndugai, wengine walikuwa ni Abdullah Ali Mwinyi ambaye ni
Mbunge wa Afrika Mashariki na Dk Tulia Ackson Mwansasu ambaye alikuwa
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali mpaka jana alipoteuliwa na Rais John
Magufuli kuwa Mbunge wa Bunge la Tanzania.
“Wagombea wengine wawili wamejitoa kwa sababu wana imani kubwa na
Ndugai, hivyo kwa vile CCM ina wabunge wengi ambao ni sawa na asilimia
74.8 ya wabunge wote waliopo bungeni hadi sasa, hatuna shaka kwamba huyu
atakuwa Spika,” alisema Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alipozungumza na waandishi wa habari jana katika Ukumbi wa White House
mjini hapa.
Akizungumza baada ya kupitishwa, Ndugai aliwashukuru wabunge wenzake
na kwamba kama leo akichaguliwa atakuwa Spika atakayetenda haki kwa
wabunge wote na atakuwa Spika bora. “Tumeambiwa kwamba ilikuwa ‘Hapa
Kazi tu’, lakini kwa sababu tushaanza kazi tuseme ‘Sasa Kazi Tu’, nami
itakuwa vivyo hivyo,” alisema Ndugai na kueleza kuwa Bunge la safari hii
litakuwa na changamoto kubwa kwani lina wabunge wengi vijana na pia
wasomi wameongezeka.
Awali, akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana aliwapongeza wabunge wa chama hicho kwa ushindi
walioupata na kuwataka waendeleze kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwa
kufupisha maneno ‘Sasa Kazi Tu’ kwa vile tayari wameanza majukumu yao.
Uchaguzi huo ulisimamiwa na wajumbe wa Kamati Kuu ambao ni Jerry Silaa,
William Lukuvi na Dk Maua Daftari.
Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama ambaye ni Mbunge wa
Peramiho akizungumza kabla ya kumkaribisha Kinana, alisema wabunge wote
wa CCM hadi sasa ni 252 na waliohudhuria jana walikuwa 228. Watanzania
wengine waliowahi kushika nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania ni Adam
Sapi Mkwawa kuanzia 1964 hadi Novemba 19, 1973, Chifu Erasto Mang'enya
Novemba 20, 1973 hadi Novemba 5, 1975, Mkwawa tena kuanzia Novemba 6,
1975 hadi Aprili 25, 1994.
Wengine ni Pius Mseka Aprili 28, 1994 hadi Novemba 20, 2005, Samuel
Sitta Desemba 26, 2005 hadi Novemba 2010, kisha Makinda Novemba 12 hadi
leo atakapopatikana Spika mpya. Naibu Spika Uchaguzi wa Naibu Spika
utafanyika Alhamisi wiki hii ambapo jana Muungano wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) ulisema tayari ulikamilisha mchakato wa kupata mgombea
wake.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene aliwaambia waandishi wa
habari kuwa Ukawa watamsimamisha Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena
Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua mkoani Tabora. Alisema Ukawa
walifanya vikao kadhaa kufikia uamuzi huo kuanzia ngazi ya vyama,
wabunge na kisha viongozi wa juu na kupata majina mawili ambayo ni Ole
Medeye kwa Uspika na Sakaya kwa Naibu Spika.
Kwa upande wa CCM, wenyewe walianza kutoa fomu jana, ambapo habari
zilizopatikana jana ni kuwa wabunge saba wa chama hicho walikuwa
wamejitokeza kuwania nafasi hiyo. Tofauti na ilivyokuwa katika mchakato
wa Spika, ambapo wanaochukua fomu walikuwa wakitangazwa, hali ni tofauti
kwa nafasi hiyo ambapo imeelezwa Kamati ya Wabunge wa CCM ndiyo
inayosimamia.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, miongoni mwa waliojitokeza jana kuchukua
fomu ni Dk Tulia na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu. Hata hivyo,
Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama hakuwa tayari
kuzungumzia suala hilo jana na kusema kuwa hawawezi kutaja majina wala
idadi kwa sababu uchukuaji fomu bado unaendelea.
Alisema leo wabunge wa CCM watakutana kwa ajili ya kupiga kura
kuchagua mbunge mmoja kati ya wabunge watakaojitokeza kwa ajili ya
nafasi ya Naibu Spika.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Monday, 16 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment