Mwanamume mmoja nchini India ameshangaza wengi baada ya kukataa kumpigia kura mamake uchaguzini.
Mwanamke
huyo Jagadamma Kumar alikuwa akiwania kiti cha udiwadi kupitia chama
tawala cha BJP katika jimbo la Kerala, na alikabiliwa na upinzani mkali.Lakini mwanawe Rajesh Kumar, ambaye ni konstebo wa polisi, aliamua kuunga mkono mgombea wa upinzani na kusema upendo kwa mama yake haungemzuia “kutekeleza wajibu wangu kwa taifa.”
Aliamua kueleza sababu zake kutompigia mamake kura kwenye ujumbe kupitia Facebook.
Ajabu ni kwamba kura yake huenda ingekuwa muhimu sana kwani mamake alishindwa kwa kura sita pekee.
“Mamangu alikuwa mwalimu shule niliyosomea, lakini aliposahau ahadi yake kwa taifa ambayo mwenyewe alinifunza, niliamua kuandika hapa kumkumbusha mamangu ahadi hiyo,” aliandika.
Aliendelea na kukosoa juhudi za chama cha BJP kutimiza ahadi zake, ikiwemo kampeni ya Waziri Mkuu Narendra Modi kuangamiza tabia ya watu kutotumia vyoo wakati wa kwenda haja.
Utafiti mmoja mwaka jana ulibaini kuwa asilimia 70 ya raia nchini humo hawatumii vyoo.
Rajesh Kumar alisema mikakati ya chama hicho haifanikiwi katika maeneo mengi ya nchi hiyo.
Aliambia BBC Trending kwamba uhusiano wake na mamake haujaathiriwa na hatua hiyo yake.
“Mamangu alisema ni haki ya kuamua msimamo wangu kisiasa,” alisema.
Baada ya kuandika ujumbe wake Facebook, kunao waliounga mkono hatua yake.
"Nakuheshimu sana kaka,” aliandika mmoja wao.
Lakini kunao waliomshutumu na kusema alimkosea heshima mamake.
Created by BBC Swahili.
0 comments:
Post a Comment