Rais John Magufuli amezifumua na kuziunda upya baadhi ya ofisi za Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam pamoja na kuwaondoa baadhi ya watumishi ambao hawana ulazima katika mfumo wa utumishi wa Ikulu.
Taarifa za uhakika zilizotufikia
kutoka ndani ya Ikulu zimeeleza kuwa Rais Magufuli alianza kufanya
ukaguzi wa ofisi moja baada ya nyingine zilizo Ikulu huku akitaka
maelezo ya kina kuhusu shughuli zake na aina ya watendaji waliopo.
Mmoja
wa maofisa waandamizi wa Ikulu aliyezungumza kwa sharti la jina lake
kuhifadhiwa, alisema katika ukaguzi huo, Rais Magufuli aliamuru kufungwa
mara moja kwa baadhi ya ofisi alizobaini kuwa hazina tija na kwamba
zina watumishi ambao ni mizigo.
Ofisa
huyo alizitaja baadhi ya ofisi zilizofungwa kuwa ni pamoja na iliyokuwa
ikishughulikia chakula cha rais na ile iliyokuwa ikijihusisha na
kupokea wageni binafsi wa rais.
“Rais
Magufuli alipoingia tu Ikulu alifanya ziara ya kukagua ofisi zote
zilizopo Ikulu, alitaka kujua utendaji kazi wa ofisi hizo lakini
alipofika kwenye kitengo maalumu cha lishe ya rais alisema haoni umuhimu
wa kuwepo kwa ofisi hiyo kwa sababu suala la lishe yake siku zote
linasimamiwa na mkewe Janeth. Akaamuru ifungwe na watumishi wake
warejeshwe walikotoka.
"Ofisi
nyingine aliyoamuru ifungwe ni kupokea wageni binafsi wa rais. Alisema
haoni tija ya kuwepo kwa ofisi hiyo kwa sababu mgeni anatakiwa kufika
Ikulu baada ya kutoa taarifa, nayo aliamuru ifungwe,” alisema ofisa huyo.
Taarifa
zaidi zimeeleza kuwa aliyekuwa mkuu wa kitengo cha lishe Ikulu
amerudishwa katika ajira yake ya awali Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, huku watumishi wengine wakipelekwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Alipotafutwa
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kupitia simu ya kiganjani
kuzungumzia hatua hiyo, simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa na
hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno ulionyesha kupokelewa kwenye
simu yake lakini haukujibiwa.
Alipoulizwa
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga kuhusu kuwepo kwa
hatua hizo alisema ni kweli Rais Magufuli alipoingia ofisini alianza
kuipanga upya Ikulu kulingana na matakwa yake wakati wa utawala wake.
Premi
ambaye alizungumza kupitia simu yake ya kiganjani alisema wakati wa
utawala wa Serikali ya awamu ya nne kulikuwa na ofisi maalumu ya lishe
Ikulu ambayo hata hivyo ilikuwa haihusiani na uandaaji wa chakula cha
rais.
Alisema
ofisi hiyo ilikuwa mahususi kwa ajili ya ushauri kuhusu programu ya
kimataifa ya urutubishaji wa vyakula kwa lengo la kupunguza tatizo la
udumavu wa watoto.
“Ofisi
hiyo ilikuwa inaongozwa na mtaalamu wa masuala ya lishe hata hivyo
kabla ya Rais Kikwete kumaliza muda wake mtaalamu huyo aliacha kazi yake
na kwenda kugombea ubunge huko kwao sasa ukiniambia amerudishwa Wizara
ya Afya sitakuwa na jibu la uhakika kwa sababu sifahamu,” alisema Premi.
Alipoulizwa
kuhusu kufungwa kwa ofisi ya wageni binafsi wa Rais, Premi alisema
ilikuwa na kazi ya kupokea malalamiko ya wananchi lakini Rais Magufuli
ameamua kuiondoa kwa sababu ameweka utaratibu wa malalamiko ya wananchi
kupokewa kuanzia ngazi za chini.
“Kama
unavyojua Rais amekuja na dira yake ya ‘hapa kazi tu,’ hivyo anataka
watendaji wa ngazi zote wawajibike kwa ufanisi. Wakati wa utawala wa
Rais Kikwete alifungua dawati hilo kwa ajili ya kusikiliza matatizo ya
wananchi, watu walitoka mikoa ya mbali kuleta kero zao hapa Ikulu lakini
Rais Magufuli ameamua malalamiko ya wananchi yasikilizwe kuanzia ngazi
za chini.
“Rais
Magufuli anataka watendaji wote wa Serikali wawajibike kupokea kero za
wananchi na kuzifanyia kazi. Zipo ofisi za madiwani, wabunge, wakuu wa
wilaya na wakuu wa mikoa ambao wote wanalo jukumu la kuwasikiliza
wananchi na kuwatatulia kero zao,” alisema Premi.
Credit:Mtanzania
Credit:Mtanzania
Credit; Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment