WABUNGE wamesifu hotuba ya ufunguzi wa Bunge la 11 iliyotolewa
bungeni jana na Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli. Hotuba hiyo ni
ufunguzi rasmi wa Bunge la 11, ambapo mkutano wa kwanza wa bunge hilo
ulianza Jumanne wiki hii mjini hapa.
“Ni hotuba nzuri sana, ambayo naonesha dira ya kule tunakotaka
kwenda, nampongeza sana Rais sasa ni suala la utekelezaji,“ alisema
Mbunge wa Bukene, Selemani Zedi (CCM).
Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), ambaye
alikuwa mbunge pekee wa upinzani aliyekuwepo ukumbini wakati hotuba hiyo
ikisomwa, alipongeza hotuba hasa katika suala la viwanda kwamba ni moja
ya maeneo ambayo naye alikuwa akiyapigia kelele.
Alisema pia Rais ametaja changamoto nyingi zilizopo katika jamii na
kwamba tayari bunge lishazinduliwa basi ni jukumu la kwenda kufanya
kazi, huku pia akipongeza suala la kudhibiti matumizi ya fedha za
serikali.
Naye Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM) alipongeza hotuba
hiyo kwa kusema inaonesha jinsi gani Rais Magufuli alivyopania
kuwasaidia Watanzania na kwamba kilichobaki sasa ni kwa watendaji
kufanya utekelezaji. Mbunge wa Korogwe Mjini, Stephen Ngonyani (CCM),
alisema hotuba hiyo haina ilichobakisha na sasa ni suala la kufanya kazi
tu ili kutekekeleza yaliyozungumzwa.
Kwa upande wake Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Mgumba Omary
(CCM), alisema hotuba hiyo ni dira nzuri kwa Taifa hasa suala la elimu,
viwanda, nishati ya gesi na vipaumbele vingine mbalimbali. yakati
tofauti walisifu hotuba hiyo ni Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, Mbunge wa
Nzega Vijijini, Dk Hamis Kigwangwala wote wa CCM wakisema imeonesha wapi
Serikali ya Awamu ya Tano inakotaka kuipeleka nchi.
“Ni moja kati ya hotuba bora kabisa, imegusa maeneo yote, Rais
amezungumza kwa msisitizo na unaona kabisa kwamba ana nia ya dhati ya
kuwaletea Watanzania maendeleo,” alisema Dk Kigwangwala.
Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisifu hotuba hiyo na kusema
wabunge wataijadili katika kikao kijacho kinachotarajiwa kuanza Januari
20, mwakani. Kwa upande wakati akisoma hotuba ya kuahirisha bunge,
Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, alisema hotuba hiyo ni ya aina
yake na kwamba Rais ameeleza kwa kina kuhusu wajibu kujenga nchi.
“Nimpongeze sana Mheshimwa Rais kwa hotuba yake nzuri, ambayo ndiyo muongozo wetu kuanza kutekeleza majukumu yetu,” alisema.
Created by gazeti la habariLeo
Saturday, 21 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment