LEO ni siku nyingine muhimu katika historia ya Serikali ya Awamu ya
Tano nchini, ambapo Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
linaanza kazi yake rasmi mjini Dodoma.
Wabunge wataanza kazi yao ya kwanza kwa kumchagua Spika wa Bunge hilo
atakayeliongoza kwa miaka mitano ijayo, kisha kuapishwa kwake na
hatimaye yeye kuwaapisha wabunge wenyewe.
Hakuna ubishi kwamba tukio la leo linafuatia mchakato ulioanza siku
nyingi, ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa kuteua wagombea wao katika
nafasi za udiwani, ubunge na urais, kuteuliwa rasmi na Tume ya Uchaguzi
ya Taifa (NEC), kugombea nafasi hizo katika kura za maoni, kuanza kwa
kampeni na hatimaye kufanyika kwa uchaguzi mkuu wenyewe Oktoba 25.
Tuna kila sababu ya kujivuna kwamba mchakato mzima ulikwenda vizuri
kwa amani na utulivu hadi kupatikana kwa viongozi hao wote katika nchi
yetu, ukiacha maeneo na majimbo machache ambayo yanarudia uchaguzi
kutokana na sababu mbalimbali za msingi.
Hatua ya kumchagua Spika wa Bunge la 11 inayofanyika leo, ni sehemu
ya mchakato mzima wa uundaji wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa mujibu wa
katiba ya nchi yetu. Mchakato wa kumtafuta Naibu Spika nao uko mbioni.
Tunapenda kuwakumbusha waheshimiwa wabunge wateule kuzingatia
utamaduni wetu tuliojijengea sisi kama Watanzania wa kuendesha mambo
yetu muhimu yanayohusu nchi yetu kwa amani, utulivu na mshikamano na
pale ambapo tutabishana basi tufanye kwa msingi wa hoja yenye mashiko
kwa taifa letu na siyo hoja ya nguvu.
Tunafahamu kwamba vyama na hata watu binafsi wanashindania nafasi
hiyo nyeti. Lakini ni ukweli pia kwamba kujitokeza wagombea zaidi ya
mmoja katika kinyang’anyiro hicho ni kipimo tosha, kwamba tuna kila
sababu ya kumchagua Spika makini atakayekuwa na uwezo wa kuliongoza
Bunge letu kwa weledi, umakini, busara na uvumilivu unaostahiki
tukizingatia kwamba wabunge wetu safari hii wametoka katika mchanganyiko
mkubwa wa vijana, wenye umri wa kati na wazee.
Wakati tunawatakia kila la heri wabunge wetu kutupatia Spika makini,
tunawaomba busara itawale ili shughuli yote ifanyike kwa mujibu wa
sheria na katiba ya nchi yetu, kwa amani, utulivu na mshikamano.
Pamoja na ukweli wa utofauti wa itikadi za vyama mbalimbali, jambo la
msingi hapa ni kumpata mwenye uwezo na sifa stahiki ya kutuongoza kwa
lengo la kuendeleza demokrasia ya vyama vingi nchini mwetu bila kuleta
mifarakano.
Tunawatakia uchaguzi wa amani wa Spika wa Bunge la 11 la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Naibu Spika na pia kuthibitisha jina la Waziri
Mkuu litakaloletwa kwao na Rais John Magufuli
Created by gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 17 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment