KASI ya Rais John Magufuli imeendelea kutikisa idara na taasisi
mbalimbali za serikali kutokana na mchakamchaka miongoni mwa watendaji
na wasimamizi wanaoendelea kuasa watumishi walio chini yao, kutii
falsafa ya ‘Hapa Kazi Tu’ vinginevyo watajiondoa kwenye mfumo.
Ari ya uwajibikaji imeonekana kutawala kwenye taasisi mbalimbali za
serikali zikiwemo halmashauri ambako baadhi ya watendaji wameweka bayana
kutokuwa tayari kugeuzwa mbuzi wa kafara kwa kutowajibika kwa watumishi
walio chini yao. Miongoni mwa halmashauri ambazo wakurugenzi wake
wamekaririwa wakisema hawako tayari kuadhibiwa kwa kushindwa kusimamia
kasi ya Dk Magufuli ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Songea
Vijijini.
Akizungumza na wakuu wa idara juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri hiyo, Sigsbert Kaijage, aliwataka wafanyakazi kuhakikisha
wanakwenda na kasi ya Rais Magufuli chini ya kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’
ili kuinua hali ya maisha ya wananchi na uchumi wa wilaya kwa ujumla.
“Mimi sikubali kugeuzwa mbuzi wa kafara kwa niaba yenu.
Nahitaji kila mmoja kutekeleza wajibu wake na kama kuna mtu anaona
hataki kufanya kazi katika halmashauri hii kutokana na maslahi, basi ni
vizuri akatafute maeneo mengine, lakini siyo kuendelea kung’ang’ania
huku ukishindwa kuleta tija mahali pa kazi,” alisema Kaijage.
Licha ya wakuu wa taasisi mbalimbali kuandaa vikao maalumu kwa ajili
ya kuwasilisha maagizo ya rais kwa watumishi walio chini yao, vile vile
katika vikao au hafla zinazowakutanisha na watumishi wa chini yao,
wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kubadilisha mfumo na kuondokana na
kufanya kazi kwa mazoea.
Juzi kwenye hafla ya kumuaga aliyekuwa Ofisa Tarafa ya Namanyere,
Nimrod Kaishozi ambaye amestaafu kisheria, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi
mkoani Rukwa, Idd Kimanta aliendelea kutumia nafasi hiyo kuhimiza
umuhimu wa watumishi kubadilika na kuendana na kasi ya Magufuli.
Kimanta alisema mtumishi atakayeshindwa kuendana na ‘Hapa ni Kazi
Tu’, atafute mlango wa kutokea haraka iwezekanavyo. Alikiri kuwapo
watumishi ambao ni wagumu kuendana na mabadiliko huku akiwahadharisha
dhidi ya kufanya kazi kwa mazoea. “Falsafa ya Rais Magufuli na Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa haizungumzwi tu, bali inakwenda kwa vitendo…
Ambaye anaona kuwa hataendana na kasi hiyo, ni bora akaamua kuondoka
mapema kabla ya kuondolewa kazini,” alisema Mkuu wa Wilaya.
Aliwaonya wanaoendekeza itikadi za kisiasa akisema kitakachofuata ni
hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi yao vinginevyo, waamue mapema
kuacha kazi. Alisema ameshatoa maelekezo kwa watumishi wote wa Serikali
kujipambanua upya. “Inasikitisha kuona baadhi yao wameendekeza siasa na
kuacha mambo ya msingi ya kuwatumikia wananchi kama ilivyo katika
miongozo yao ya kiutumishi,” alisema.
Akisisitiza uwajibika, Kimanta aliwaambia kwamba kama ambavyo wengi
walimuona ama kumsikia Dk Magufuli akihutubia Bunge la 11, mambo
aliyosema alimaanisha utekelezaji na uwajibikaji. Alisisitiza kwamba
kama yupo mtu anayeona ni utani, ataanza naye kummaliza.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fadhili Nkulu, alitoa rai kwa wahitimu
wa Chuo cha Uhasibu kilichoko Arusha kutumia taaluma walizopata kwa
kuitikia kaulimbi ya ‘Hapa Kazi Tu’. “Nawasihi mkatumie taaluma yenu
vizuri, sababu serikali tulionayo ‘sasa ni kazi tu’. Atakayeleta mchezo
atakuwa anachezea kibarua chake mwenyewe,” alisema Nkulu aliyekuwa mgeni
rasmi katika mahafali ya 17 ya chuo hicho.
Tangu Rais Magufuli alipoapishwa Novemba 5 na kuweka wazi msimamo
wake kuhusu uwajibikaji, watumishi serikalini wameendelea kuhadharishwa
wakiambiwa atakayeshindwa kuendana na mabadiliko, yuko kwenye hatari ya
kupoteza kazi. Makatibu wakuu wa wizara mbalimbali wameendelea kukutana
na taasisi zilizo chini yao kueleza maagizo ya rais kwa ajili ya
utekelezaji.
Hotuba yake bungeni iliyopigilia msumari msimamo wake, imeendelea
kuibua mjadala mkubwa kwenye majukwaa mbalimbali, ikiwemo mitandao ya
kijamii na vyombo vya habari. Wachangiaji wengi wameasa watendaji wa
umma wanapaswa kutekeleza maagizo ya rais vinginevyo, wapo watakaopoteza
ajira. Wasomi, wanasiasa na viongozi wa sekta mbalimbali binafsi,
wameelezea hotuba yake kuwa ya kihistoria inayoonesha dhamira ya kweli
kwa nchi.
Maeneo ambayo rais aliyatilia mkazo katika hotuba yake, ni pamoja na
ukusanyaji wa mapato ambao alisema umekuwa chini ya makadirio kutokana
na sababu mbalimbali. Udhibiti wa safari zote za nje ya nchi zisizo za
lazima kwa ajili ya kupunguza matumizi, ni eneo ambalo liliibua mjadala
mkubwa hususani baada ya rais kutoa takwimu za baadhi ya taasisi za
serikali zilizoongoza kwa kutumia fedha nyingi kutokana na safari hizo.
Miongoni mwa wasomi waliokaririwa na gazeti hili, ni Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana
aliyesema watendaji wa umma wanapaswa kutekeleza maagizo huku akisema
sasa utakuwa mwisho wa kufanya kazi kwa mazoea. Kwa upande wake, Mbunge
wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT Wazalendo), alisema mtu atakayempinga
Magufuli, analinda mafisadi na ana maslahi nao.
Created by gazeti la HabariLeo
Sunday, 22 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment