Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akimpongeza Rais wa awamu ya Tano, Dk John Pombe Magufuli.
RAIS John Magufuli ameendelea kupokea salamu za pongezi kutoka kwa
viongozi mbalimbali duniani kutokana na kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, safari hii akiwamo Malkia Elizabeth II
wa Uingereza.
Katika salamu hizo, Malkia Elizabeth II amemueleza Dk Magufuli kuwa,
“Natumaini kuwa uhusiano baina ya nchi hizi mbili ambazo ni wanachama wa
Jumuiya ya Madola yataendelea wakati wa utawala wako, nakutakia heri
pamoja na wananchi wa Tanzania.”
Mwingine aliyemtumia salamu Rais ni Mfalme Akihito wa Japan ambaye
alimueleza Dk Magufuli, “Nakutumia salamu za dhati, mafanikio na furaha
kwako Mheshimiwa Rais na watu wa nchi yako.”
Dk Magufuli pia amepokea salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kiarabu ya Saharawi, Mohamed Abdelaziz aliyemtakia heri
Rais na kumueleza kuwa “Nina imani kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
itaendelea vyema chini ya uongozi wako kuelekea katika kupata maendeleo
na mafanikio zaidi.”
Pia alikipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Watanzania kwa uchaguzi
wa kidemokrasia ulioendeshwa katika mazingira ya kistaarabu chini ya
usimamizi wa waangalizi kutoka kwenye kanda, bara na kimataifa na hivyo
kuliletea sifa Bara la Afrika.
Aidha, amepokea salamu kutoka kwa Rais wa Namibia, Hage Geingob na
kumueleza Rais kuwa salamu zake na zile za wananchi wa Namibia ni za
dhati kwa Serikali na Watanzania kwa ujumla kwa ushindi wa kiti cha
urais.
Salamu kama hizo zimetoka kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye
amesema Tanzania kwa mara nyingine tena imedhihirisha kuwa ni nguzo ya
demokrasia barani Afrika. Naye Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la
Ujerumani, Joachim Gauck alimtakia Dk Magufuli na Watanzania kwa ujumla
mafanikio katika kuendeleza Taifa kwa ujumla.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Monday, 16 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment