Tuesday, 24 November 2015

Tagged Under:

Marekani kuwekea vikwazo wakuu wanne Burundi

By: Unknown On: 02:16
  • Share The Gag
  • Machafuko yamekuwa yakiendelea Burundi tangu Aprili
    Marekani imesema itawawekea vikwazo maafisa wakuu wanne wa sasa na wa zamani Burundi kuhusiana na machafuko ambayo yamekuwa yakiendelea nchini humo.
    Wanne hao ni pamoja na waziri wa usalama wa umma na naibu mkuu wa polisi.
    Mali ya wanne hao itazuiwa na pia watanyimwa viza.
    Marekani inasema hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kusisitiza aongoze kwa muhula wa tatu imezidisha machafuko hayo ambayo yamesababisha kuuawa kwa watu zaidi ya 240 tangu Aprili.
    Visa vya mauaji vimeongezeka wiki za hivi karibuni na miili inapatikana mara kwa mara barabarani.
    Watakaowekewa vikwazo na Marekani ni:
    • Waziri wa usalama wa umma Alain Guillaume Bunyoni
    • Naibu mkuu wa polisi, Godefroid Bizimana
    • Mkuu wa zamani wa ujasusi Godefroid Niyombare
    • Waziri wa zamani wa ulinzi Cyrille Ndayirukiye
    Bw Niyombare na Ndayirukiye waliongoza jaribio la mapinduzi ya serikali Mei mwaka huu Rais Nkurunziza alipokuwa ziarani Tanzania.
    Ikulu ya White House imesema imepokea habari za kuaminika za visa vya watu kukamatwa, kuteswa na kuuawa na vikosi vya usalama pamoja na ukiukaji wa haki unaotekelezwa na magenge ya vijana wenye uhusiano na chama tawala.
    Aidha, wale wanaopinga serikali ya Nkurunziza wamekuwa wakitekeleza mashambulizi dhidi ya wafuasi wa serikali.
    Created by BBC Swahili.


    0 comments:

    Post a Comment